Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Msigwa aeleza magumu aliyopitia Lissu

Muktasari:

  • Mchungaji Msigwa amesimulia tiba anayoipata Lissu na ulinzi ulivyoimarishwa hospitalini alikolazwa huku pia akidokeza mipango ya kusaka Sh550 milioni za kukodi ndege maalumu ya kumsafirisha kwenda ng’ambo kwa matibabu zaidi.

Dar es Salaam. Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa ameelezea mateso na uchungu ambao mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu alipitia wakati alipokuwa akisafirishwa kwenda Nairobi, Kenya kwa matibabu baada ya kupigwa risasi mjini Dodoma.

Mchungaji Msigwa amesimulia tiba anayoipata Lissu na ulinzi ulivyoimarishwa hospitalini alikolazwa huku pia akidokeza mipango ya kusaka Sh550 milioni za kukodi ndege maalumu ya kumsafirisha kwenda ng’ambo kwa matibabu zaidi.

Akizungumza jana baada ya kutembelea chumba cha habari cha Mwananchi, Tabata Relini jijini Dar es Salaam, Msigwa alisema mwanasheria huyo mkuu wa Chadema, alivuja damu nyingi na kama asingepata huduma ya haraka angefariki dunia.

“Nataka tu niwaambie Watanzania kwamba Tundu Lissu aliumizwa sana katika jaribio la kuchukua uhai wake. Watu wasichukulie kama ni jambo dogo, ni jambo kubwa lililoharibu hata akili za watu tuliokuwa karibu naye,” alisema Msigwa kwa hisia kali. “Mimi mwenyewe ambaye nilikuwa miongoni mwa watu wa kwanza tuliokuwa naye, nikafika mahali nikaona risasi siiogopi tena kwa maumivu aliyokuwa nayo. Nisingependa kama Taifa tufikie huko.”

Alisema kwa hali aliyokuwa nayo, hata walipofika Nairobi, madaktari walishangaa kuona Rais huyo wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) akiwa hai.

Safari ilivyokuwa

Akieleza hali ilivyokuwa ndani ya ndege baada ya kuondoka Dodoma, Msigwa alisema, “Tulipata shida, kuna wakati kitanda kwenye ndege kilifyatuka mimi nikawa nashikilia, mwenyekiti (wa Chadema, Freeman Mbowe), kuna hewa ya Oxygen alikuwa anashikilia mirija kutoka kwenye mtungi ilikuwa imetoboka. Kwa hiyo muda mrefu mimi nimeshikilia kitanda, madaktari wale nao wameshikilia drip za maji,” alisema na kuongeza kuwa kimo kifupi cha ndege hiyo nacho kilikuwa changamoto.

“Kwa hiyo kisaikolojia unaathirika kwa kuona mateso aliyopata. Lakini tumefika Nairobi vizuri wametupokea wakaanza kushughulika naye, mpaka mambo yakaenda vizuri, lakini niseme mwenzetu ameumizwa sana.”

Msigwa alisema Lissu amekuwa akihudumiwa na jopo la madaktari 10 wanaofanya kazi kwa kushirikiana na kila siku wanatoa ripoti.

“Kwa hiyo utaona lile jopo la madaktari 10, wengine ni wa mifupa, wengine wa saikolojia, wengine wa ndani ya tumbo na maeneo mengine, wote wanakaa kumhudumia,” alisema. Kuhusu kumpeleka nchi nyingine kwa matibabu zaidi, Msigwa alisema timu ya viongozi wa Chadema inaendelea kujadiliana na madaktari hao wanaokutana nao kila siku huku akirejea kusema kwamba sababu ya kumwondoa nchini zilikuwa za kiusalama.

“Tulipomwondoa hapa, hatukusema kuwa madaktari wetu hawawezi. Sababu kubwa ni security (usalama), lakini ni ukweli usiopingika kuwa hospitali ya Muhimbili haina tofauti na hospitali ya Jomo Kenyatta kule Kenya ambayo nayo ni ya Serikali. Lakini hospitali tuliyompeleka siyo ya umma, ina gharama kubwa lakini ina huduma kubwa,” alisema.

Kupelekwa ng’ambo

Kuhusu gharama za matibabu, Msigwa alisema ikiwa Lissu atalazimika kupelekwa Marekani au Ujerumani kwa matibabu zaidi watahitaji dola 250,000 za Marekani ambazo ni takriban Sh550milioni kwa ajili ya kukodi ndege maalumu ya matibabu (air ambulance) huku akiwaomba wananchi kuendelea kuchangia.

“Watanzania wenye nia njema waendelee kumchangia walichonacho kwa ajili ya matibabu. Wananchi wasione ni jambo dogo, imani yetu ni kuwa watatuunga mkono kwa sababu imeonekana kwa mara ya kwanza Watanzania wameweka tofauti zao pembeni na kuguswa na jambo la kupigwa risasi, ” alisema Msigwa.

Alisema mpaka sasa wameshatumia hadi Sh160 milioni kwa matibabu tu, mbali na gharama za viongozi wa chama hicho kuishi jijini Nairobi.

Kuhusu kufuata utaratibu wa Serikali uliobainishwa na Spika wa Bunge, Job Ndugai wa kupelekwa Muhimbili kisha Apollo, India, Msigwa alisema isingewezekana kwa kuwa hali ilikuwa mbaya.

“Tuna wataalamu wengi hapo Muhimbili, lakini hatuna vifaa vya kutosha na madaktari, kimekuwa kilio chao kikubwa. Sasa Lissu yuko katika hali ya dharura, unasema tufuate ‘procedures’ (utaratibu) kwamba aende Dar es Salaam, madaktari wakae!” Alikosoa huduma za afya wanazopewa wabunge nchini akisema wenzao wa Kenya wanawashangaa.

Alisema suala la Bunge kumtibu Lissu siyo ombi, bali ni wajibu wake kwa kuwa wabunge wanaisaidia Serikali.

“Tunasimama kwenye jukwaa, tunakamata microphone, tunawaambia Serikali imekosea 1,2,3… tunawaambia bombardier imekamatwa, wawekezaji wanaondoka, sisi tunaisaidia Serikali, sisi ni marafiki. Serikali inapaswa iwalinde hawa watu wanaoisaidia Serikali,” alisema.

Pia alizungumzia usalama wa wabunge akisema, “Ukiangalia wenzetu (Kenya), mbunge analindwa na Serikali, walinzi zaidi ya wanne ambao wako full armed (wana silaha), lakini na nyumbani wako wawili, kwa sababu huyu ni mbunge anayeisimamia Serikali...,” alisema Msigwa.

Alililaumu Jeshi la Polisi akishangaa kwa nini hadi sasa hajakamatwa mtu yeyote anayehisiwa kuhusika.

“Kibaya zaidi hadi sasa hakuna mtu aliyekamatwa kutokana na tukio lile...Viongozi wa Chadema vitisho tulivyokuwa tunasema sasa vimeanza kutokea wazi katika maisha yetu,” alisema.

Kuhusu Balozi wa Tanzania nchini Kenya, alisema siku waliyofika nchini humo hawakumkuta wala ofisa yoyote uwanja wa ndege.

“Balozi kweli alikuwa Tanzania, lakini hatukukuta mtu yeyote. Kule ubalozini kuna mwambata wa Jeshi, kuna mwambata wa usalama wa Taifa, kuna watu wa visa, uchumi, angalau tungekuta mtu. Hakukuwa na official arrangement,” alisema Msigwa.