ANTI BETTIE: Ananipenda japo ana mke, je ni sahihi kusubiri waachane ili anioe?

Sunday March 22 2020

 

Anti kuna mwanaume napendana naye sana, kila mmoja hataki na hayupo tayari kumpoteza mwenzake. Lakini mwanaume huyu ameoa na ana mtoto mmoja, ila ndoa yao ina mgogoro wa muda mrefu. Je, wakiachana akinioa nitakuwa nimekosea?

Umekaa unaiombea ndoa ya wenzako dua mbaya waachane ili uolewe, huoni kama unafanya jambo baya na la kupingwa. Kibaya zaidi wenzako wana mtoto, wakiachana wa kwanza kuathirika ni mtoto wao kwa kukosa mapenzi ya baba na mama. Japo sina uhakika, ila nahisi hata huo mgogoro wewe unaukoleza ili kutimiza azma yako ya kuolewa na mume wa mwenzako.

Siku zote mnaambiwa mume wa mtu sumu, wewe unakaza buti ukijipangia mipango mikubwa ya kufunga naye ndoa.

Tuliza akili na ufikirie mara mbili, kama anaachana na mkewe kwa ajili yako, huoni kama anaweza kukuacha na wewe. Kwanza hana adabu anakushirikisha migogoro yake na mkewe , ili iweje?

Mhurumie mwenzako na utamsaidia sana iwapo utaachana na mumewe, inawezekana uwepo wako unampa jeuri ya kutojali kuwapo kwa mgogoro kati yake na mkewe.

Chukua hatua kabla hujaingia katika matatizo ya kujitakia, waache waachane kwa yao na usiwe kati kati ya mgogoro wao.

Advertisement

Natafuta mchumba ambaye hajawahi kujamiiana

Habari. Nimetafuta mchumba ninayemtaka kwa miaka mitatu sasa bila mafanikio. Lengo langu ni kufunga ndoa na mwanamke nitakayemkuta hajaanza uhusiano, ambaye kwa kipindi chote cha maisha yangu sasa nina miaka 32 sijawahi kukutana naye licha ya kuwa na mahusiano na wasichana wengi nikidhani kuna siku nitabahatisha lakini sijafanikiwa.

Nifanyeje?

Kwa hadithi yako hii isiyovutia unachokitafuta sasa ni maradhi na si mke wa kuoa. Miaka mitatu unatumia kutafuta mke wa kuoa kwa kujaribu huyu na yule kutafuta ambaye hajashiriki tendo, sijui kama unatumia akili hii ya kawaida au una tatizo lisilo la kawaida kichwani. Tafadhali usiwadhalilishe wanawake, hicho unachokitafuta mbona wewe huna, maana ungekuwa nacho kwanza ndiyo utamani na wengine wakitunze. Kama wewe uliamua kuanza na wao walifanya kama ulivyofanya. Mke mwema, bora na mwenye hekima haangaliwi ameshiriki mara ngapi jambo hilo, huangaliwa tabia zake. Je, kama alikutana na mwanaume mwenye tabia kama zako za kujaribu jaribu akidhani amepata, bila shaka angekuwa miongoni mwa unaowaona hawafai, kumbe alikutana na mtu mwenye tabia mbaya.

Nimekujibu kwa faida ya wengine, tofauti na hapo umenikera sana kwa swali lako la ajabu ambalo limepitwa na wakati, wala hakuna anayelifikiria katika karne hii zaidi yako.

Unajua kuna wanawake hawajawahi kushiriki tendo la ndoa na hicho unachokitafuta hawana, kimetoka kwa sababu mbalimbali je, nao waonjwe na kuachwa?

Jitulize na kabla hujauliza jifikirie mara mbili unataka kuuliza nini, hili suala linahitaji akili ya kawaida tu, kulijua kama halifai.

Advertisement