MAKALA YA MALOTO: Hili la Rais kuongezewa miaka inaletwa na hofu

Wednesday February 26 2020

 

By Luqman Maloto

Kuna afadhali kubwa kuona Tanzania tunajadili suala la Rais John Magufuli kuongezewa miaka ya utawala. Japo si mjadala mzuri kwa nchi ya kidemokrasia tena ambayo inafuata misingi ya usia wa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere.

Kuna afya nzuri Tanzania katika mjadala wa uondoaji wa mihula ya uongozi. Rais wa tatu, Benjamin Mkapa, amesema anaamini Rais Magufuli ataheshimu utaratibu uliowekwa kikatiba.

Kwamba atasalia madarakani kwa mihula miwili yenye jumla ya miaka 10, kisha atapisha. Rais Magufuli mwenyewe mara kadhaa ametamka kutokuwa na kiu ya kuongeza miaka ya uongozi. Mwaka 2016, alimtuma Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole atoe taarifa kwa umma kwamba hakuwa na mpango wa kuongeza muda wake wa uongozi. Alimwambia auambie umma wa Watanzania kuwa yeye binafsi alikuwa havutiwi na mjadala huo. Lakini pia Rais mstaafu Ali Hassan Mwinyi, alishatamka kuwa ingekuwa ni uamuzi wake, angemfanya Rais Magufuli kuwa mtawala wa milele kwa sababu uongozi wake una matokeo makubwa kuliko watangulizi wake, akiwemo yeye (Mwinyi).

Mjadala wa nyongeza ya utawala wa Rais Magufuli, upo kwenye makundi mawili. Kuna wanaotaka mihula irefushwe, kutoka miaka mitano mpaka saba. Hiyo ni hoja ya mbunge wa Kondoa, Juma Mkamia. Wapo wanaotamani ukomo wa mihula miwili uondolewe ili Rais Magufuli awe anagombea na kuchaguliwa mpaka achoke mwenyewe au Mungu akimchukua.

Hoja ya wanaotaka Rais Magufuli aongezewe umri wa uongozi ni moja; kwamba ni kiongozi wa kipekee. Kupata mfanano wake kiuongozi ni vigumu.

Angalau Mhashamu Kadinali Polycarp Pengo, alisema mtu ambaye anaweza kuvaa viatu vya Rais Magufuli na kumtosha ni Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda.

Advertisement

Je, ni kweli kukosekana kwa watu wenye sifa za Rais Magufuli ndiyo sababu ya kutamani aongezewe muda wa uongozi? Ni sahihi kwamba taifa halina watu wenye sifa? Nani kapima na kugundua hilo? Halafu tujiulize; yameanza wakati huu? Mwalimu Nyerere alipata kusema kuwa alipotangaza kung’atuka, watu wengi walimwambia aahirishe uamuzi wake, kwa sababu bila yeye nchi isingekwenda. Mwinyi, mwaka 1995 alipofanya ziara nchi nzima kuwaaga wananchi wakati nchi inaingia kwenye uchaguzi, watu walimlilia wakisema walitamani kuona akiendelea kutawala.

Mkapa amekiri kuwa aliombwa na wazee wa Zanzibar aendelee kutawala hata baada ya vipindi vyake vya muongo mmoja. Kipindi cha Kikwete iliibuka hoja ya nyongeza ya kurefusha umri wa mihula ya Urais, kutoka mitano hadi sita. Mtoa hoja alikuwa mbunge wa Chadema wakati huo, Zitto Kabwe. Ni kuthibitisha kuwa hoja ya nyongeza ya miaka ya uongozi ipo na hujirudia mara kwa mara. Katika kitabu cha Mkapa “My Life My Purpose”, ameeleza jinsi Rais wa Tano wa Zanzibar, Salmin Amour alivyotaka kuvuka mihula miwili, lakini alipambana kumdhibiti.

Kabla ya kueleza sababu ya hoja hiyo kujirudia, nikumbushe kauli ya Rais wa 44 wa Marekani, Barack Obama alipohutubia wakuu wa nchi za Umoja wa Afrika kabla ya kuondoka madarakani. Alisema kiongozi kung’ang’ania madaraka kisa hakuna mwenye kufaa kuachiwa ni kufeli kiongozi huyo. Obama alisema kitendo cha mtu kuwapo madarakani bila kutengeneza viongozi warithi wenye sifa, maana yake kiuongozi aliyepo amefeli. Alimaanisha uongozi ni pamoja na kutengeneza viongozi wazuri wa baadaye.

Sasa turudi kwa Rais Magufuli; ameshasema hataki kuongeza miaka ya utawala. Na hapendi mjadala huo. Katika mkutano mmoja, Rais Magufuli alisema kustaafu ni kuzuri, akamtolea mfano Kikwete alivyo. Akasema muda wake ukifika hataongeza hata dakika. Swali; kwa nini mjadala unaendelea? Jibu ni hofu.

Hofu hiyo ipo pande mbili ya wanaomtaka Magufuli na wasiomtaka. Wanaomtaka ni wale wanao amini Magufuli ni bora kupata mfano wake ni vigumu na akiondoka aliyoyaanza yataharibiwa.

Wanaomtaka wapo wenye kutazama maslahi yao. Kipindi hiki wamepata nafasi nzuri, hivyo wanaamini Rais Magufuli akiondoka hawatapata fursa walizonazo kwa sasa.

Ni hofu ya ulaji wao. Mwalimu Nyerere alisema aligundua wengi waliotaka abaki madarakani walipigia chapuo nafasi zao.

Ipo hofu ya wasiomtaka na wanamhofia wanamuona ni kikwazo kwao. Wanatengeneza mjadala mapema ili wazo la nyongeza ya umri likiibuliwa likose maana. Wanaita ku-pre-empty. Yaani kulitangulia jambo.

Kuelekea Uchaguzi Mkuu 2015, uongozi wa vyama vya Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), walitoa tahadhari kuwa Rais Kikwete alikuwa na mpango wa kujiongezea muda wa kusalia madarakani. Kikwete alijibu akicheka: “Wale wazee sijui huwa wanawaza nini?” Hivyo hoja huwa ipo na huibuliwa kwa hofu.

Wakati mwingine hoja haiibuliwi kwa hofu, bali kujipendekeza. Mtoa hoja aonekane ni mtu mzuri kwa mtawala, amteue nafasi fulani au amfikirie pakubwa.

.

Advertisement