Polepole atangaza kupokea wabunge zaidi wa Chadema

Katibu wa Itikadi na uenezi CCM Taifa akisaini kitabu baada ya kuwasili Mtaa wa Rebu kata ya Turwa Wilayani Tarime kuzindua Kampeni za uchaguzi nafasi ya Udiwani
Muktasari:
Asema wawili watajiunga wakati wowote, madiwani hawana idadi
Tarime. Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole ametumia mkutao wa kampeni za kumnadi mgombea wa chama hicho katika uchaguzi mdogo Kata ya Turwa kumnanga Mwenyekiti wa (Chadema), Freeman Mbowe.
Akihutubia mkutano wa uzinduzi wa kampeni hizo katika viwanja vya Rebu mjini Tarime jana Julai 29, 2018, Polepole amedai uking’ang’anizi wa Mbowe katika nafasi ya uenyekiti wa chama hicho ndicho kinawakimbiza makada na viongozi wake wakiwemo wabunge na madiwani wanaotimkia CCM.
“Kukosa ushirikiano kutoka uongozi wa juu wa chama na kutoambilika kwa Mbowe ni kati ya sababu zinazowakimbiza wanaohama Chadema. Natabiria chama kile kuendelea kuporomoka zaidi,” alisema Polepole
“Kuna wabunge wawili ambao kwa sasa nahifadhi majina yao nao watahamia CCM wakati wowote kuanzia sasa; madiwani wanaoomba kuja idadi yao haihesabiki,” aliongeza.
Akimnadi mgombea wa CCM, Mwita Chacha maarufu Chacha Kamanda kiongozi huyo aliwaomba wapiga kura wa Kata ya Turwa kumchangua mgombea huyo ili akashirikiane na viongozi wa CCM inayoongoza Serikali kuwaletea maendeleo.
Polepole alitumia mkutano huo kutaja baadhi ya miradi inayotekelezwa ikiwemo ununuzi wa ndege, ujenzi wa reli ya kisasa, elimu bure, ujenzi wa barabara na madaraja kuwa mfano wa utekelezaji wa ilani na ahadi za CCM wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu wa 2015.
Aliyekuwa diwani wa Turwa kupitia Chadema aliyetimkia CCM, Zakayo Wangwe alitumia mkutano huo kuwaeleza wapiga kura sababu zake za kuhama ni kukosa ushirikiano kutoka kwa mbunge wa Tarime Mjini, Ester Matiko akidai alikuwa akipinga kila wazo alilotoa kwa hofu ya yeye kuwania ubunge 2020.
Zakayo ambaye sasa ni Ofisa Mtendaji wa Kijiji katika moja ya vijiji vya Kata ya Nyamwaga pia alimtuhumu Mbowe hakuwa upande wake kutokana na historia ya upinzani kati yake na marehemu baba yake, Chacha Wangwe.
Mbunge wa Jimbo la Bunda Vijijini (CCM), Born Getele akimwombea kura mgombea udiwani akisema CCM ndiyo chama imara kilichomakini kisicho na ubinafsi hivyo kubaki Chadema ni kupoteza muda.
Akiomba kura, mgombea Mwita Chacha aliwaomba wapiga kura kumwamini na kumchagua ili akasimamie utekelezaji wa ilani ya CCM ambayo ndiyo inatekelezwa licha ya halmashauri na jimbo la Tarime kuongozwa na Chadema.