Sumaye atoboa siri ya Waitara kutimkia CCM

Muktasari:

  • Kuongezea alichosema Sumaye, viongozi wengine wa Chadema wamesema Waitara amekimbia kuhojiwa na kamati ya maadili.

Dar es Salaam. Siku moja baada ya aliyekuwa mbunge wa Ukonga, Mwita Waitara kutangaza kurudi CCM, mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Pwani, Frederick Sumaye ametoboa siri ya sakata hilo.

Kuongezea alichosema Sumaye, viongozi wengine wa Chadema wamesema Waitara amekimbia kuhojiwa na kamati ya maadili.

“Waitara alikuwa mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, yote aliyoyasema angeweza kuyahoji vikaoni, lakini hakufanya hivyo. Waitara ameondoka kipindi ambacho kamati kuu imempa adhabu lakini si ya kumfukuza,” alisema Sumaye jana alipozungumza na Mwananchi.

Hata hivyo, Sumaye ambaye alikuwa Waziri Mkuu kwa muongo mmoja kuanzia mwaka 1995 hadi 2005 katika utawala wa Awamu ya Tatu, alisema hawezi kumlaumu Waitara kwa uamuzi wake huo.

“Siwezi kumlaumu kwa uamuzi wa kuhama, hata mimi nilihama CCM na kujiunga Chadema Agosti 22, 2015,” alisema Sumaye ambaye ni mjumbe wa Kamati Kuu ya chama hicho.

Juzi, Waitara alitangaza kurudi CCM katika mkutano na waandishi wa habari ulioitishwa na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole uliofanyika ofisi ndogo za chama hicho, Lumumba jijini Dar es Salaam.

Waitara aliyekuwa Mwenyekiti wa Chadema Dar es Salaam alitaja sababu za kuchukua hatua hiyo kuwa ni pamoja na matumizi ya ruzuku kutowekwa bayana na uenyekiti wa Freeman Mbowe kutofika mwisho.

Akifafanua hoja hizo jana alipozungumza na Mwananchi, Waitara alisema suala la ruzuku limekuwa tatizo.

“Hakuna anayeruhusiwa kuhoji, Mbowe pekee ndiye anajua matumizi yake, anajua fedha anazipeleka wapi,” alidai.

Alipoulizwa iwapo aliwahi kuhoji katika vikao vyovyote vya chama alijibu, “Mimi si mjumbe wa Kamati Kuu, lakini Mbowe hataki kuachia uenyekiti kwani ananufaika nao, anajua akitoka atakayekuja anaweza kufanya ukaguzi na kumtia hatiani.”

Kuhusu hilo, Sumaye alisema, “Waitara angeweza kuuliza suala la ruzuku katika vikao kwamba ripoti ya CAG (Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali) ijadiliwe, lakini hakufanya hivyo.

“Hilo la Mbowe kuongoza, Waitara nalo angeweza kulileta Kamati Kuu (ya Chadema) na kuhoji uenyekiti wa Mbowe lakini hakufanya hivyo na sababu alizozitoa anazijua yeye kwa malengo yake ili kuhalalisha hicho anachokitaka.”

Alipoulizwa chanzo cha Waitara kupewa adhabu ni nini, Sumaye alisema, “Siwezi kwenda kwa undani kwani hilo lilikuwa la Kamati Kuu na alipelekwa kamati ya maadili ambayo mimi sikuhudhuria na hata ningekwenda nisingeweza kulizungumzia.”

Siri nyingine

Sababu nyingine inayodaiwa kuwa huenda ilikuwa chanzo cha Waitara kuchukua hatua hiyo ni juu ya tetesi za kushughulikiwa jimboni kwake.

“...Katika uchaguzi ngazi ya chini ya chama, waliwaondoa watu wangu wote na kupanga safu yao.

“Wamefanya hivyo ili nikose nguvu ndani ya chama ili nami nimpigie magoti Mbowe mwaka 2020 kama nitashindwa kushinda, sasa hili limenishinda,” alisema Waitara.

Sumaye akizungumzia hilo alisema, “Kusema watu wangu, hiyo ndiyo kasoro na kosa kubwa.Unaposema watu wangu ni kosa, chama chochote wanachama au viongozi ni wa chama na si wa mtu.”

Sumaye alisema, “Sasa yeye (Waitara) alikuwa anasema kundi lake limeenguliwa, mimi nilimweleza kwamba, katika chama hakuna viongozi au wanachama wa watu binafsi na kama unaona hao waliochaguliwa si wako, cha kufanya, wachukue uwe unafanya nao kazi.

“Ukiwa unafanya nao kazi mwisho mtakuwa katika mrengo mmoja na mimi nafikiri Waitara alianza kufanya hivyo na matokeo yalionekana sasa sijui kilichotokea jana (juzi) cha yeye kuhama,” alisema Sumaye aliyewahi kuwa mbunge wa Hanang’.

Amekimbia kabla ya kujieleza

Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano na Mambo ya Nje wa Chadema, John Mrema akizungumzia na Mwananchi jana kuhusu Waitara kupewa adhabu alisema, “Ni kweli alijadiliwa na kamati kuu na aliandikiwa barua aliyokabidhiwa juzi (Julai 27) ya tuhuma zake na kutakiwa kujieleza mbele ya kamati ya maadili taifa.

“Ameamua kukimbia na sasa haelezi ukweli ila anatunga propaganda mpya,” alisema Mrema.

Alisema, “Nilimpokea Waitara kwenye chama 2008 ameamua kuondoka, namtakia safari salama huko aendako na ndoto zake za kuwa mwenyekiti wa chama cha siasa huenda zikatimia huko CCM, ngoja nijipe muda.”

Waitara alipotafutwa kuzungumzia adhabu aliyopewa alisema, “Hilo la adhabu ndiyo kwanza nalisikia kwako, sijawahi kupewa barua au kuitwa nami nilikuwa nakwenda ofisi za chama mbona sikuwahi kuelezwa na wala sijawahi kuvuliwa uongozi wowote?”

Mrema akizungumzia hoja aliyoitoa Waitara ya ruzuku na uenyekiti wa Mbowe alisema ni mufilisi kwa kuwa taarifa za matumizi ya fedha zinakaguliwa na mkaguzi wa ndani na CAG ambaye ripoti zake huwekwa wazi.

“Mbowe si katibu mkuu wa chama, bali ni mwenyekiti. Katibu mkuu ndiye ofisa maduhuli wa chama, Waitara anamrukia Mbowe ili kumchafua, tunajua wana CCM wengi hawapendi kuona Chadema imara chini ya uongozi wa Mbowe,” alisema.

Segerea kwafukuta

Wakati hayo yakitokea, Chadema Wilaya ya Ilala imetoa onyo kwa wanachama wake 13 akiwamo Mbunge wa Viti Maalumu, Anatropia Theonest ambao watakuwa chini ya uangalizi kwa miezi 18.

Mbali ya wanachama hao, aliyekuwa Mwenyekiti wa Segerea, Gango Kidera amefukuzwa uanachama, huku Katibu wa Kata ya Kinyerezi, Alex Massaba na mwanachama mwingine, Lillian Wassira wakifikishwa mbele ya kamati ya maadili.

Mwenyekiti wa wilaya hiyo, Makongoro Mahanga alisema hatua hiyo inatokana na viongozi na wanachama kukiuka katiba na maadili ya chama.

“Tunataka kurejesha nidhamu ya chama. Chama kisipokuwa na nidhamu hata Ikulu tunaweza kuisikia tu. Kwa hiyo, hawa wamechukuliwa hatua kwa mujibu wa katiba,” alisema Mahanga aliyewahi kuwa naibu waziri wa Kazi na Ajira

Alisema watakaokuwa chini ya uangalizi hawatapaswa kurudia makosa na hawatagombea nafasi yoyote ya uongozi ndani ya chama.

Kuhusu kuondoka kwa Waitara, Makongoro alisema, “Ameondoka kipindi ambacho anatakiwa kujibu tuhuma. Waitara alikuwa ameshavuliwa uenyekiti wa wabunge wa Kanda ya Pwani na uenyekiti wa Greater Dar es Salaam (Dar es Salaam Kuu).

“Uamuzi huu ulichukuliwa na kikao cha kamati kuu ambacho kimekaa kama wiki mbili zilizopita, Waitara alikuwa anajua lakini kama anasema alikuwa hajui, hilo ni yeye. Ukweli hatua zilikuwa zimechukuliwa na barua amepewa,” alisema.

“Unajua watu wanapewa barua wanakimbiakimbia hata sisi huku Segerea tuliowachukulia hatua wanakwepa kupokea barua lakini Waitara anafahamu hatua zilizochukuliwa,” alisema Mahanga aliyewahi kuwa Mbunge wa Segerea kwa tiketi ya CCM.