Bei ya mafuta duniani yapanda

Muktasari:
- Ni baada ya mashambulio dhidi ya vituo vya mafuta Saudia
Saudi Arabia. Gharama ya mafuta imepanda kwa kiwango cha juu kuwahi kushuhudiwa katika miezi minne iliyopita.
Imeelezwa kuwa kwa sasa bei ya mafuta ghafi imepanda kwa asilimia 19 sawa na Dola 71.95 karibu Sh165, 485 kwa kila pipa.
Kwa mujibu wa Shirika la habari la BBC, kupanda kwa bei hiyo kumesababishwa na mashambulio mawili dhidi ya vituo vya mafuta yaliyofanywa nchini Saudi Arabia.
Mashambulizi hayo yaliyotokea Jumamosi iliyopita yalihusisha ndege 10 zisizo na rubani na kusababisha kumwagika kwa asilimia tano ya mafuta duniani.
Jumapili iliyopita Serikali ya Saudia Arabia, ilitangaza kusitisha uchimbaji wa mafuta kwa muda katika vituo vilivyoshambuliwa na waasi wa Houthi.
Usitishwaji huo unahusisha vituo viwili vinavyomilikiwa na kampuni ya mafuta ya Saudi Aramco.
Waziri wa Nishati wa nchi hiyo na mwana mfalme, Abdulaziz bin Salman alisema hayo jana kupitia taarifa yake na kuongeza kuwa mashambulizi hayo yalifanywa kwa kutumia ndege 10 zisizo na rubani.