Mazao sita ya kupanda msimu huu wa ukame

Saturday March 30 2019

 

By Elias Msuya, Mwananchi [email protected]

Wakulima katika baadhi ya maeneo nchini wako njia panda kufuatia taarifa za hali ya ukame iliyotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA).

Taarifa inataja kuwapo kwa vimbunga viwili vya Idai na Savannah ambavyo vimeathiri mifumo ya hali ya hewa na unyeshaji wa mvua za msimu nchini.

Mikoa ambayo imeathirika kwa kiwango kikubwa ni ya Morogoro (upande wa Kaskazini), Pwani, Tanga, Manyara na Kilimanjaro.

Hata hivyo, lakini kwa upande wa nyanda za Juu Kusini na kanda ya Ziwa Victoria, mvua za msimu zinaendelea kunyesha kama ilivyotarajiwa, huku kimbunga cha Savannah kikitarajiwa kutoweka mapema kabla ya kufika Mashariki mwa Madagascar.

Bado kuna fursa

Licha ya upungufu huo wa mvua, wataalamu wa kilimo wanaona bado ipo fursa ya uzalishaji wa kilimo kwa sababu maeneo yatakayoathirika siyo mengi.

Advertisement

Mkurugenzi wa taasisi ya Utafiti wa Kilimo (Tari), Dk Geoffrey Mkamilo anasema licha ya mvua kuchelewa katika ukanda wa Pwani, bado kuna matumaini ya kupatikana kwa mazao kutoka kwenye kanda nyingine nchi ambazo mvua za kutosha zimenyesha.

“Ukanda wa Pwani hupata mvua za kutosha mara mbili kwa mwaka, japo siku hizi mvua za Vuli zimepungua, lakini mvua za masika zitanyesha na huwa zinaazia Machi. Kwa hiyo tusubiri tu,’’ anasema na kuongeza:

‘’Kwa kanda ya Kati mikoa ya Dodoma na Singida, mvua za mwaka hunyesha kuanzia Desemba hadi kati kati ya Aprili na zimeshanyesha sana.”

Hata hivyo, anasema ili kukabiliana na upungufu wa mvua ni lazima wakulima wapande mazao yanayovumilia ukame kama vile mtama, uwele, muhogo na mbaazi.

“Kama mvua zitaanza kunyesha, basi wakulima wapande mapema na kama kutakuwa na upungufu wapande mazao yanayovumilia ukame na mbegu zinazokomaa mapema kama miezi miwili aua mitatu. Kuna zinazokaa hadi miezi mitano,” anasema.

“Kuna mazao yanayovumilia ukame kama vile mtama, uwele, ulezi na muhogo na viazi vitamu hayo ndiyo yanapaswa kupandwa kukiwa na upungufu wa mvua. Mbegu zipo zimeshafanyiwa utafiti na zinapatikana kwa wasambazaji. Bahati nzuri mazao haya yanalimwa maeneo mengi kama vile kanda ya Ziwa, kanda ya Mashariki, Kusini na Kati.”

Anasema hata kwa mbegu za mahindi zipo mbegu aina 15 zinazovumilia ukame zilizofanyiwa utafiti.

Ushauri wa Dk Mkamilo unaungwa mkono na mtafiti wa kilimo kutoka kituo cha utafiti cha Ilonga, Dk Justine Ringo anayewatoa hofu wakulima kuhusu mbegu zinazovumilia ukame.

“Tatizo la mvua siyo la mtu mmoja, bali ni mabadiliko ya hali ya hewa yanayoikumba dunia. Lakini kwa baadhi ya mikoa kama hapa Morogoro, mvua zimeshaanza kunyesha. Kwa hiyo zipo mbegu zinazovumilia ukame kwa maeneo yatakayokuwa na upungufu wa mvua,” anasema Dk Ringo.

Ushauri kama huo pia umetolewa na mtafiti wa kilimo Mashimini Malima akisema kwa hali ya sasa wakulima wanapaswa kupewa elimu ya kupanda mazao yanayovumilia ukame kwa kuwa unyeshaji wa mvua hautabiriki.

‘Yapo mazao yanayovumilia ukame kama uwele, mtama na alizeti. Yapo mahindi yaliyofanyiwa utafiti na yanavumilia ukame na yanakomaa mapema. Mbegu zipo zimeshafanyiwa utafiti na zinapatikana madukani,” anasema Malima.

Mkurugenzi wa Wakala wa Mbegu nchini, (ASA), Sophia Kashenge mesema bado wanafanya tathmini ya athari ya kuchelewa kwa mvua kwani pia kumeshaathiri uzalishaji wa mbegu.

“Leo ndiyo tunaingia shambani kuangalia athari zilizojitokeza kwenye mashamba yetu ya kuzalisha mbegu, kwa sababu tuna mashamba nchi nzima,” anasema Kashenge.

“Kwa sasa niko Kigoma kuna mvua ya mawe imenyesha na imeathiri mashamba. Huo ndiyo mfumo wa mvua, hapa hainyeshai lakini kwingine inaleta athari,” anaongeza.

Ufumbuzi wa kudumu

Licha ya kushauriwa kupanda mbegu zinazovumilia ukame na zinazokomaa mapema, Serikali sasa inapaswa kuwekeza zaidi kwenye kilimo cha umwagiliaji na kupunguza utegemezi wa mvua kwa kuwa athari za mabadiliko ya tabia nchi zinajidhihirisha wazi.

Maofisa ugani nao wanapaswa kuwatembelea na kuwashauri wakulima mbinu bora za kilimo hasa maeneo yenye upungufu wa mvua. Wawaeleze kuhusu aina na upatikanaji wa mbegu zinazovumilia ukame.

Advertisement