Stella Mutta; msomi aliyejiajiri kwa kuziongezea thamani chupa

Siku hizi suala la kutafuta au kupata ajira rasmi limekuwa ni mtihani, huku wachache ndiyo hufaulu.

Hali hii haijaikumba Tanzania pekee bali ni janga la kimataifa.

Baadhi ya kampuni zimekuwa zikilalamika kwamba muitikio wa kibiashara hauendani ya hali ya uchumi kwa sasa.

Hata hivyo, Stella Mutta (31), suala la ajira kwake si changamoto kubwa kwa sababu ameamua kujiajiri.

Mhitimu huyo wa shahada ya kwanza kutoka Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE), Dodoma anasema baada ya kumaliza masomo yake hayo alikuwa anafahamu vizuri kwamba kupata ajira ya kuajiriwa siyo jambo rahisi licha ya kufaulu vizuri masomo yake.

“Nilimaliza chuo mwaka 2010. Tangu hapo niliweza kupata ajira za muda mfupi na hatimaye nikaamua kuanzisha kitu changu binafsi,” anasimulia Mutta.

Baada ya kufanya kazi za muda mfupi ikiwamo ya uhasibu kwenye asasi za kiraia na nyumba za starehe zinazouza vinywaji aliamua kufanya kitu tofauti na ajira yake.

Anasema wakati akiwa mhasibu kwenye maeneo ya vinywaji, alikuwa akihifadhi chupa na kuwauzia watu waliokuwa wakizihitaji kwa bei ya maelewano. “Kila Ijumaa jioni nilikuwa tayari nimeweza kufanikiwa kukusanya zaidi ya chupa 200 za vinywaji mbalimbali na nilikuwa na watu wa kuzichukua, maana bosi wangu hakuzihitaji tena,” anasimulia Mutta.

Pia, anasema chupa moja tupu alikuwa anaiuza kati ya Sh1,000 hadi Sh4,000 ikitegemea na muonekano wake.

Mwaka 2016 aliamua kufuatilia matumizi ya chupa alizoziuza na kubaini kuwa wateja wake wote walionunua chupa zile walikuwa ni mawakala wa watu wengine ambao ndiyo wao waliokuwa wahitaji na watumiaji wakubwa.

“Baadhi ya watumiaji hao walihifadhia vinywaji vya kawaida ndani na hatimaye kuviuza mitaani. Bila shaka vinywaji hivyo havikuwa na ubora unaotakiwa,” anasema.

Mama huyo wa watoto wawili wa Ethan na Owen, anasema kazi ya kuajiriwa ilimwelemea kwa kuwa hakupata kile alichokikusudia mwisho wa mwezi.

“Licha ya kuwa na mshahara mdogo, sikuwa na uhakika wa kuupata kwa wakati uliotakiwa,” anasema.

Mwishoni mwa mwaka 2017 aliamua kuacha kazi ya kuajiriwa.

Anasema katika pitapita zake katikati ya jiji la Mwanza, alibahatika kuingia kwenye duka la bidhaa za maua na kuona yakiwa yametengenezwa kwa vifaa mbalimbali zikiwamo mbao na karatasi.

Mutta anasema hapo ndipo alitambua kwamba anaweza akaigizilia alichokiona pale dukani na kukitengeneza hata kama si kwa ubora ule.

Kwa kuwa alikuwa na uhusiano mzuri na baadhi ya watu aliowahi kufanya nao kazi, aliwaomba kumsaidia chupa chache ili ajaribu kutengeneza alichokuwa amekiona.

“Nilichukua chupa za dompo, savanna na pia Robertson. Kwa fedha kidogo nilizokuwa nimejitunzia, nilinunua baadhi ya vifaa kama vile saruji, nyembe maalumu na rangi za kupaka na kuchora maua kwenye zile chupa,” anasema Mutta

Baada ya kumaliza kurembesha chupa hizo, hakutaka kuziuza ila aliamua kuzigawa kwa marafiki zake ili wampe ushauri wa namna ya kuboresha kazi yake hiyo mpya.

Anaeleza kwamba kati ya marafiki wake hao, wote walipenda kazi ile, hali iliyompa moyo na kumtia nguvu ya zaidi ya kufanya hiyo kazi.

Mutta anasema kadri siku zilivyoenda ndivyo alivyaonza kubobea kwa kutengeneza na kurembesha maua, kazi yake hiyo inaitwa Flower Vases.

Mhasibu huyo anasema kwamba hadi kufikia Juni 2018 alikuwa amepata ofisi ya kutengeneza bidhaa hizo.

Mauzo na wateja

Mutta anaweka wazi kwamba, angejua asingepoteza muda wake kutafuta kazi nyingine kwa kuwa urembeshaji wa chupa na kuzigeuza kuwa maua umempa kipato kikubwa.

Anasema kipato anachopata kinamtosha kufanya vitu vingi ikiwamo kulisha familia na kuwasomesha wadogo zake.

Asilimia kubwa ya wateja wake ni wamiliki wa hoteli na ofisi za Serikali.

Anasema anaweza kuchora nembo ya kitu chochote au kuandika jina katika chupa na ikaonekana vizuri kutegemea na namna mteja anavyotaka.

Mutta anasema kuna wale wanaohitaji chupa zake kwa ajili ya mapambo ya ndani, “kwa mfano ukitaka niandike jina la mtoto wako naweza.”

Bei ya chupa zake hizo inategemea na namna alivyozipamba au uhitaji wa mteja.

“Kwa mfano, chupa moja ya Roberson yenye kitako kipana, naiuza kati ya Sh30,000 hadi 50,000 kutokana na ubunifu niliouweka,” anasema Mutta.

Kutokana na kazi hiyo anasema ameweza kufungua akaunti ya kibishara ya Starshinetz ambayo ipo kwenye mitandao ya kijamii.

“Ni watu wachache sana wanaamini kwamba hizi bidhaa nazitengeneza kwa mikono yangu. Kuna wanaofikiri naagiza labda na kuanza kuuza, kitu ambacho sio kweli,” anasema Mutta.

Kwa sasa mjasiriamali huyo ameweza kutoa ajira kwa zaidi ya vijana sita ambao wote wana uhakika wa kupata mshahara mwishoni mwa mwezi.