ANTI BETTIE: Natamani aniache, harufu ya pombe anazokunywa inanishinda

Sunday April 12 2020

Habari!

Nimeolewa huu mwaka wa pili, lakini sina raha na ndoa yangu. Mume wangu kila siku lazima anywe pombe nami harufu yake inanikera. Nimesema naye lakini hanisikii, kwa mwendo huu siwezi kuvumilia.

Nishauri nifanyeje?

Hujaniambia kama ameanza kunywa pombe ghafla, bila shaka tangu anakutokea alikuwa anakunywa.

Inawezekana kuna mabadiliko ya matumizi yake ya pombe, kutoka unywaji sasa amekuwa mlevi badala ya mnywaji kama huko nyuma. Unachonishangaza kukerwa na harufu ambayo hutoka katika kinywa cha yeyote kati ya wawili wanaotumia pombe, mlevi na mnywaji.

Hujanishawishi, labda useme sababu nyingine ya kushindwana na mumeo si harufu ya pombe, naamini alikuwa anakunywa kabla hajakuoa.

Advertisement

Tena anayetumia pombe wakati mwingine ili akupange vizuri umuelewe lazima alikuwa anapitia mahali anapata kidogo ndiyo anakuja kuzungumza nawe au kukutoa kwa ajili ya matembezi.

Kama ulimvumilia wakati wa uchumba hukukemea nasikitika kukwambia unalo hilo. Ulipaswa kumwambia tangu mapema kuwa hupendi harufu ya pombe kama anakupenda labda angeacha, lakini upo katika ndoa naye kwa miaka miwili iweje sasa useme unataka kuachika kwa sababu ya harufu ya pombe? . Vumilia huku ukiendelea kumsihi aache pombe.

Kwa nini sipati mimba?

Niliwahi kupata mimba mwaka 2013, kwa bahati mbaya ikatoka na nikasafishwa. Cha ajabu hadi leo sijapata nyingine.

Je, inawezekana nina tatizo?

Pole sana kwa kuharibu mimba japo miaka mingi imepita. Suala lako ni la kitaalamu na hakuna anayejua zaidi ya vipimo vya kitabibu.

Nenda hospitali kaonane na daktari bingwa wa masuala ya kina mama hususani ya uzazi atakupa ushauri wa kitaalamu na vipimo gani upime kubaini tatizo lako. Majibu ndiyo yatatoa mwanga wa nini cha kufanya.

Rafiki yake ananivutia zaidi

Nilikuwa na uhusiano na binti fulani, lakini siku moja alikuja na rafiki yake nikampenda zaidi. Siku niliyomwambia kuwa nampenda alinitukana na kuniita malaya.

Lakini kutoka moyoni akinikubali ninamuoa ana vigezo nilivyokuwa navitafuta ambavyo rafiki yake niliyekuwa katika mahusiano naye hana.

Nifanyeje?

Zungumza kwa nguvu hiki ulichoniuliza halafu ujisikilize usike unavyouliza vitu vya ajabu. Umeanzisha uhusiano na mtu usiyekuwa na haja naye lakini ulitaka kutimiza haja zako za kimwili na ndiyo maana alipokuja na rafiki yake bila kumjua ukampenda kwa madai yako, lakini kwa namna ulivyouliza swali lako hata yeye hujampenda unamtamani tu.

Kuwa makini na tabia zako, fanya uamuzi sahihi na uache kuwachonganisha wasichana.

Kwa tabia yako hiyo tayari umeshatengeneza uhasama kati ya marafiki hao, licha ya kuwa uliyemtamani ameonyesha msimamo.

Majina yote aliyokuita amepatia kwa sababu unastahili hilo kutokana na tabia yako. Tulia wasichana wapo wengi kama unataka kuoa utampata mwenye sifa unazotaka na siyo kuwamaliza kwa kigezo cha kumtafuta umtakaye.

Advertisement