KALAMU HURU: CCM inangoja nini kuufuta upinzani nchini?

Wednesday February 5 2020Elias Msuya

Elias Msuya 

Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM), Kheri James amekaririwa hivi karibuni akisema “wapinzani nchi hii tunawadekeza sana.”

Alikuwa akizungumza katika mkutano wa vijana wa chama hicho uliofanyika jijini Arusha hivi karibuni. Alisema wao kama vijana hawatakubali wapinzani waendelee kudekezwa.

Alisema CCM ndiyo iliyoruhusu mfumo wa vyama vingi na kama wasingetaka, bungeni wao ndiyo wengi wanaweza kupeleka hoja ya kufuta vyama vingi.

Pengine hoja iliyowakera CCM wiki iliyopita ni kitendo cha kiongozi wa chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe kuiandikia barua Benki ya Dunia akiitaka isimamishe mkopo wa Sh1.2 trilioni kwa ajili ya kugharamia elimu nchini.

Mkopo huo ulizusha mjadala mkali miongoni mwa wanasiasa na baadhi ya wanaharakati wakihoji sababu ya Benki hiyo kutoa fedha kwa Serikali ilihali inapinga wanafunzi wa kike wanaopata mimba kuendelea na masomo.

Zitto aliyekuwa safarini katika nchi za Ulaya na Marekani ameshutumiwa na wanaCCM kama msaliti na hata bungeni Spika Job Ndugai amemtaka Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuangalia kama kuna jinai kwa kitendo alichokifanya.

Advertisement

Hata baadhi ya wabunge wa CCM waliochangia mjadala huo mwisho wa wiki iliyopita walimwita Zitto msaliti na wengine wakasema, msaliti hana budi kuuawa.

Kauli ya mauaji pia imetolewa na Mwenyekiti wa UVCCM Mkoa wa Iringa, Kenani Kihongosi akisema kama msaliti angekuwa Iringa wangelala naye mbele.

Kihongosi aliwataka wanafunzi wa vyuo vikuu kuwakosoa na kuwapinga wale wote wanaochafua taifa letu, akisema hao ni maadui namba moja na wanahitaji kuuawa.

Pamoja na kauli hizi kutolewa hadharani, Jeshi la Polisi halijachukua hatua yoyote, jambo ambalo bila shaka lingekuwa kinyume chake endapo zingetolewa na upinzani.

Tukirudi kwa kauli ya Kheri James kwamba wapinzani wanadekezwa, wasiachwe wakaenda mahotelini, Je, ni kweli wapinzani wanadekezwa? Kheri hajui kwamba CCM ni chama dola kilichobeba vyombo vyote vya ulinzi na usalama na ndiyo maana makada wa CCM wanatishia kuua hadharani nahawafanywi lolote.

Kheri hajui kwamba hata Tume ya uchaguzi inateuliwa na Rais ambaye pia ni mwenyekiti wa CCM?

Kheri haoni jinsi vyama vya upinzani vinavyonyimwa hata haki ya kufanya mikutano ya hadhara na hata ile ya ndani inavyoingiliwa?

Kheri anaposema CCM inaweza kuufuta mfumo wa vyama vingi kwa kutumia wingi wake bungeni, kwa nini wasifanye hivyo? Kama wanaona hilo ndilo suluhisho, kwa nini wateswe na kitu kilicho ndani ya uwezo wao?

Advertisement