Mjasiriamali atengeneza mashine kubaini mayai yatakayototoa vifaranga

Thursday May 9 2019

 

By Aurea Simtowe

Kila biashara huwa na changamoto zake; cha muhimu ni kuwa mvumilivu, kuwajali wateja na kupokea malalamiko yao ili uyafanyie kazi.

Moja kati ya biashara ambazo wateja wamekuwa wakiwalalamikia sana wafanyabiashara wake, ni ya mayai kwa ajili ya kutotolesha vifaranga vya kuku.

Wafanyabiashara wengi wamekuwa wakilalamikiwa kuuza mayai 100 kwa mteja lakini yanapototoleshwa wanapatikana vifaranga 20 au 50.

Hali hiyo, inaweza kusababishwa na mayai ambayo hayafai kutoa vifaranga, lakini wateja hununua bila kujua.

Ili kuondokana na changamoto hiyo, mjasiriamali John Haule amebuni kifaa cha Egg tester kinachowasaidia watotoleshaji kuangalia kama yai linafaa kutotoleshwa na aina ya kuku atakayepatikana.

“Kwa mara ya kwanza nilitumia miezi mitatu kuhakikisha napata kifaa hiki na kila nilipotengeneza nilijua wapi nakosea hadi nilipoweza kutengeneza kitu bora.

Advertisement

“Nilipata ujuzi wa kutengeneza mashine za kutotoleshea kutoka kwa Mjerumani na pia, nilijifunza kutengeneza Egg tester kupitia mitandao ili niweze kuondokana na kesi ya mayai kushindwa kutoa vifaranga,” anasema mjasiriamali huyo.

Anasema kifaa hicho ambacho hukiuza kwa kati ya Sh30,000 hadi 40,000; hukitengenezwa kwa kutumia tochi na vifuniko vya kiyoyozi (air condition) katika gari.

Haule anasema: “Kwa sasa nina uwezo wa kutengeneza hadi vifaa vitano kwa siku, lakini kwa sababu natamani kuwagusa walio na maisha ya chini endapo nikipata wafadhili naweza kutengeneza hadi 100 kwa siku na kuviuza kwa bei ya chini.”

Anasema moja ya malengo yake ni kuwa mfugaji mkubwa wa kuku huku akiamini wafugaji wengine watafanikiwa kupitia vifaa hivyo.

Advertisement