HOJA ZA KARUGENDO: Je, hivi ndivyo alivyo Frederick Sumaye?

Mwaka 2005, wakati Benjamin Mkapa anamaliza kipindi chake cha kuliongoza Taifa letu Tanzania, aliyekuwa Waziri Mkuu wake Frederick Sumaye, alitamba kwamba yeye ndiye anayefaa kumrithi Mkapa.

Anayeweza kulijibu swali hili ni Mkapa. Mzee huyu alikuwa makini sana na ni rais aliyeifahamu vizuri kazi yake. Kama aliweza kumvumilia Sumaye, kwa miaka yote kumi, ina maana Sumaye si mzigo. Ni mtu ambaye alikuwa na mengi ya kuchangia.

Bahati mbaya wakati huo kuna watu walifikiri Sumaye ni tajiri mkubwa. Bahati mbaya nyingine aliyokuwa nayo Sumaye, ni kwamba vyombo vya habari havikumpenda.

Kwa hasira, akasema anaachana na siasa. Alitangaza kabisa, kwamba yeye sasa siasa basi. Tulimsikia akiwa Marekani anasoma. Na huko ndiko alipata mwanga wa kutambua umasikini wa Tanzania. Akashangaa na kujiuliza ni kwa nini Tanzania ni masikini hivyo. Alipokuwa waziri mkuu hakufanikiwa kutambua umasikini wa Watanzania na sababu zake. Alipoamua kuachana na siasa, alitoa maombi au shinikizo kwa serikali inayokuja, isimtupe John Magufuli. Alisema yeye sawa anatoka, lakini Magufuli, apatiwe nafasi kwenye serikali inayokuja. Kwa maana Serikali ya Rais Jakaya Kikwete. Wanaofuatilia mambo wakitafuta magazeti ya Septemba 2005, wanashuhudia kabisa yale yaliyokuwa yakiandikwa juu ya suala hili.

Tulimsikia Sumaye akiziimba sifa za Magufuli, kwamba alikuwa mchapakazi. Wakati huo Magufuli, alikuwa kwenye Wizara ya Ujenzi. Na kwa vile yeye alikuwa ni Waziri Mkuu, sote tulimwamini na kumsikiliza na serikali iliyoingia madarakani ilisikia kilio chake na Magufuli, hakutupwa. Hadi leo hii hajatupwa. Na wale wanaomfahamu kwa karibu, wanasema kiwango chake cha kufanya kazi hakijashuka hata kidogo.

Leo hii Magufuli yule yule, mwenye utendaji ule ule, na hata kuzidi, maana kazi aliyoifanya kwenye ujenzi wa barabara haina kifani, alipoteuliwa na chama chake kugombea urais, Sumaye akamkimbia. Maana yake ni nini? Ina maana Mafuguli alibadilika? Ina maana utendaji kazi ambao Sumaye aliuona miaka hiyo, ulikwisha. Au mtu huyu ndivyo alivyo?

Wakati akichukua fomu ya kuiomba CCM imteue kuwa mgombea urais 2015 tulimsikia kwenye vyombo vya habari akilalamika kwamba kama chama chake kikishawishika kumpitisha mla rushwa, basi yeye atakihama maana hawezi kuendelea kuwa kwenye chama kinachoongozwa na mla rushwa. Baadaye tulishuhudia akitimkia upinzani ambako alikuwa akimfanyia kampeni mgombea urais wa Chadema na Ukawa, Edward Lowassa. Huyu ni mtu wa namna gani? Mnafiki au ndivyo alivyo.

Juzi, akabwagwa kwenye uchaguzi wa Chadema. Akalalamika kwamba huko nako hakuna demokrasia. Akatangaza kujitoa na kuachana na siasa. Huyo ndiye Frederick Sumaye, aliyekuwa waziri Mkuu wa awamu ya tatu kwa kipindi cha miaka kumi…Mnafiki au ndivyo alivyo?