Kampuni ya TALA inayokopesha mtandaoni yafunga ofisi Tanzania

Muktasari:

  • Kampuni ya TALA inayokopesha kwa njia ya mtandao wa simu za kiganjani, imetangaza kufunga shughuli zake Tanzania.

Dar es Salaam. Kampuni ya TALA inayokopesha kwa njia ya mtandao wa simu za kiganjani, imetangaza kufunga shughuli zake Tanzania.
Imetoa taarifa hiyo leo Jumanne Septemba 17, 2019 na kubainisha kuwa maelezo ya kina kuhusu uamuzi huo yatatolewa hivi karibuni.
Kampuni  hiyo inayoendeshwa na teknolojia ambayo kwa sasa inafanya kazi nchini Kenya, Mexico, India na Ufilipino hutoa mikopo ya haraka, na binafsi kwa wakopaji na  kuvutia zaidi ya watu milioni 27 duniani.
"Tunakujulisha kuwa kwa sasa TALA  haitoi mikopo nchini Tanzania. Tunathamini nafasi ya kukutumikia na tunatamani wateja wetu waaminifu waendelee na mafanikio katika safari yao ya kifedha, "inasomeka taarifa iliyotolewa na kampuni hiyo.
Akizungumza na Mwananchi kupitia ukurasa wa mtandao wa kijamii wa Facebook, mmoja wa maofisa wa kampuni hiyo aliyejitambulisha kwa jina moja la Kelly amesema, "Ndio, hatujatoa mikopo tena nchini Tanzania. Kwa bahati mbaya, kwa sababu za kisheria hatuwezi kusambaza habari nyingine yoyote isipokuwa ile iliyosambazwa kwenye mtandao wa kijamii.”
Ripoti ya kampuni hiyo mwaka 2018 inaonyesha kuwa katika nchi za  Afrika Mashariki asilimia 78 ya mikopo hutumiwa kwa biashara, asilimia 32 ya wateja wake wakiwa  wanawake na wanaume, kati yao asilimia 68 wana umri chini ya miaka 34.