Breaking News

Kilimo cha mbogamboga kilivyowatoa wasomi wa chuo kikuu

Saturday May 25 2019

 

By Hadija Jumanne, Mwananchi [email protected]

“Mimi na dada yangu, tuliamini kilimo kinalipa, ndio maana baada ya kuhitimu chuo kikuu, hatukutaka kuajiriwa na badala yake tumeamua kijiajiri kwa kuanzisha kilimo cha spinachi na chainizi” anasema Ngiye Nyabakari.

Ngiye na mdogo wake, Bambala Nyabakari, wameamua kujikita katika kilimo kwa kulima kisasa wakitumia Banda kitalu au Nyumba kitalu (green house).

“Nilipomaliza chuo, ajira ilikuwa tatizo kama unavyofahamu vijana wengi tunatamani kuajiriwa na sio kujiajiri, lakini mimi nilikuwa na mawazo tofauti, nilitamani kujiajiri na sio kuajiriwa,” anasema Ngiye ambaye ana shahada ya Biashara na Utawala, aliyoipata mwaka 2015 kutoka Chuo Kikuu cha Bangalore, nchini India.

Anasema baada ya kuhitimu shahada hiyo India, alirudi Tanzania na wakati wote akiwa nchini alijiuliza anaenda kutafuta kazi gani na wapi?

Ngiye anasema baada ya kurudi nchini alimkuta mdogo wake Bambala, naye amemaliza Shahada ya Uhandisi katika Chuo Kikuu cha St Joseph kampasi ya Dar es Salaam.

Anasema baada ya mdogo wake kumaliza masomo, waliamua kumuomba baba yao mtaji kwa ajili ya kuanzisha kilimo cha mbogamboga.

Advertisement

“Bahati nzuri kabla ya kuanza kilimo, tulipata taarifa kuwa kuna kampuni moja ya kimataifa iitwayo Greenhouse Ltd, inaendesha mafunzo ya ujasiriamali kwa vijana, hivyo tukaenda katika mafunzo hayo na baadaye tuliamua kuanzisha kilimo cha kisasa cha shamba darasa,” anasema.

Anabainisha kuwa kampuni ya Greehouse, iliwajengea banda kitalu nyumbani kwao, Mbezi Beach na kuanza kulima kilimo hicho, Juni 2018.

Anasema kilimo hicho sasa kinawaingizia zaidi ya Sh4.9 milioni kwa mwezi.

“Kitu kilichotuvutia ni kwamba kampuni hii ya Greenhouse Ltd, ndio imebeba jukumu la kutafuta soko, mkulima huhitaji kuumiza kichwa wapi utauza mboga zako, wao wananunua mboga hizo na kutafuta wateja” anasema Ngiye.

Wakati Ngiye akieleza hayo, mdogo wake Bambala anasema malengo yao ni kuhakikisha kuwa wanatengeneza nyumba kitalu nyingi kadri wawezavyo ili kufika walikokusudia.

Mabinti hao wamewekeza zaidi ya Sh20 milioni katika kilimo cha mbogamboga kwenye eneo hilo na kwamba baada ya kuvuna mboga hizo, wanatarajia kulima nyanya boga (pilipili hoho).

Wanasema kiasi hicho cha fedha kimetumika katika ujenzi wa green house, uandaaji shamba, ulimaji wenyewe, dawa za kuzuia wadudu na kumlipa mtaalamu wa kilimo.

“Uzuri ni kwamba ujenzi wa kitalu nyumba unaweza kudumu kwa miaka zaidi ya saba bila kubadilisha, ukiona kuna sehemu imeharibika unatengeneza, palipoharibika unabadilisha, ukiona ‘neti’ imeharibika unatengeneza. Ukishajenga green house utalima kila unachotaka,” anasema Ngiye.

Ulimaji na uchumaji wa spinachi

Mtaalamu wa masuala ya kilimo, Isack Mgallah anasema tuta moja la spinachi linakuwa na miche 300 na hutengeneza Sh80,000 kwa mchumo mmoja.

Mgallah ambaye pia ni bwanashamba anayesimamia shamba la mabinti hao, anasema spinachi zinazolimwa kwa njia ya kisasa ya kutumia kitalu banda, hudumu kwa zaidi ya miezi minne na baada ya hapo mkulima anaweza kubadilisha kwa kulima zao lingine.

Anasema katika eneo hilo akina dada hao wamelima matuta 22 ya mboga hizo ambapo 10 ni ya chainizi na 12 ya spinachi.

Soko la spinach liko wapi?

Simon Mnkondya ni Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Kimataifa ya Greenhouse, anafafanua kuwa baada ya kampuni hiyo kununua spinach hiyo, huisafirisha kwenda visiwa vya Comoro kwa ajili ya kuiuza.

“Soko letu kubwa la mboga hizi tunazozalisha lipo visiwa vya Comoro, husafirishwa kwa ndege kutoka Dar es Salaam hadi katika visiwa hivyo,” anasema Mnkondya na kuongeza.

“Tumepata mapokeo mazuri ya mazao ya mbogamboga katika visiwa vya Commoro ikiwamo Mayotte kutokana na ubora wa mboga hizi,” anasema.

Anabainisha kuwa moja ya changamoto iliyokuwa ikiwakabili wakulima wengi ni kutopata wataalamu bora wa kilimo, hivyo kupitia kampuni yake wameweza kutoa mafunzo kwa vijana wanaotoka vyuoni.

“Vijana hawa baada ya kuwapatia mafunzo, tunawapeleka kusimamia mashamba darasa ya wakulima tuliyowalimia kilimo cha green house,” anasema.

Anasema vijana hao hupelekwa katika mashamba hayo kwa ajili ya kuyatunza mazao yaliyolimwa kwa kipindi cha mwaka mzima na wawapo katika mashamba hayo huendelea kutoa mafunzo ya moja kwa moja kwa njia ya vitendo.

Mambo ya kuzingatia

Mgallah anasema mkulima anatakiwa kuandaa shamba na kujua muda sahihi wa kuweka mbolea. “Ukichelewa kuweka mbolea unaweza kukosa mavuno mazuri na hivyo kukosa mapato,” anasema.

Anafafanua kuwa kitu kingine cha kuzingatia katika kilimo hicho ni kujua changamaoto, dalili za magonjwa na kukabiliana nazo.

Kwa mujibu wa Mgallah, kabla ya kupanda huweka mbolea ya samadi, baada ya kupanda huweka mbolea nyingine na mwisho ni mbolea ya kukuzia mimea.

Aidha, baada ya mmea kukua, mkulima anatakiwa kupulizia dawa ya kuua wadudu waharibifu kila baada ya siku 14.

“Pulizia dawa ya kuua wadudu mboga zako ili kuzuia wadudu waharibifu na baada ya kupulizia unatakiwa kuzimwagilia maji mengi kisha utatakiwa kuziacha kwa wiki nzima kabla ya kuzichuma ili dawa iishe,” anasema.

Anasema ndani ya mwezi mmoja tangu kupandwa kwa spinachi, mkulima anaweza kuanza kuvuna.

Advertisement