Mchango wa Reginald Mengi katika uchumi wa Tanzania

Kati ya habari kuu kuliko zote Tanzania katika wiki ya kwanza ya Mei ni kuhusu kifo cha Reginald Mengi. Hadi anafariki dunia huko Dubai, alikuwa ni mwenyekiti mtendaji wa Kampuni za IPP.

Mengi ameshika nyadhifa nyingi hasa katika sekta binafsi, amekuwa mchangiaji katika shughuli mbalimbali za maendeleo ya nchi kiujumla na kwa baadhi ya makundi kimahususi. Makala haya ni maalumu kwa kumuenzi Mengi kwa kuainisha mchango wake katika uchumi wa Tanzania.

Maendeleo sekta binafsi

Sekta binafsi nchini bado ni changa na inakua katika viwango vya dunia. Hii inachangiwa na siasa ya Ujamaa na Kujitegemea na hasa Azimio la Arusha. Siasa hii ilitamalaki kuanzia mwaka 1967 hadi katikati ya miaka ya 1980.

Hiki ni kipindi ambacho Serikali ilishika hatamu za uchumi. Sekta binafsi kama tunavyoiona na kuifahamu leo ilianza kuzaliwa na kukua katikati ya miaka ya 1980 kufuatia mageuzi makubwa na ya kufika mbali katika uchumi wa Tanzania.

Mengi alikuwa kati ya Watanzania wa kwanza kuikumbatia na kuikuza sekta binafsi. Hii ni sekta iliyotambuliwa rasmi kama injini ya ukuaji wa uchumi na kinara katika uchumi wa soko.

Alikuwa chachu ya wazawa kuanzisha shughuli mbalimbali za kiuchumi katika sekta mbalimbali. Hii inaonekana katika uwekezaji wake katika Kampuni za IPP kikiwamo kiwanda cha Bonite na sekta ya habari.

Kuwa na mtu kama Mengi wakati sekta binafsi inazaliwa Tanzania ilikuwa n muhimu sana kwa ajiili ya kuonyesha njia na mfano wa namna wazawa wanavyoweza kufanya mambo makubwa katika sekta hii.

Mchango wake wa kimaendeleo unaonekana pia kwenye uongozi wake katika Shirikisho la Wenye Viwanda (CTI), Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF), Baraza la Taifa la Biashara (TNBC) na Baraza la Biashara la Afrika Mashariki (EABC).

Hiyo ni baadhi ya mifano ya michango yaMengi katika maendeleo ya sekta binafsi kimahususi na uchumi wa nchi kwa ujumla.

Ujasiriamali

Mchango wa Mengi katika ukuaji na ustawi wa ujasiriamali nchini ni mkubwa. Amechangia kwa vitendo kuonyesha mifano ya namna ya kukuza ujasiriamali ikiwa ni pamoja na kufadhili mashindano ya uandishi wa mawazo ya biashara.

Alionyesha kwa vitendo sifa za wajasiriamali wazuri ambazo ni uthubutu, uvumilivi, ubunifu, kuona fursa na kuzitendea haki, utayari wa kuanzisha, kulea na kukuza biashara, kuwa tayari kupambana na viatarishi na changamoto, uwezo mkubwa wa kutafuta na kuweka pamoja vizalishia maji na kadhalika.

Kwa kufanya hivyo alitia moyo na shime wale wote walio katika sekta ya ujasiriamali. Alionyesha nini kinawezekana pale baadhi walipofikiria haiwezekani.

Ujasiriamali wake na kwa wale waliojifunza na kuvutiwa naye nao wakawa wajasiriamali ni mchango mkubwa katika uchumi wa Tanzania kutokana na umuhimu wa ujasiriamali katika uchumi.

Ajira

Uwekezaji wa Mengi katika sekta mbalimbali kama vile viwanda, habari, madini na kadhalika umechochea kuzalisha na kuongeza ajira kwa wananchi.

Ajira ni kati ya masuala muhimu katika uchumi mkubwa wa nchi yoyote ile, kuongeza ajira ni malengo mapana ya mikakati na sera za maendeleo ya nchi.

Mapato ya Serikali

Mapato ya aina mbalimbali ni muhimu sana katika kuiwezesha Serikali kutoa huduma na bidhaa za umma. Huduma hizi ni pamoja na elimu, afya, maji, ulinzi na usalama na miundombinu ya kiuchumi. Miundombinu hii ni pamoja na barabara, reli, viwanja vya ndege, bandari na vyanzo vya umeme.

Kwa uwekezaji uliofanywa na Mengi ni wazi kuwa kumekuwapo mapato ya kikodi na yasiyo ya kikodi kwa serikali kuu na zile za mitaa.

Fedha za kigeni

Nchi yeyote ile inayoshiriki katika uchumi wa kimataifa kwa maana ya kununua na kuuza bidhaa na huduma nje ya nchi huitaji fedha za kigeni. Uwekezaji wa Mengi umesaidia katika eneo la fedha za kigeni.