Hakuna mgonjwa mpya wa corona China

Muktasari:
Tume ya Taifa ya Afya China imesema wagonjwa wanaopatikana sasa ni wale wanaoendelea kupimwa baada ya kuzuiwa katika katantini walipoingia nchini humo.
Hubei, China. Wakati virusi vya corona vikizidi kusambaa kwa kasi katika nchi za Afrika, China imesema kuwa hajapata mgonjwa mpya kwa siku ya jana.
Tume ya Taifa ya Afya ya China ilisema hali katika Jimbo la Hubei lililopo katika mji wa Wuhan imetengamaa na hakuna mgonjwa mpya aliyeripotiwa.
Jimbo la Hubei, Wuhan ndiyo chimbuko la virusi vya corona vilivyoanza miezi mitatu iliyopita kabla ya kusambaa katika nchi zaidi ya 100 duniani.
Kwa mujibu wa Tume hiyo, hiyo ni mara ya kwanza katika muda wa wiki nane zilizopita kutotokea mgonjwampya kutoka ndani ya China.
Hata hivyo, Tume hiyo ilisema wagonjwa wapya 34 wameripotiwa baada ya kuingia nchini humo wakitokea nje ya China.
Tume hiyo ilisema kuwa sasa wageni wote wanaoingia China huwekwa kwa lazima katika karantini kwa muda wa wiki mbili.
Alisema wagonjwa hao wapya wamepatikana baada ya kufanyiwa vipimo wakiwa katika karantini hizo mara baada ya kuwasili nchini humo.