Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Serikali yaagiza waliolipia ving’amuzi Azam, Dstv, Zuku warejeshewe fedha

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Isack Kamwelwe akizungumza na wanahabari

Muktasari:

Kamwelwe amezitaja kampuni hizo kuwa Azam, Dstv na Zuku na kwamba zimekiuka masharti ya leseni zao.

 


Dar es Salaam. Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Isack Kamwelwe amesema kampuni zinazotoa huduma za ving’amuzi

zinapaswa kuwarejeshea fedha wateja wanaotumia ving’amuzi hivyo kutokana na kukiuka masharti ya leseni.

Kamwelwe amezitaja kampuni hizo kuwa Azam, Dstv na Zuku na kwamba zimekiuka masharti ya leseni zao.

Kampuni hizo ziliondoa chaneli za ndani zisizolipiwa baada ya tangazo  la Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), lililokusudia kusimamisha leseni kwa maelezo ya ukiukwaji wa masharti.

Tangazo hilo la TCRA lilieleza kuwa kampuni hizo zimekuwa zikionyesha chaneli zilizopo kwenye orodha ya zile za bure kinyume cha matakwa ya leseni zao ambazo zinaelekeza kuwa wasionyeshe.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumamosi Agosti 11, 2018 Kamwelwe amesema, “lazima watumiaji walipwe kwa sababu kampuni hizi zina makosa na fedha hizo hazijalipwa serikalini. Subiri tutatoa deadline (muda wa ukomo) wa namna watakavyolipwa watumiaji hawa wa ving’amuzi.”

Waziri Kamwelwe ameongeza akisema, “naona mmetuwahi kutuuliza jambo hili, lakini niwahakikishe TCRA inalifanyika kazi kuhusu urejeshaji huu. Lazima warudishe (fedha) kwa mujibu wa taratibu kwa sababu wamefanya makosa.”

Amesema televisheni za ITV, Clouds, EATV na Channel Ten walitoa maoni kwenye mitandao ya kijamii kuhusu kadhia hiyo wakiwa na hoja kuwa busara iliyotumika huko nyuma kwa vituo hivyo kupeleka maudhui yao kupitia ving’amuzi vya Azam, Dstv na Zuku iendelee wakati utaratibu wa kurekebisha sheria ukiendelea.

“Jambo la msingi la kujiuliza ni TCRA kuendelea kuangalia sheria na kanuni za utangazaji zikivunjwa kila kukicha au wachukue hatua ili sekta ya habari iendeshwe kwa mujibu wa sheria?” amehoji Kamwelwe.

Amesema kuna mambo mengi ya kujiuliza, baada ya uamuzi uliolekeza utaratibu mpya wa matumizi ya ving’amuzi kama kanuni zinavyoelekeza kwa watoa huduma wa Azam, DSTV na Zuku ambao walikwenda Mahakama Kuu kupinga uamuzi wa TCRA, lakini shauri lao lilitupiliwa mbali Agosti 22, 2017.

“Hata hivyo mahakama ilitupilia mbali pingamizi hilo Agosti 22, mwaka jana. Baadaye watoa huduma hao walikwenda FCC kwa makundi mawili kwa shauri hilo,” amesema Kamwelwe.

Amefafanua kuwa kundi la kwanza lilihusu Azam ambalo lilitupiliwa mbali na FCC na shauri la kundi la pili ni Azam, DSTV na Zuku ambapo bado linashughulikiwa.

“Kifungu cha 45 (5) cha Sheria ya TCRA ya mwaka 2003 kinasema kuwa uamuzi wowote wa TCRA katika kutekeleza majukumu yake ya kudhibiti, utatekelezwa pasipo kujali iwapo mtu ambaye hajaridhishwa na uamuzi amekata rufaa au anatarajia kuchukua hatua dhidi ya uamuzi huo,” amesema.

“Hii ina maana watoa huduma hawa walipaswa kutekeleza uamuzi wa TCRA kwanza pamoja na kuwa walikata rufaa FCC. Nitumie nafasi hii kuipongeza Azam ambao wametekelezaagizo la Serikali.”

Kamwelwe ametumia nafasi hiyo kuwataka wananchi kuzingatia kuwa ni lazima sheria na kanuni za nchi zifuatwe kikamilifu na kila mwenye leseni aiheshimu.

Pia, aliwataka wananchi kutumia ving’amuzi sahihi ili kupata huduma za maudhui yasiyo na malipo.

“Ving’amuzi vya Azam, Zuku na Multichoice havijazuiliwa, bali vitaendelea kutumika kwa mujibu wa masharti ya leseni zao,” amesema waziri huyo.