Jaji New York aamuru Trump arudishe dola milioni mbili alizochukua

Washington. Jaji wa Jimbo la New York ameamuru Rais Donald Trump arudishe dola 2 milioni alizozichukua kwa matumizi ambayo ni kinyume cha sheria.

Trump anadaiwa kuchukua fedha hizo kutoka mfuko wa misaada wa 'Trump Foundation' na kuzitumia katika kampeni zake mwaka 2016 ulipoingia madarakani.

Uamuzi huu unahusu mashtaka yaliyowasilishwa na ofisi ya mwanasheria mkuu wa Jimbo la New York dhidi ya mfuko wa misaada wa 'Donald J Trump Foundation', akiwamo rais mwenyewe na watoto wake watatu, Donald Junior, Ivanka na Eric.

Mahakama pia imeelekeza watoto wa Trump wanaosimamia uendeshaji wa mfuko huo kupatiwa mafunzo ya uongozi na kujua namna ya kufanya maamuzi ya matumizi ya fedha kwa misingi inayokubalika kisheria.

"Donald Trump Jr, Eric Trump na Ivanka Trump - ambao pia walikuwa wakurugenzi wa Trump Foundation - wanapaswa kupata mafunzo ya lazima kuhusu majukumu ya kuwa watendaji na wakurugenzi wa mifuko ya misaada," alisema Letitia James, mwanasheria mkuu wa New York.

Kutokana na uamuzi huo wa mahakama, Rais Trump ametakiwa kukiri waziwazi juu ya matumizi mabaya ya fedha za mfuko huo na kueleza kwamba wakati mwingine atazingatia masharti ya matumizi ya fedha za mfuko huo.

Asasi ya hiari ya Donald Trump ilifungwa mwaka 2018 baada ya waendesha mashtaka kumshutumu kuwa anafanya kazi kidogo kuliko fedha zinazotumika.

Taasisi hiyo inapaswa kutohusisha siasa, mahakama imeeleza.

Vilevile suluhisho pekee la kesi hiyo ni kuwa lazima fedha hizo zilipwe na Trump mwenyewe na kiasi hicho kitaenda kwenye taasisi za msaada ambayo Trump hana uhusiano nayo," aliamuru Jaji Saliann Scarpulla.

"Malipo ya fedha hizo ndiyo suluhisho la mwisho la kesi hiyo," amesema mwendesha mashtaka.

Akizungumzia uamuzi huo, Jordan Libowitz, msemaji kundi maalumu linaloendesha kampeni ya wajibu wa jamii na maadili jijini Washington, amsema: "Huu ni uamuzi mzuri sana, kiasi cha dola milioni mbili si fedha kidogo hata kwa mtu kama Donald Trump.

“Tungependa kuona uamuzi wa mahakama ukienda mbali zaidi hata kutoa zuio kwake na wanawe kujihusisha na mifuko hii ya kijamii,” Jordan Libowitz ameeleza.

Trump na mwanasheria wake wanasema kuwa kesi hiyo ina njama za kisiasa na wamekilaumu chama cha Democrats kutumia kila mbinu ili kumuondoa madarakani.