Mafuta ya alizeti yanavyowapa ulaji wahitimu wa chuo

Kutokana na kuongezeka kwa msukumo wa vijana hasa wahitimu wa vyuo vikuu kuchangamkia fursa zilizopo kwenye sekta mbalimbali, baadhi yao wameanza kuitikia wito hivyo kumudu kuendesha maisha yao.

Hamasa hiyo, imewashawishi vijana watatu kuungana na kuanzisha kampuni ijukanayo kama Asili Group inayouza mafuta ya alizeti tangu Juni mwaka jana.

Waasisi wa kampuni hiyo ni George Lyatuu (Udom), Issa Jabiri (Chuo Kikuu cha Ardhi) na Joshua Mlelwa (Chuo Kikuu cha Ruaha) ambao walianza biashara hiyo wakiwa na mtaji wa Sh600,000 tu.

“Tulichagua mafuta kwa sababu ni kitu ambacho ni lazima kitumiwe kila siku katika mapishi ya nyumbani na hakuna namna mtu anavyoweza kuyakwepa kwa zaidi ya siku mbili,” anasema Lyatuu.

Kwa mtaji waliokuwa nao, walitumia nusu kununua madumu sita ya lita 20 ambayo kila moja liliwagharimu Sh60,000. Baadaye, Lyatuu anasema waliyajaza kwenye madumu ya lita tano tano na kuyauza kwa Sh20,000 kila moja.

“Mwanzo tulikuwa tunachukua madumu 10 kwa mwezi lakini sasa hivi tunanunua kila baada ya wiki mbili kutokana na uhitaji wa soko letu,” anasema Lyatuu.

Anasema kuna soko kubwa ambalo hawawezi kulimaliza kwani mtaji wao ambao sasa umefika Sh900,000 bado ni mdogo ingawa wanakusudia kuwa na stoo kubwa sehemu mbalimbali za Jiji la Dar es Salaam ili kupunguza gharama za kuwapelekea wateja.