KALAMU HURU: Serikali inahakikishaje haki uchaguzi wa serikali za mitaa unakuwapo?

Wakati uandikishaji wa wapiga kura katika uchaguzi wa serikali za mitaa ukiwa umekamilika kwa zaidi ya wapiga kura 19 milioni kujiandikisha, kuna dosari kadhaa zimejitokeza ambazo zinapaswa kuangaliwa kwa umakini.

Uchaguzi huo unaotarajiwa kufanyika Novemba 24 mwaka huu ulianza kwa malalamiko hasa kwa vyama vya upinzani kutokana na kanuni zake zinazodaiwa zinazolalamikiwa na baadhi ya wadau.

Uchaguzi ni mchakato, achilia mbali siku ya kupiga kura tu, lakini tangu mwanzo kila hatua inatakiwa ifuatwe kikamilifu.

Awali uandikishaji huo ulioanza Oktoba 8 na ambao ulitarajiwa kwisha Oktoba 14 ulionekana kususiwa na baadhi ya wapiga kura, ndipo Serikali ikaongeza siku tatu.

Dosari zimejidhihirisha kwenye uandikishaji huo, kwa mfano, mtu anakwenda kuandikishwa bila kitambulisho na baadhi ya vituo hakukuwa hata na mawakala wa vyama wanaomtambua. Kwa maana nyingine unaweza kusema uandikishaji ulikuwa holela.

Katika baadhi ya maeneo waandikishaji waliondoka kwenye vituo vyao na kuwafuata wananchi katika maeneo yao, jambo ambalo halikubaliki kikanuni. Inawezekana walifanya hivyo ili kuwafikia watu wengi zaidi, lakini pia huko ndiko kuvunja kanuni.

Kulikuwa na utata wa jinsi waandikishaji wanavyohifadhi vitabu vyao ambapo katika baadhi ya maeneo ilielezwa kuwa walikuwa wakihifadhi kwenye maduka ya wenyeji na hata uangalizi wake haukuwa wa uhakika kiasi cha watu wasiohusika kupachika majina yao.

Tunaambiwa kuna watu 19.6 wameandikishwa kwenye daftari la wapiga kura, je ni watu halisi ikiwa ndiyo uandikishaji ulikuwa hivyo?

Swali hili linaweza kujibiwa kama majina yote yatabandikwa na wapiga kura wayatambue.

Suala lingine linalozua utata ni muda wa kampeni. Awali vyama vya upinzani vililalamikia muda mfupi wa kampeni, lakini Serikali ilisema siku saba zinatosha. Kama imewezekana kuongeza siku za kuandikisha, kwa nini isiwezekane kuongeza siku za kampeni?

Msingi wa hoja hii ni kamba mikutano ya hadhara na maandamano ilizuiwa na hivyo vyama vya siasa havikupata muda wa kutosha kueleza sera zake kwa wananchi kama ambavyo CCM inabebwa na viongozi wa Serikali wanaotumia nafasi zao kupiga siasa.

Kuna malalamiko mengi ya mfumo wa uchaguzi yanayopaswa kuangaliwa na kujadiliwa na wadau. Serikali nayo inapaswa kuwa sikivu na kuyafanyia kazi.

Msingi wa malalamiko haya ni kwa sababu mfumo mzima wa usimamizi wa uchaguzi huo umetawaliwa na upande mmoja.

Kinachoonekana figisu zote ni mbinu ya kukitafutia ushindi chama chao, lakini tunaambiwa kuwa kanuni wakati mwingine zinawafanya kuwa wasimamizi.

Ilitakiwa uchaguzi huu uwe mfano wa utekelezaji wa demokrasia ya usawa kwa kuweka vyombo huru vya usimamizi wa uchaguzi.

Bila hivyo ni kuufanya uchaguzi kuwa kituko na hii ndiyo sababu ya wananchi wengi kutopiga kura. Haki tu inatakiwa itendeke, bali pia ionekane ikitendeka.

Kupiga kura ni haki ya wananchi, lakini ni lazima Serikali iweke mifumo ya haki ya watu kuthamini haki ya kuchagua viongozi wanaowataka.