MUM: Tanzania ya viwanda iendane na nchi kuwa na wasomi wenye maadili

Muktasari:

Hayo yameelezwa na naibu makamu mkuu wa Chuo Kikuu cha Kiislamu cha Morogoro (MUM), Dk Abdallah Tego

Dar es Salaam. Chuo Kikuu cha Kiislamu cha Morogoro (MUM) kimesema ili kuifikia Tanzania ya viwanda ni muhimu vikawepo vyuo  vitakavyozalisha wasomi wenye weledi na maadili.

Hayo yameelezwa na naibu makamu mkuu wa chuo hicho, Dk Abdallah Tego wakati akizungumza na baadhi ya washiriki wa maonyehso Vyuo vya Elimu ya Juu yaliyoandaliwa na Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU), yanayofanyika katika viwanja vya Mnazi mmoja jijini Dar es Salaam.

Dk Tego amesema vyuo vina mchango mkubwa wa kuhakikisha Tanzania ya viwanda inafikiwa ikiwa ni pamoja na kuzalisha wasomi ambao watakuwa tayari kufanya kazi kwa maslahi mapana ya Taifa.

 

“Nchi inaweza kuwa na wasomi wengi wenye maarifa na viwanda vikawepo, lakini kwa kukosa maadili, badala ya kulisaidia Taifa, wanakuwa chanzo cha kukithitiri kwa mikataba mibovu na ongezeko la rushwa na vitendo vya ufisadi,” amesema Dk Tego.

Amesema maonyesho hayo ya kila mwaka yanasaidia  vyuo kuonyesha umahiri wao katika kusaidia Serikali na jamii kwa ujumla katika kukuza uchumi wa viwanda wa nchi yetu.

Amebainisha  kuwa wamekuwa wakifundisha lugha mbalimbali za kigeni zikiwemo Kichina, Kifaransa, Kiarabu na Kiingereza ili kuwezesha wahitimu kuwa na uwanja mpana wa ufahamu wa lugha ili kwenda sambamba na soko la dunia.

Amesema miongoni mwa mambo wanayoyaonyesha ni maajabu ya mji wa Kilwa Kisiwani ambao umesheheni vivutio mbalimbali ambavyo havipatikani mahala pengine hapa nchini.

Mmoja wa washiriki wa maonyesho hayo, Juma Abdallah mkazi wa Mbagala amesema kupitia maonyesho hayo wamefahamu vyuo mbalimbali kuwa rahisi kuchagua kipi kinafaa kwa watoto.