TRA yafungia vituo vya mafuta 241, vingine 840 hatarini

Thursday August 10 2017
mafuta

Dar es Salaam. Unaweza kusema  kwamba moto ambao Rais John Magufuli aliuwasha dhidi ya wafanyabiashara ya mafuta waliokuwa wakilalamikia matumizi ya mashine za kielektroniki za kutoa risiti (EFD), haukuwa wa kifuu.

Kuthibitisha hilo, tayari vituo 241 vya mafuta katika maeneo mbalimbali nchini vimefungiwa kuendelea na biashara hiyo hadi pale vitakapotekeleza agizo hilo huku vingine 840 vikipewa wiki tatu kuanzia leo kuhakikisha kuwa vinafunga na kuanza kutumia mashine hizo.

Hatua ya kufungwa kwa vituo hivyo iliyochukuliwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imekuja siku ya 12, tangu Rais Magufuli alipotoa siku 14 kwa vituo hivyo kuwa na mashine hizo la sivyo vifungiwe.

Rais Magufuli alitoa agizo hilo Julai 20, wakati wa uzinduzi wa Barabara ya Kigoma - Biharamulo - Lusahunga na kuwataka wafanyabiashara hao kutekeleza hitaji hilo la kisheria, la sivyo watafute shughuli nyingine ya kufanya kwa sababu leseni zao zitafutwa. Aliiagiza Wizara ya Fedha kwa kushirikiana na ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kupitia TRA, kusimamia utekelezaji wa agizo hilo kwa kufuta leseni zote za vituo vitakavyokuwa havijafunga mashine hizo.

Hata hivyo, siku chache baada ya agizo hilo la Rais Magufuli, katibu wa uhusiano na mawasiliano wa Chama cha Wamiliki na Wauza Mafuta Rejareja (Tapsoa), Kanda ya Ziwa, Ahmed Msanga alikaririwa akisema bei kubwa ya mashine hizo ni moja ya changamoto zinazozorotesha utekelezaji wa agizo la Serikali na kuiomba kuingilia kati kwa kuwadhibiti wafanyabiashara wa kati wanaoagiza na kuziuza.

Alisema moja inanunuliwa kati ya Dola 2,500 na 3,500 za Marekani; hivyo mfanyabiashara mwenye pampu nne hadi tano kulazimika kutumia kati ya Sh40 milioni hadi Sh50 milioni.

Advertisement

Lakini jana, Mkurugenzi wa Elimu kwa Mlipakodi TRA, Richard Kayombo alisema baada ya kukagua vituo hivyo, 241 vilikutwa havijafunga wala kununua mashine hizo.

Kwa mujibu wa Sheria ya Usimamizi wa Kodi ya mwaka 2015 na kanuni zake za mwaka 2016, mfanyabiashara anayethibitika kukwepa kutumia au kutoa risiti za kielektroniki anaweza kukabiliwa na adhabu ya faini ya Sh3 milioni hadi Sh4.5 milioni, huku mnunuzi anayekutwa na kosa la kutodai risiti, adhabu yake ikiwa faini ya kati ya Sh30,000 hadi Sh150,000 au kifungo au adhabu zote kwa pamoja.

“Vituo hivyo viko maeneo mbalimbali mikoani, tumevifungia kabisa kutokufanya biashara yoyote ya mafuta hadi pale watakaponunua na kufunga mashine hizo, ni sawa na unapofunga duka lisifanye biashara yoyote,” alisema.

Kayombo alisema kufungiwa kwa vituo hivyo kumetokana na wamiliki wake kushindwa na kutoonyesha nia ya kufunga mashine hizo. “Tumeagiza mameneja mikoa wote kufunga vituo hivyo na bado kuna vingine ambavyo vinaendelea kufungwa moja kwa moja,” alisema.

Kuhusu vituo 840, Kayombo alisema wamiliki wamepewa wiki tatu kuanza sasa na watasainishwa mikataba ya kufunga mashine hizo vinginevyo vitafungiwa pia. Alisema wapo ambao walishalipia mashine hizo na kazi inayoendelea ni usambazaji na ufungaji.

“Hawa wamesaini makubaliano, ikifika Agosti 31, wanatakiwa wawe wamemaliza kufunga na kuanza kutumia mashine hizo. Tumetoa muda huo kwa sababu wengi wao wapo mikoani kama Mbeya, Bukoba na maeneo mengine hivyo wana kazi ya kusafirisha...” alisema.

Kayombo alisema hadi kufikia jana, vituo 519 vilikuwa vimeshafungwa mashine za EFD.

Majengo yaingiza Sh31 bilioni

Mbali ya kuzungumzia vituo vya mafuta, Kayombo pia aligusia mafanikio yaliyopatikana katika operesheni kubwa ya kodi ya majengo akisema TRA imekusanya kiasi cha Sh31 bilioni kwa mwaka wa fedha ulioisha Juni 31.

“Tunaendelea kusisitiza ukusanyaji wa kodi pamoja na kwamba muda uliongezwa kwa sababu ya wingi wa watu kuja mwishoni. Waendelee kulipa kodi kwa mwaka wa fedha 2017/2018,” alisema.

Alisema mamlaka inaendelea kupokea kodi ya majengo, na wale ambao walichelewa kulipa ya mwaka 2016/2017, bado wataendelea kulipa ila watalipa na adhabu kwa kuwa ulitolewa muda wa nyongeza na walishindwa kutekeleza.

Alisema kwa ambao hawajalipa kodi ya majengo hadi kufikia jana, wanatakiwa wafanye hivyo.

Mkurugenzi huyo wa elimu kwa mlipakodi TRA, alisisitiza ulipaji kodi  kwa mujibu wa sheria, “Wananchi watoe ushirikiano. Nia sio kuadhibu wafanyabiashara kwa kutoa risiti au kudai risiti, ni kujenga utamaduni na mazoea ya kulipa kodi.”

Alisema mfanyabiashara mwenye mauzo yanayozidi Sh14 milioni kwa mwaka, anatakiwa kutumia mashine za EFD.

Profesa wa uchumi Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Haji Semboja alisema pamoja na juhudi hizo, Rais Magufuli anakabiliwa na changamoto ya wafanyabiashara wadogo maarufu kama wamachinga baada ya kuwaruhusu kufanya biashara maeneo yoyote.

“Hawa ni bomu la kisiasa, kiuchumi na kijamii, ni wengi na baadhi yao wanauza bidhaa zisizokuwa na ubora, hazina uhalali, hazina utambulisho (nembo) kwenye soko.

Alisema kisiasa, kundi hilo linaweza kukwamisha hata ndoto za uchumi wa viwanda kwa sababu vingine itabidi vianze kujiendesha kiujanjaujanja ili kuleta ushindani wa masoko katikati ya changamoto hiyo.

Advertisement