TUONGEE KIUME: Mama wa mkeo anatamani mkwe ‘mapesa’ zaidi yako

Sunday January 26 2020

 

By Kelvin Kagambo

Ukiwa baba huwa unatamani kuwa na mtoto bora kuliko baba wote duniani. Mtoto ambaye kila linapozungumzwa jambo zuri basi yeye ndio awe amelifanya.

Habari za ‘mabangi’, vigodoro, mapepe, kutatarika na takataka zote zenye kuchafua taswira ya familia zifanywe na watoto wa jirani ila wako awe na desturi za kufanana na malaika kabisa.

Kisayansi hii haiitwi roho mbaya, yaani kutaka sifa mbaya ziwe za watoto wa wenzako tu, ni sahihi kabisa, kwa sababu ili ubora wa mwanao uonekane kwa urahisi ni lazima kuwe na jirani mwenye mtoto pasua kichwa ili wakati upuuzi wake unazungumziwa, uongelewe kupitia mazuri ya mwanao.

Lakini katika yote ni muhimu kufahamu kwamba wewe na jirani yako mnafanana mioyo, yaani wote dua zenu ni moja, wakati wewe unaomba kuwa na mtoto kichwa darasani, naye anakesha akiomba mwanae awe namba moja kila siku kwenye mitihani ambayo mwanao anaburuza mkia. Na kwa msingi huo basi ili dua ya mmoja ipokelewe ni lazima ya mwingine ipigwe chini na ubaya ni kwamba inaweza kutokea dua yako ndiyo ikashindwa kufika hata ‘mbingu ya tatu’.

Dua yako ikikataliwa ndiyo utaanza kuona mwanao haeleweki tangu akiwa vidudu, wakati wenzake wanarudi na vyema za mwalimu, yeye ana rudi na madudu tu yasiyoeleweka na mbaya zaidi unaona waziwazi kwamba hana dalili ya kubadilika kuwa bora kwa namna unavyohitaji.

Kama wazazi mara nyingi tunakumbwa na mihemko. Unapogundua mwanao si wa aina unayotamani awe unakuwa mtu wa kumrudi isivyotakiwa. Mtoto akikosea kidogo unakuwa mbogo, kama si kumtia kibano basi utamshushia maneno ya kumfanya ajihisi kilaza wa kiwango cha juu duniani.

Advertisement

Tunakosea zaidi kuwakosoa watoto wetu kwa kuwafanisha na wengine, kuwadhihirishia kwamba ili wawe bora ni lazima wafanane na watoto fulani. Labda ni kitu kizuri kwa sababu kinawapa mfano rahisi na halisi wa kujua vile unavyopenda kumuona, lakini amini usiamini, hakuna kitu kinachomuumiza binadamu mwenye mwili wenye mifupa na damu kama kufanyiwa kipimo na mtu ambaye anajua kabisa yuko juu zaidi yake na huenda si rahisi kumfikia.

Kwa mfano kuna kituko kilimtokea jamaa yetu, yeye ana gari ya kutembelea hizi ndogo ndogo ‘majuzi’ alikuwa na safari ya kumrejesha nyumbani mama mkwe wake aliyewatembelea.

Wakiwa njiani, yeye, mkewe na mama mkwe wake, ghafla nyuma yao ikatokea gari aina ya Range Rover Sport na kuwapita kwa kasi, na haikuisha hata dakika moja ikawapotea kabisa. Basi mama mkwe akajikuta ameropoka kwa sauti eti: “Aaah! Mwanaume huyo amepita.”

Tunavyomjua jamaa yetu si mtu wa kuchukia vitu vidogo vidogo lakini naamini siku hiyo alikasirika na huenda ilibaki kidogo tu asimamishe gari amteremshe mkwewe, safari iishie pale.

Sasa ikiwa kwa mtu mzima inachoma hivyo, vipi tunapofanyia watoto wetu na kuwalazimisha wawe kama fulani bila kuchunguza kujua waliumbwa ili wawe nani?

Advertisement