Breaking News

Mauzo ya data ni vita mpya kampuni za mawasiliano

Monday November 11 2019

 

By Samuel Kamndaya, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Wakati matumizi ya intaneti yakizidi kuongezeka, kampuni za huduma za mawasiliano zinachuana kuingiza simu za kisasa za bei nafuu ili kuongeza wateja.

Simu hizo za kisasa zinawezesha wateja kutumia data kwa ajili ya mawasiliano, kuangalia filamu au kupakua filamu, nyimbo au programu nyingine za matumizi ya kawaida katika shughuli za kila siku.

Mchuano huo umepamba moto kwa kampuni hizo kuhakikisha zinakuwa na wateja wengi zaidi wanaotumia intaneti katika kipindi hiki ambacho taarifa za Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) zikionyesha kasi ya kuenea kwa wateja ni asilimia 43.

Kutoka kwa wateja milioni 43.74 waliosajiliwa mpaka Juni, intaneti ni miongoni mwa bidhaa zinazoziingizia fedha nyingi kampuni za simu. Huduma nyingine ni utumaji fedha na utumaji wa ujumbe mfupi (SMS).

Kwa mwaka ulioishia Machi 2019-- kwa mfano-- taarifa za kampuni ya Vodacom, ambayo inaongoza kwa kuwa na wateja wengi, zinaonyesha mapato yatokanayo na upigaji simu yalipungua kwa asilimia 1.1 yakilinganishwa na yaliyopatikana kipindi kama hicho mwaka 2018.

Kinyume chake, mapato ya SMS yaliongezeka kwa asilimia 31.3 wakati ya data yakipanda kwa asilimia 17 na Mpesa kwa asilimia 14.5.

Advertisement

Vodacom, kampuni pekee iliyoorodheshwa Soko al Hisa Dar es Salaam (DSE), iliingiza Sh167.01 bilioni kutokana na mauzo ya data katika kipindi hicho ikilinganishwa na Sh141.61 bilioni ilizopata Machi 2018.

Maendeleo ya teknolojia yamebadili matumizi ya wateja wengi wa simu za mkononi huku wengi wakijielekeza zaidi kwenye data na kuachana na upigaji wa simu wa kawaida ili kupunguza gharama.

Kutokana na ukweli huo, kampuni za simu nazo zimeelekeza mapambano yao ya kusaka wateja eneo hilo, hivyo kulazimika kuhakikisha zinakuwa na bidhaa zinazowavutia wateja wao.

“Utafiti unaonyesha endapo simu za kisasa zitauzwa chini ya dola 30 za Kimarekani, wananchi wengi zaidi watamudu kuzinunua hivyo kuongeza matumizi ya intaneti,” alisema Woinde Shisael, meneja mawasiliano wa kampuni ya Tigo.

“Tigo ndiyo kampuni yenye mtandao mkubwa wa 4G nchini, ni lazima tuwe na wateja wa kutosha ili wanufaike nao.”

Pamoja na hayo, Woinde alisema wanajielekeza zaidi kuelimisha wateja wao matumizi mapana ya intaneti ili waachane na program za kawaida ambazo ni WhatsApp, Youtube, Facebook na Insatgram.

Alisema walianza siku nyingi walipozindua Facebook kwa Kiswahili kisha wakatoa simu za kisasa zinazotumia Kiswahili pia.

“Licha ya kushusha bei ya simu zetu tunatoa vifurushi nafuu zaidi vitakavyomuwezesha mteja kutumia program nyigi zaidi zilizopo kwenye simu yake,” alisema.

Kwa sasa Tigo wanauza simu aina ya Kitochi 4G Smart kwa Sh49,000 wakati Vodacom wakiwa nayo Smart Kitochi wanayoiuza kwa Sh48,000 huku Zantel wakiuza Samrta kwa Sh39,999.

“Tumeingiza Smarta sokoni ili kuwapa wateja wetu fursa ya kumiliki simu ya kisasa itakayowaunganisha na ulimwengu na kufurahia huduma za kidijitali zinazopatikana kwa gharama nafuu kupitia mtandao wa 4G kutoka Zantel,” alisema Aneth Muga, mkuu wa idara ya mauzo ya simu ya kampuni hiyo.

Ushindani huu unafanywa baada ya kampuni hizo kuwekeza katika miundombinu hivyo kulazimika kuwa na watumiaji wa kutosha watakaozipa faida.

Ripoti ya Shirikisho la Kampuni za Simu Duniani (GSMA) kwa nchi zilizo kusini mwa Jangwa la Sahara iliyotolewa hivi karibuni inaonyesha ughali wa kupatikana kwa simu za kisasa ndicho kikwazo cha matumizi ya intaneti has amtandao wa 4G katika mataifa mengi.

Ripoti hiyo inasema simu moja inagharimu wastani wa Dola 100 ambazo wengi hawawezi kumudu ingawa wengi walionazo (asilimia 32) wanasema huzitumia kucheza gemu wakati asilimia 30 hutazama video na asilimia 22 husikiliza muziki.

Ingawa Airtel haijaingiza simu mpya hivi karibuni kama ilivyo kwa washindani wake, meneja mawasiliano wake, Jackson Mmbando alisema wanazo nyingi kwenye maduka yao.

“Tunazo simu mpaka za Sh29,000. Wateja wetu wanaweza kuzipata popote lilipo duka letu,” alisema Mmbando.

Advertisement