Breaking News

Tanesco inapoteza fursa ya kukusanya mabilioni

Thursday March 7 2019

 

By Kelvin Matandiko, Mwananchi [email protected]

Licha ya mikakati mizuri liliyojiwekea, Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) linapoteza mabilioni ya mapato ambayo yangeliwezesha kufanikisha mipango yake kutoka migodini.

Tathmini iliyofanywa na gazeti hili kwenye migodi miwili ya Biharamulo na Geita imebaini hilo, jambo ambalo wataalamu wa masuala ya uchumi na uwekezaji wanasema ni fursa inayopotezwa bila sababu za msingi.

Tangu ulipoanza uchimbaji wa dhahabu mwaka 2001, Mgodi wa Geita (GGM) unatumia umeme unaozalishwa kutokana na mafuta.

Taarifa ya kampuni ya Anglogold Ashanti inayoendesha mgodi huo, inaonyesha kuanzia Januari hadi Desemba mwaka jana, ilitumia zaidi ya lita milioni 4.1 za dizeli kuzalisha megawati 35 ikitumia Sh8 bilioni kila mwezi.

“Ni gharama zaidi ikilinganishwa na umeme wa gridi ya Taifa. Mtambo wa kuzalishia umeme unagharimu Sh519.61 kwa kilowati moja ikilinganishwa na Sh159 ya umeme wa gridi,” inasomeka taarifa ya kampuni hiyo.

Kwa hesabu hiyo, Mgodi wa Geita ulitumia Sh8 bilioni kila mwezi sawa na Sh96 bilioni mwaka jana kuzalisha umeme fursa ambayo endapo Tanesco ingepeleka umeme ingeweza kuingiza Sh31.2 bilioni.

Advertisement

“Shughuli za uzalishaji zinahitaji umeme wa uhakika kwa saa 24 kufanikisha utekelezaji wa mipango ya uendeshaji wa mgodi. Mwaka 2000 hakukuwa na gridi ya Taifa mkoani Geita,” inasomeka taarifa ya mgodi huo.

Uchambuzi wa hesabu za Mgodi wa Biharamulo unaonyesha Tanesco ingeingiza Sh350 milioni kila mwezi sawa na Sh16.8 bilioni kwa miaka minne kwa huduma ya umeme kuanzia mwaka 2014.

Mgodi huo uliopo wilayani Biharamulo mkoani Kagera ulikuwa unatumia wastani wa Sh900 milioni kununua lita 360,000 za dizeli kila mwezi.

Mratibu wa shughuli za uboreshaji biashara wa mgodi wa Stamigold, Godfrey Rweyemamu anasema mgodi huo ungepunguza wastani wa asilimia 60 ya gharama za umeme ndani ya miaka hiyo minne.

“Sh550 milioni ambazo zingeokolewa kwa matumizi ya umeme wa gridi ya Taifa zingesaidia kuongeza mtaji wa kampuni,” anasema Rweyemamu.

Msemaji wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura), Titus Kaguo anasema hali hii inatoa fursa kubwa kwa Tanesco kufanya biashara ya umeme kwenye migodi.

Mkurugenzi mtendaji msaidizi wa Tanesco anayeshughulikia uwekezaji na miradi, Khalidi James anasema uchelewashaji wa gridi ya Taifa katika maeneo ya migodi kadhaa kumechangiwa na ukosefu wa miundombinu.

Anasema siku chache zijazo wanatarajia kuanza kusambaza umeme kutoka Bulyanhulu hadi Geita umbali wa kilometa 55 kusafirisha megawati 460 ambazo kati yake, megawati 80 zitatengwa kwa ajili ya Mkoa wa Geita ikiwamo GGML.

Maandalizi ya mradi huo wa Dola 23 milioni maandalizi yake yamekamilika na utaanza wakati wowote.

Mwenyekiti wa bodi ya wakurugenzi wa Tanesco, Dk Alexander Kyaruzi anasema shirika hilo linatamani kufikisha huduma kwa kampuni na Watanzania wote lakini linakabiliwa na uhaba wa bajeti kufanikisha miradi mikubwa.

Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo anasema wizara yake ilipobaini changamoto hiyo iliwasiliana na wizara ya nishati ili Tanesco ipeleke umeme katika migodi hiyo.

“Kuna mawasiliano ya ndani yanaendelea na siyo kwa migodi mikubwa tu hata wachimbaji wadogo wanahitaji umeme wa Tanesco, kwa hiyo ni changamoto ambayo inaathiri hata mapato ya Serikali,” anasema.

Pamoja na kukosekana kwa fursa hiyo ya Tanesco, mkurugenzi mkazi kanda ya Afrika wa Shirika la Usimamizi wa Rasilimali za Asili (NRGI), Silas Olang’ anasema licha ya kuongeza gharama kwa mgodi, matumizi ya mafuta yanaathiri mapato ya Serikali pia.

Advertisement