Halima, mbunge kijana mwenye staili yake ya kuchangia bungeni

Ni mbunge mwenye umri mdogo kuliko wabunge wote 393 katika Bunge la 11. Hiki pia ni kipindi chake cha kwanza bungeni.

Huyu si mwingine, Halima Bulembo (28), mbunge wa viti maalumu (CCM). Ili kufanikisha malengo yake, ameibuka na staili ya aina yake katika kuchangia bungeni. Kila anapochangia hulinganisha ilani za vyama vitatu vilivyosimamisha wagombea urais mwaka 2015.

Mfano, akichangia kuhusu miundombinu, anatoa mifano ya uboreshaji wa usafiri ndege na reli, mambo yaliyopo katika ilani ya CCM, Chadema na ACT-Wazalendo.

“CCM imesema itaimarisha huduma kwa kujenga Shirika la Ndege (ATCL), Chadema wamesema wataliboresha shirika liwe linalojiendesha kiuchumi na ACT-Wazalendo wanasema wataunda upya shirika ili iwe chachu ya kuongeza mapato ya fedha za kigeni nchini,” anasema Halima.

Anasema Rais John Magufuli amehakikisha ananunua ndege sita ili aweze kukuza biashara ya usafirishaji, jambo ambalo linamaanisha kuwa ametekeleza ilani za vyama vitatu kwa mpigo kwa sababu hayo pia yamo katika Ilani ya vyama hivyo.

Kuhusu reli, anasema CCM iliahidi ujenzi wa reli ya kisasa ya Standard Geuge, ahadi pia iliyotolewa na Chadema ni kujenga reli mpya na kukarabati zilizopo kwa viwango vya kisasa.

Anasema wapinzani hawatakiwi kumpinga Rais Magufuli, bali wamuunge mkono kwa vile ametekeleza yaliyopo katika ilani zao.

“Rais Magufuli ameyatekeleza na wakiona wameishiwa hoja wafunge milango wahamie CCM. Haitakuwa mara ya kwanza wala hakuna atakayewacheka. Mwaka 1960 kulikuwa na chama kinaitwa United Tanganyika Party kilifunga ofisi kikahamia Tanu kwa kuona hakina hoja,” anasema:

“Mwaka 1963 kulikuwa na ANC cha Zuberi Mtemvu walipoona hawana hoja mpya walifunga na kujiunga na Tanu. Tunawakaribisha CCM tujenge nchi na tutawapokea. Rais anafanya vizuri. Muache kumbeza, kumdharau, kumdhoofisha, badala yake mumuunge mkono kwa bidii anatekeleza matakwa ya Watanzania,” alisema.

Anasema ameamua kuchangia kwa kutumia ilani za uchaguzi za vyama ili kuwadhihirishia kuwa yanayofanyika sasa pia yamo katika ilani zao, hivyo badala ya kulalamika wamuunge mkono.

“Suala jingine ni la sekta ya afya, tangu ameingia madarakani vituo vingi vimejengwa na sasa malalamiko kuhusu kukosekana kwa dawa hakuna. Hizi ndizo hoja ambazo zilikuwa zinashikiwa kidedea na upinzani sasa hazipo tena,” anasema.

Mbali na hilo, anasema kuna masuala ambayo amejifunza katika kipindi cha miaka minne bungeni, Halima anasema amefahamu kwa kina changamoto za maisha walizonazo Watanzania.

“Nimejua namna gani wanapata taabu, maisha magumu wanayoishi na nimejua msaada gani wanaohitaji. Mbunge anatakiwa kuwa mvumilivu, kutokata tamaa na kutotoka nje ya malengo yake,” anasema.

Halima aliingia katika siasa mwaka 2002 akiwa mjumbe wa Baraza la UVCCM Taifa kupitia chipukizi. Wakati huo alikuwa anaona vijana wanagombea wanapata ubunge na hivyo ikamhamasisha kuweka malengo kuwa akifikia miaka 21 naye angegombea.

Nini kilimshawishi? Halima anasema alivutiwa na marehemu Amina Chifupa na Ester Bulaya jinsi walivyothubutu kugombea wakiwa na umri mdogo.

“Niliamini kuwa nitaweza ingawa kwa watu waliokuwa wakiniona marafiki zangu wanasema wewe mdogo sana huwezi kuchaguliwa lakini mimi niliwaambia nitagombea kwa uwezo wa Mungu nitashinda,” anasema.

Anasema ulipofika mwaka 2015 aligombea na kushinda kiti hicho na sasa ana miaka minne bungeni.

Hata hivyo, Halima ambaye hafikirii kugombea kupitia jimbo kwa sasa, anawashauri vijana wengi kujitokeza kuwania ubunge na wasikubali kuaminishwa kuwa nafasi hizo zina wenyewe kila mtu anaweza kugombea na kushinda.

“Iwapo watajitokeza na kushindwa wasikate tamaa wajaribu tena. Kama kuna walioshindwa mwaka 2015 wakashindwa warudi tena waangalie nafasi zao wanaweza kushinda.

“Vijana wajitokeze kwa wingi wasikate tamaa wawe majasiri wapambane kufikia katika ndoto zao,” anasema.

Kuhusu utaratibu wa kuwapata wabunge wa viti maalumu ambao wengi wamekuwa wakishauri kuboreshwa, Halima anasema hajaona shida yoyote katika kuwapata wabunge hao chini ya utaratibu huo.