Hali ya Virusi vya Corona Duniani

Muktasari:

Wanafunzi milioni 300 duniani kubakia nyumbani

Rome, Italia. Karibu wanafunzi milioni 300 kote duniani wanakabiliwa na kipindi cha wiki kadhaa za kukaa nyumbani, huku Italia ikitangaza kufunga shule kutokana na homa ya virusi vya corona na Shirika la Afya Duniani (WHO) likishauri  kufanyika juhudi za pamoja kupambana na janga hilo.

Zaidi ya watu 95,000 wameambukizwa ugonjwa huo na zaidi ya watu 3,200 wamefariki dunia kote duniani kutokana na virusi hivyo vipya na ambavyo maambukizi yake yamefikia nchi 80 hadi leo.

Katika jimbo la California, Gavana Gavin Newsom leo ametangaza dharura baada ya kutokea kifo cha kwanza, ambacho kimeongeza idadi ya watu waliofariki dunia kwa ugonjwa huo nchini Marekani hadi 11, na meli imezuiwa kuingia bandarini baada ya mfanyakazi kupata maambukizi.

Nayo Uswisi leo imetangaza kifo cha kwanza kinachotokana na mlipuko wa virusi hivyo, baada ya mwanamke mwenye umri wa miaka 74 kufariki, wakati Bosnia imethibitisha kuwepo na watu wawili wenye maambukizi.

Idadi kubwa ya watu wanaoambukizwa na wanaofariki dunia iko nchini China, ambako virusi hivyo viliibukia mwishoni mwa mwaka jana, hali iliyoifanya nchi hiyo kuweka karantini katika miji yote mikubwa, kufunga viwanda kwa muda na kufunga shule kwa muda usiojulikana.

Kutokana na kusambaa kwa virusi hivyo, nchi nyingine pia zimechukua hatua zisizo za kawaida, huku Unesco ikisema nchi 13 zimeshafunga shule na kuathiri watoto milioni 290.5.

Wakati ufungaji shule wa muda wakati wa majanga kama hayo si jambo jipya, kiongozi wa Unesco, Audrey Azoulay alisema "kiwango na kasi ya kuvurugwa kwa elimu hakina mfano na kama kikiendelea, kinaweza kuhatarisha haki ya kupata elimu."