ANTI BETTIE: Mwanamke wangu kama baunsa kitu kidogo anataka kunitwanga - VIDEO

Sunday September 15 2019

 

Ninaishi na mwanamke huu ni mwezi wa sita, lakini kila tunapokwaruzana huwa anatishia kunipiga na silaha mbalimbali ikiwamo samani za ndani.

Je, anafaa kuwa mke?

Unataka kuoa baunsa wa nini? Kwa nini unaishi na mwanamke bila kumuoa kwa mfano akikuumiza utampata wapi au yeye ukimuumiza kwenye hayo malumbano utaanzia wapi kujitetea?

Anakutishia kukupiga kwa sababu haoni umuhimu wako na pengine ana hasira anaona unaishi naye na huna mpango wa kumuoa.

Nakushauri kama unataka kufanya naye maisha, mwambie aache hiyo tabia na akiendelea baada ya kumueleza athari za kufanya hivyo achana naye. Mapenzi ni raha, kubembelezana, kudekezana, kuelekezana mnapotofautiana na si kutishia kupigana tena na silaha. Kuwa makini na uchukue hatua mapema, mzaha mzaha siku zote hutumbua usaha.

Hanipi nafasi, ananihukumu kwa kila jambo

Advertisement

Mume wangu hanipi nafasi ya kunisikiliza, kiasi kwamba ananihukumu kwa kila jambo.

Nifanyeje?

Nafasi ya kusikilizwa wewe ndiyo unaitengeneza. Usikubali kukandamizwa na usiwe kiburi, kilichotokea ulishindwa kutengeneza nafasi hiyo tangu mlipooana na sasa inakuwa ngumu kwa sababu mumeo ameshazoea kukuhukumu bila kukupa nafasi ya kujitetea.

Unachotakiwa kufanya sasa ni kuidai kwa kufuata hatua na unyeyekevu kama mke anavyotakiwa kufanya. Muombe kuzungumza naye mara mbili au tatu, akikataa wafuate jamaa zake anaowaheshimu wawili au watatu uwaeleze namna jambo hilo linavyoitafuna ndoa yenu. Kwa bahati akikubali kuzungumza na wewe mweleze ni kwa namna gani unaumizwa na tabia yake ya kutokupa nafasi ya kujieleza au kukusikiliza katika kila jambo.

Mweleze namna ambavyo hamtapiga hatua kwa sababu hasikilizi mawazo yako, hamtawalea watoto kwa ushirikiano na kupata matokeo chanya kwa sababu hakusikilizi na hakupi nafasi ya kutoa maoni yako kama mke.

Uwezo hauniruhusu kuwa na watoto wengi

Nimezaa na mke wangu watoto watatu, wawili wakiwa pacha. Kutokana na hali ya maisha na kipato changu sitaki kuongeza wengine. Lakini mwenza wangu anang’ang’ania tuongeze watoto wengine wawili.

Sikatai kuongeza watoto, ila hofu yangu ni kushindwa kuwahudumia ipasavyo ikiwamo kuwapa elimu bora. Nifanyeje?

Kwanza nikupongeze kwa kutambua haki ya watoto, kupata huduma na kujipima uwezo wako kabla ya kuwajaza wakakushinda na kugeuka ongezeko la watoto wa mitaani.

Suala lako linajadilika na iwapo hautafikia muafaka na mwenza wako ni rahisi kukutegea akapata mimba, hivyo kaa naye mpe sababu za kina siyo juu juu. Unaweza kumuomba mtoke, muende sehemu tofauti na nyumbani, ikiwezekana mnunulie anachopenda kisha mfanye majadiliano kuhusu suala hilo.

Kinachomtenganisha mwanamke na mwanaume kama hana shida yoyote ya kimwili ni kuzaa, hivyo anachoking’ang’ania ana haki nacho unachotakiwa ni kumuelewesha hadi akuelewe.

Ukifanikiwa kumshawishi nenda naye kwa mshauri wa masuala ya uzazi wa mpango ili awashauri kwa pamoja njia bora za kutumia kuzuia kupata mimba. Onyesha uanaume wako hapa kwa kujenga hoja bila kuwa mkali, hapo mtafikia mwafaka wa suala hilo.

Advertisement