Msekwa aeleza hatua kwa hatua CCM ilivyozaliwa

Muktasari:

Msekwa alikuma mmoja wa wajumbe 20 kutoka vyama vya Tanu na ASP walioteuliwa kufanya kazi ya kuunganisha vyama hivyo, anasema:

Wakati CCM leo ikitimiza miaka 43 tangu kuzaliwa kwake, mmoja wa waasisi wake, Pius Msekwa ameeleza hatua kwa hatua jinsi chama hicho kilivyozaliwa.

Msekwa alikuma mmoja wa wajumbe 20 kutoka vyama vya Tanu na ASP walioteuliwa kufanya kazi ya kuunganisha vyama hivyo, anasema:

“Mwalimu Nyerere kwenye mkutano mkuu wa Tanu uliompitisha kugombea urais katika uchaguzi mkuu wa 1975, mwishoni mwa hotuba yake ya kushukuru alisema ‘nchi hii ni ya mfumo wa chama kimoja, lakini ndani ya nchi kuna vyama viwili Tanu na Afro Shirazi.’

“Akapendekeza, ‘mimi ninafikiri ni jambo linalofaa tukifikiria kuunganisha vyama vyetu hivi viwili tukawa na chama kimoja tukafanana na katiba yetu inavyosema ya nchi ya chama kimoja.’”

“Mzee Aboud Jumbe ndiye alikuwa mwenyekiti wa chama cha Afro Shirazi kwa wakati huo akasimama akasema, ‘Mwalimu tumelipokea wazo hili tunakwenda kulijadili ndani ya Afro Shirazi Party’,” anasema Msekwa ambaye baadaye aliteuliwa kuwa katibu mtendaji wa kwanza wa CCM.

“Nadhani (Mwalimu Nyerere) alikuwa amekwishaongea na mwenyekiti mwenzake, Aboud Jumbe ambaye ndiye alikuwa mwenyekiti wa ASP.”

Msekwa anasema kwa upande wa Tanu, Mwalimu aliwataka nao wajadili suala hilo kwa kuwa lilikuwa ni wazo lake binafsi na akakitaka chama kilitafakari.

Alisema wazo hilo lilijadiliwa katika ngazi ya matawi kwa Tanzania Bara na matawi mengi yaliafiki wazo hilo na matokeo ya majadiliano hayo yalipelekwa kwenye mkutano wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya Tanu mwaka 1976.

Kwa upande wa Afro Shirazi, anasema nao walijadili wazo hilo katika matawi yao.

“Matawi yao yalikuwa ni machache zaidi, yalikuwa kama 237 tu, kwa hiyo walimaliza mjadala haraka,” anasema.

Kama ilivyokuwa kwa Tanu, Afro Shirazi nao walipeleka matokeo ya majadiliano yao kwenye mkutano wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya Afro Shirazi na matawi yao yote yalikubali vyama hivyo kuungana na Tanu.

Msekwa alisema baada ya matokeo hayo ndipo halmashauri kuu ikaamua kuunda tume ya watu 20 kwa kila chama kilitoa wajumbe 10.

Halmashauri Kuu ya Taifa ya Tanu na ile ya ASP, zilikutana na kufanya kikao cha pamoja Oktoba, 1976. Katika mkutano huo iliteuliwa Tume ya watu 20 iliyopewa jukumu la kutayarisha katiba ya chama kipya.

Msekwa aliitaja tume hiyo, kutoka ASP walikuwa Thabiti Kombo (mwenyekiti), Ali Mzee (katibu), Abdalla Natepe, Seif Bakari, Hamisi Hemed, Rajab Kheri, Asia Amour, Hassan Moyo, Juma Salum na Hamdan Muhiddin.

Kutoka Tanu walikuwa Peter Kisumo (mwenyekiti), Pius Msekwa (katibu), Daudi Mwakawago, Kingunge Ngombale-Mwiru, Jackson Kaaya, Peter Siyovelwa, Nicodemus Banduka, Lawi Sijaona, Beatrice Mhango na Basheikh Mikidadi.

“Tulikubaliana mwenyekiti atoke Afro Shirazi na makamu mwenyekiti atoke Tanu, pia katibu atoke Tanu na katibu msaidizi atoke Afro Shirazi,” alisema.

Alisema mwenyekiti wa Tume hiyo alikuwa Thabiti Kombo na Katibu wake alikuwa Pius Msekwa. Makamu mwenyekiti alikuwa Peter Kisumo na katibu msaidizi alikuwa Ali Mzee.

Msekwa alisema tume ilikuwa na kazi ya kuangalia taratibu za kuunganisha vyama, bendera zake, katiba zake na mambo yote yanayohusiana na chama kwamba chama kipya kitakuwaje.

“Tulianza na katiba, tukajaribu kuunganisha katiba za Tanu na Afro Shirazi, tulikuwa tunasoma katiba zote mbili tunaunganisha yale yaliyokuwa yanafanana fanana, mengi yalikuwa yanafanana, ilikuwa rahisi sana.

“Baada ya kumaliza katiba ndio tukaingia kwenye vyombo vingine vinavyodhihirisha chama, bendera yake, nembo yake jembe na nyundo. Kila hatua tulikuwa tunaripoti kwenye halmashauri kuu. NEC zote mbili zilikuwa zinakutana pamoja kupokea ripoti yetu na mimi katibu ndiyo mwandikaji wa ripoti na ndiye msomaji,” alisema.

Kuhusu rangi ya kijani kwenye bendera ya CCM imetoka kwenye bendera za Tanu na Afro Shirazi.

“Ni ‘domonant’ rangi ya nchi, rangi ya mazao. ‘Of course’ tulikuwa tunashauriana na wenye chama chao (Nyerere na Jumbe). Kama katibu nilikuwa naripoti kwa wote wawili (Nyerere na Jumbe).

“Tukipata wazo kabla ya kuendelea nalo nilikuwa nakwenda kuonana na wote wawili. Mengi walikuwa wanatuongoza wao. Mfano, nembo ya jembe na nyundo tulikuwa tumependekeza iwe katikati lakini Mwalimu Nyerere akasema bora ikae pembeni ndio itapendeza,” alisema.

Bendera ya Tanu ilikuwa na rangi mbili nyeusi na kijani wakati bendera ya Afro Shirazi ilikuwa na rangi tatu, bluu, nyeusi na kijani.

Jina la CCM

Msekwa anasema kuhusu jina la chama kuitwa Chama cha Mapinduzi lilitoka kwa Mwalimu Nyerere mwenyewe.

“Baada ya kukamilisha mambo ya katiba jina lilikuwa mwisho. Tulimuuliza Mwalimu akasema kiitwe Chama cha Mapinduzi, sababu vyama viwili vikiungana vitaleta mapinduzi ya maendeleo kwa wananchi,” alisema Msekwa.

Hivyo, Chama cha Mapinduzi au CCM kwa kifupi lilitokana na azma ya Mwalimu Nyerere ya kutaka kuleta mapinduzi ya kimaendeleo kwa wananchi.

Msekwa alisema kazi ya kuviunganisha vyama vya Tanu na ASP ilikamilika rasmi Januari 21, 1977, lakini kutokana na sababu tatu chama kipya cha CCM ilikubaliwa kizaliwe Februari 5, 1977. Upande wa Afro Shirazi ulikuwa na sababu moja na Tanu ilikuwa na sababu mbili.

Alisema vyama vyote viliikubali Februari 5 kwa kuwa ilikuwa ni tarehe ya kihistoria ya vyama hivyo. Afro Shirazi ilikuwa ni siku kuzaliwa kwao. Wakati Tanu ilikuwa ni Siku ya Vijana na pia ni siku lilizaliwa Azimio la Arusha.

Msekwa alisema CCM ya sasa haina tofauti na ile waliyoiunda kwa kuwa mfumo wa uongozi ni uleule, katiba ni ileile na vikao vya chama ni vilevile ila kilichobadilika ni idadi ya wajumbe.

Historia

“Sisi wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Taifa wa pamoja wa TANU na ASP tuliokutana leo tarehe 21 Januari, 1977 mjini Dar es Salaam, chini ya uongozi wa pamoja wa Mwalimu Julius K. Nyerere, Rais wa Tanu na Ndugu Aboud Jumbe, Rais wa ASP, kwa kauli moja tunaamua na kutamka rasmi kuvunjwa kwa Tanganyika African National Union (Tanu) na Afro Shirazi Party (ASP) ifikapo tarehe 5 Februari 1977 na wakati huohuo kuundwa kwa chama kipya cha pekee na chenye uwezo wa mwisho katika mambo yote kwa mujibu wa Katiba ya chama (Katiba ya CCM),” lilikuwa ni azimio la kuanzisha CCM.

Aidha, Azimio hilo lilisisitiza kwamba: chama tunachokiunda tunataka kiwe chombo madhubuti katika muundo wake na hasa katika fikra zake na vitendo vyake vya kimapinduzi vya kufutilia mbali aina zote za unyonyaji nchini.

Mkutano mkuu huo wa pamoja ulipitisha pia katiba ya CCM na kumchagua Mwalimu Nyerere kuwa Mwenyekiti wa CCM, Sheikh Aboud Jumbe kuwa Makamu Mwenyekiti wa CCM na Pius Msekwa kuwa Katibu Mtendaji Mkuu wa CCM.

Azma ya CCM ilikuwa ni kuendeleza mazuri yote ya Tanu na ASP na kuyaacha mabaya. Miongoni mwa mazuri yaliyoendelezwa na CCM ni pamoja na kuendelea kuimarisha uhuru wa Tanzania ikiwa ni pamoja na kudumisha Mapinduzi ya Zanzibar.

Kuendelea kuimarisha umoja na mshikamano wa kitaifa, kuendelea kutekeleza siasa ya Ujamaa na Kujitegemea, kuendelea kupanua na kuimarisha demokrasia ndani ya chama na nchini ikiwa ni pamoja na kufungua milango ya demokrasia Zanzibar.

Katiba ya CCM iliwataka wanachama wake Zanzibar kuwa na viongozi wengi wa kuchaguliwa badala ya uteuzi kama ilivyokuwa chini ya ASP.

Kwa kupitia Katiba ya Kudumu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Mwaka 1977, wananchi wa Zanzibar walipata fursa ya kwanza ya kuwachagua wabunge wao. Aidha, kwa kupitia Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1979, Baraza la Wawakilishi liliundwa mwaka 1980 na Wawakilishi kupatikana kwa njia ya kura ya siri.

CCM katika kipindi cha mageuzi

CCM kama ilivyokuwa kwa Tanu na ASP, imeendelea kuongoza nchi hata chini ya mfumo wa vyama vingi vya siasa uliorejeshwa rasmi Julai Mosi, 1992.

Changamoto inayoikabili CCM ni kuendelea kuwa chombo cha uongozi katika mazingira haya ya mfumo wa vyama vingi vya siasa na mazingira ya utandawazi bila ya kuwepo Baba wa Taifa.

Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alifariki dunia Oktoba 14, 1999 jijini London nchini Uingereza katika Hospitali ya Mtakatifu Thomas. Kifo cha Baba wa Taifa kilikuwa ni pigo kwa CCM na Taifa.

Chini ya mfumo wa Vyama vingi vya siasa CCM kimeweza kufanya mageuzi ya kisiasa kiuchumi na kijamii.

Mageuzi ya kisiasa yameibua kuanzishwa kwa vyama vingi vya siasa vilivyosajiliwa. Hata hivyo, CCM kimeweza kujiimarisha kisiasa na kiuhalali kupitia ushindi wa chaguzi kuu za 1995, 2000, 2005, 2010 na 2015.