MAKALA YA MALOTO: Usajili wa simu umejenga taifa la “watoa amri na watekelezaji”

Mwananchi ni nani? Nafasi ya kiongozi ni ipi? Tuanze kuulizana maswali hayo mawili kisha tusogee kwenye mjadala wa mchakato wa usajili wa simu kwa alama za vidole na namba ya kitambulisho cha taifa.

Mwananchi ni mwanahisa wa nchi. Kiongozi naye ni mwananchi ambaye amepewa dhamana na wananchi wenzake ili awaongoze. Wote wawili ni wananchi.

Dhamana ambayo kiongozi anakuwa amepewa ni ya kuitumikia nchi, kwa ajili yake na kwa niaba ya wananchi wenzake.

Kiongozi anapopewa dhamana, hafiki anajiamulia kila kitu, bali kuna mifumo imewekwa. Kama ni sheria Bunge litaipitisha, kama mapato na matumizi yake, yatapita bungeni au kwenye mabaraza ya madiwani.

Kila kitu kinakwenda kwa mfumo na hakuna kulazimishana. Hivi wanahisa katika taasisi huamrishwa au huelimishwa kama kuna mabadiliko?

Kama mwanahisa hashurutishwi, iweje kwenye nchi ujengwe mfumo wa kuwaamrisha wananchi, badala ya kuwaelimisha ili wayakubali mabadiliko pale yanapotokea.

Kosa huanza pale mchakato wa mabadiliko ya yanapowekwa katika taswira kama ya fasihi, kwamba yupo fanani na ipo hadhira. Katika fasihi, fanani huburudisha au kusimulia, fanani wa mabadiliko ya kimfumo hutisha hadhira.

Unakuta kiongozi aliyepewa dhamana kwenye mfumo wa nchi, anasema “lazima mfanye hivi, msipofanya hivi kitawatokea hiki”.

Ukifikia hapo unajiuliza, “hivi mwananchi bado ni mwenye nchi au sentensi ya kinadharia?”

Ikiwa mabadiliko ni kwa faida ya kila mmoja kwenye nchi, kwa nini yasitolewe maneno ya kuelimishana badala ya kutishana?

Wengine watatii kwa woga na wapo ambao wataona wanashurutishwa pasipo kujua mantiki ya kufanya wanachoamrishwa.

Usajili wa simu

Ni kweli muda uliotolewa ili watu wasajili simu zao kwa alama za vidole ni mrefu, kisha ukaongezwa. Je, wananchi walikuwa wanaambiwa nini?

Utaona tangazo la jumla kwamba Desemba 31, mwaka jana simu ambazo hazijasajiliwa kwa alama ya vidole zingezimwa. Halafu Rais John Magufuli, kwa huruma akaongeza muda mpaka Januari 20.

Mwananchi akiwasha televisheni anasikia vitisho, redioni anatishwa. Mitandaoni hivyohivyo. Wangezungumza mawaziri, wangefuata viongozi wa Mamlaka ya Mawasiliano (TCRA), wakuu wa mikoa nao wangehimiza. Ujumbe wa simu pia ulijaa vitisho.

Unajiuliza; hivi ni lini huyu mwananchi alielimishwa na akaelimika kuhusu umuhimu na ulazima wa kusajili simu kwa alama za vidole?

Mwananchi anapaswa kulibeba jambo la nchi kama lake, si kwa hofu kwamba asipofanya kitu fulani atakosa huduma.

Kukimbilia kutisha watu badala ya kuwaelimisha ni kujenga taifa la “watoa amri na watekelezaji”. Kwamba kuna watu wanaamrisha, wengine wanaamrishwa wakati ni jambo la wote.

Hali hii inaweza kufanya baadhi ya watu kuhoji “tunaamrishwa kwa faida ya nani? Na kuna agenda gani nyuma ya hizi amri?” Wenye kuuliza hivyo hawatakuwa na makosa, kwani hawajaelimishwa.

Changamoto Nida

Wakati TCRA wanatambulisha kusajili simu kwa alama za vidole, rekodi za Nida zilionesha wenye vitambulisho ni wachache mno.

Kumbe sasa, kabla ya mchakato wa usajili wa simu kwa alama ya vidole na namba za vitambulisho vya taifa, kilichopaswa kuanza ni kuhimiza Watanzania kumiliki vitambulisho hivyo.

Lakini wakati hawajaelimika kiasi cha kutosha, wamerushwa hatua ya juu zaidi kwenda kwenye simu za mkononi.

Ni hapo wananchi kwa kuhofia kukosa mawasiliano, inabidi wakimbilie Nida kuomba vitambulisho ambako wanakuta uwezo mdogo na hivyo msongamano unakuwa mkubwa.

Kule Nida nako vitisho vinashamiri. Waziri wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola anaagiza aelezwe kwa nini mkurugenzi asifukuzwe kazi kwa kuchelewesha vitambulisho. Utadhani alikaa navyo nyumbani hataki tu kuwapa, wakati uwezo wa taasisi ni mdogo.

Watu wanashinda Nida, si kwa sababu wanajua umuhimu wa vitambulisho, ni kwa kuwa wasipokuwa na namba ya kitambulisho hawatamiliki simu.