Wataalamu Bakita wakoleza mjadala wa lugha ya kufundishia

Siku chache baada ya msomi nguli wa elimu nchini Profesa Issa Omari kuibua tena hoja ya lugha inayofaa kufundishi shuleni, Baraza la Kiswahili Tanzania (Bakita) limesema bado Kiswahili kina umuhimu na sifa za kutumika shuleni.

Akizungumza katika mahojiano maalumu na Mwananchi, Profesa Omari alisema haoni sababu wala haja ya Tanzania kutumia lugha ya Kiswahili na kwamba matumizi yake hayataboresha sekta ya elimu.

Kinyume chake alisema Tanzania ijiandae kuwa na wasomi watakaokosa ajira ndani ya ukanda wa Afrika Mashariki na duniani kwa jumla.

Wakizungumzia kauli hiyo, wataalamu wa Kiswahili kutoka Bakita wanasema sio tu Kiswahili kina sifa za kitaaluma, lakini hata mazingira yanaonyesha kuwa tayari nchi ipo tayari kukitumia kama lugha ya kufundishia.

Mchunguzi wa lugha kutoka Bakita, Ambrose Mghanga anasema kuwa nchi ipo tayari kutumia lugha ya Kiswahili kufundishia, ila ni mchakato unaohitaji tamko.

Anasema inawezekana kwa Serikali kutoa tamko rasmi kama ilivyofanya mwaka 1968 kwa kuzitaka shule zifundishe lugha ya Kiswahili kipindi ambacho jamii nyingi zilikuwa zikitumia lugha za makabila.

“Ikiwa kwa tamko hilo kutoka kutumia lugha za makabila mbalimbali, Kiswahili kilipenya na kuzungumzwa kote Tanzania, sioni ugumu wowote; yanahitajika maandalizi kidogo tu, kulikamilisha hilo, ”anasema Mghanga.

Anasema kinachofanyika sasa ni kujihadaa wenyewe kwa kuendelea kutumia Kiingereza kama lugha ya kufundishia, ilihali walimu hadi vyuoni kuna nyakati wanatoa ufafanuzi kwa Kiswahili kwa sababu wao nao hawakijui vizuri Kiingereza.

Vitabu vipo

Mtaalamu mwingine kutoka Bakita, Musa Kaoneka anasema kuna utafiti mwingi unaoonyesha kuwa ili mwanafunzi amuelewe mwalimu na apate maarifa, anatakiwa kufundishwa kwa lugha anayoielewa.

Anasema kilichopo sasa katika shule nchini ni kuwa walimu hawajui Kiingereza, wala Kiswahili na bado wanalazimisha kukitumia.

“Mimi nilikuwa mwalimu, nimewahi kumshuhudia mwalimu akiwadanganya wanafunzi darasani; hii inatokana na kutotulia katika kutumia lugha moja,”anasema Kaoneka anayefanya kazi ya uchunguzi wa lugha.

Kuhusu madai kuwa Kiswahili hakina vitabu vya kutosha hasa katika masomo ya sayansi, Mghanga anasema tayari wameshajitokeza watunzi walioanza kutafsiri vitabu.

‘’Kiputiputi (jina la mwandishi) ametafsiri vitabu vya masomo ya Kemia, Fizikia na kamusi ya Tehama kwa lugha ya Kiswahili; hii yote inaonyesha utayari uliopo, ”anasema Mghanga na kuongeza kuwa hata Tanzania ya viwanda inahitaji zaidi watu wenye weledi na sio wanaojua Kiingereza.

‘’Kwa mfano, wakati huu tunapokwenda kwenye uchumi wa viwanda, hakutahitajika Kiingereza zaidi ya weledi wa kazi, hivyo suala la kuwajenga wanafunzi kimaarifa liwe na mawanda mapana, ”anasema.

Kwa nini lugha zote zisitumike?

Wapo wanaopigia chapuo matumizi ya lugha zote mbili na hata Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014 inasisitiza hilo. Hata hivyo, Kaonekana anasema kama kuna haja ya kufundisha lugha zote mbili, hakuna budi wapatikane walimu wa Kiingereza wanaokijua fika.

Anasema kwa sasa wanafunzi wanadanganywa sana kwenye Kiingereza tena kwenye vitu vidogo kama miundo ya sentensi.

“Huo ni mkanganyiko ambao mimi sikubaliani nao, uchaguzi huo ndiyo unatufanya tufikie hapa tulipo. Imeaminishwa mwanafunzi anayezungumza Kiingereza ndiyo amesoma na kupata elimu bora, jambo ambalo siliafiki, ”anaeleza.

Kwa upande wake, Mnghaga hakubaliani na hoja ya lugha mbili, anaishauri Serikali kubaki na lugha moja kwa sababu kuhama hama kunawahangaisha watoto kitaaluma.

“Watoto wanahangaika, hatuko wa moto wala baridi, ibaki moja nayo ni Kiswahili. Kiingereza kibaki kama somo watakaobobea huko watakuwa wataalamu na wakalimani,” anasema.

Kiswahili kimekua

Mnghaga anasema kielimu lugha ya Kiswahili imekuwa kwa kiwango kikubwa.

Anasema zamani ilikuwa inatolewa elimu kwa ngazi ya cheti, lakini sasa imefikia ngazi ya shahada ya uzamivu.

Anasema kulikuwa na kamusi moja ya Kiswahili – Kiingereza, lakini sasa zipo zaidi ya 39 katika nyanja mbalimbali, huku pia akisifu kuwapo kwa vyombo vingi vya habari vinavyotumia lugha ya Kiswahili.

“Mafanikio ni makubwa kwa kweli hata orodha ya lugha duniani inalionyesha hilo ambapo Kiswahili kinashika namba 10. Ukumbuke kukua kwa lugha kunategemea wingi wa watu, kadri watu wetu wanavyotawanyika duniani na Kiswahili kinakua,” anasema.

‘‘Baadhi ya nchi zinafundisha Kiswahili kama vile Ujerumani, Marekani na Korea. Kuna vyuo zaidi ya 200 nje ya nchi vinafundisha lugha hiyo , huku 50 vikiwa nchini Marekani pekee.’’

Mbali na hilo anasema kuna redio zaidi ya 100 zinazorusha matangazo kwa lugha ya Kiswahili zikiwamo za Nigeria, Umoja wa Mataifa, Redio Iran na China.