Iran yawakamata walioidungua kimakosa ndege ya Ukraine

Muktasari:

Tukio hilo lilisababisha vifo vya watu wote 176 waliokuwapo ndani ya ndege hiyo.

Iran. Serikali ya Iran imetangaza kuwakamata watu kadhaa waliohusika kulipua kombora kimakosa na kuangusha ndege ya Ukraine.

Tukio hilo lilisababisha watu wote 176 waliokuwapo ndani ya ndege hiyo kufariki wakitokea Uwanja wa Ndege wa Tehran.

Tangazo hilo limetolewa leo Jumanne Januari 14 muda mfupi baada ya Rais Hassan Rouhani kutaka iundwe mahakama maalum kushughulikia mkasa huo.

Hata hivyo, msemaji wa idara ya mahakama, Gholamhossein Esmaili aliyetoa tangazo hilo, hakubainisha idadi ya watu waliotiwa mbaroni kuhusiana na mkasa huo.

Katika hatua nyingine, wanadiplomasia wa nchi za Magharibi wamesema mataifa matatu ya Ulaya yaliyosaini mkataba wa kimataifa kuhusu mpango wa Nyuklia wa Iran yakiwamo Uingereza, Ufaransa na Ujerumani yanatarajiwa kukutana na kujadili mizozo katika mkataba huo uliosainiwa mwaka 2015.

Tayari Marekani imejiondoa katika makubaliano hayo na Iran imesema itaacha kuheshimu ukomo wa kurutubisha madini ya urani uliowekwa katika makubaliano hayo.