Wahalifu wa kimtandao waibua taharuki Chuo Kikuu Huria

Wednesday October 25 2017
HACKERS

Dar es Salaam. Taharuki iliibuka kwa saa kadhaa jana katika Chuo Kikuu Huria (OUT) baada ya wahalifu wa kimtandao waliojitambulisha kwa jina la ‘Tanzania Hackers’ kuingilia mawasiliano ya tovuti ya chuo hicho huku wakiacha ujumbe wa vitisho vya mahitaji ya ajira kwa nguvu vinginevyo wataingilia hadi mifumo ya Serikali.

Wahalifu wa mtandao ni wataalamu wa teknolojia ya mawasiliano (IT) wanaotumia programu zao au lugha za kompyuta kuingilia mtandao wa kampuni au Serikali bila kuwa na nywila (password) inayotumika kwa lengo la kuiba taarifa za siri au nyinginezo.

Mmoja wa watumishi chuoni hapo ambaye aliomba kuhifadhiwa jina lake, alisema taharuki iliyotokea ilisababisha watumishi wa taasisi hiyo kushindwa kufanya kazi kuanzia asubuhi hadi saa 10 jioni wakati uongozi wa chuo ukiendelea na jitihada za kurejesha tovuti hiyo katika mfumo wake wa awali.

“Asubuhi watu tunaingia ofisini, tunakuta tovuti zimeingiliwa ilikuwa ni taharuki kidogo, wameshughulikia suala hilo hadi jioni wameandika ujumbe wa kushtua kidogo na unasikitisha,” kilieleza chanzo kutoka chuoni hapo.

Akizungumzia tukio hilo mkurugenzi wa Idara ya IT chuoni hapo, Dk Edephonce Nfuka alikiri kutokea kwa shambulio hilo la kimtandao huku akisikitishwa na ujumbe wa watu hao. “Tumeliona tatizo asubuhi lakini tuliweka mfumo mbadala, tunashukuru TCRA (Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania) nao walipoliona tatizo hilo wakatujulisha,” alisema Dk Nfuka.

Dk Nfuka alisema baada ya tukio hilo alitoa taarifa kwa Wakala wa Serikali Mtandao (e-Government Agency) ili wachukue tahadhari kutokana na vitisho vilivyotolewa na wahalifu hao.

Advertisement

“Kwa hiyo wamesema wamejiweka sawa kwa uhalifu wowote utakaojitokeza, wako vizuri,”alisema.

Kuhusu matokeo ya kuibuka kwa kundi hilo, Dk Nfuka alisema ni changamoto inayotokana na ukuaji wa teknolojia ya mawasiliano huku akikemea vijana wanaopata taaluma hiyo na kuanza kuitumia katika matukio ya uhalifu.

Baada ya kuingilia ukurasa wa tovuti hiyo ujumbe wa vijana hao umeeleza kuchukizwa na hali ya kuishi maisha ya bila ajira huku wakiwa na taaluma hiyo.

Kaimu meneja mawasiliano wa TCRA, Semu Mwakanjala alisema inapotokea uhalifu wa mitandao mamlaka hiyo hupokea malalamiko kutoka kwa mwathirika au polisi.

“Makundi yote hayo ya kihalifu yanashughulikiwa na cyber crime unit ipo chini ya Jeshi la Polisi ndiyo wanaofuatilia wizi wa kwenye mashine za ATM, ujambazi wa kutumia teknolojia na wanapohitaji msaada wetu wa karibu sisi tunatoa ufumbuzi, lakini hata waathirika mmoja mmoja huleta madai yao,” alisema Mwakanjala.     

Advertisement