Kamera CCTV zamnasa muumini akiiba sadaka

Muktasari:

  • Kamera zilizofungwa katika Kanisa Kuu la Mt. James, katika Mji wa Muranga nchini Kenya zimemnasa muumini mmoja akiiba sadaka jana Alhamisi Februari 13.

Taarifa zilizorushwa na Televisheni ya Citizen ya nchi hiyo zimeeleza kuwa Peter Muiya amekamatwa baada ya video za tukio hilo kuonyesha tabia yake iliyokithiri ya wizi wa sadaka katika kanisa hilo.

Mtuhumiwa alinaswa kiwa na bunda za noti katika mifuko yake.

Kilichowashangaza waumini wa Kanisa hilo ni kwamba Muiya alikuwa miongoni mwa waumini wazuri, ambaye hakuwa anakosekana kila siku katika ibada.

Mtuhumiwa huyo wakati mwingine alikuwa akiachwa peke yake akiendelea kusali baada ya ibada kumalizika, fursa ambayo alikuwa anakitumia kufungua masanduku ya sadaka kwa kutumia waya maalumu.

Kwa mujibu wa mratibu wa kanisa hilo, waliamua kufunga kamera za CCTV kanisani baada ya kubaini kila mara sadaka zinapungua.

Na wakati mwingine waliona noti zimechanika katika masanduku ya sadaka, kutokana na juhudi za mtu kutaka kuzitoa kwa kuzivuta.

Katika video ya CCTV, mtuhumiwa anayeaminika ni Muiya, anaonekana akijaribu kufungua sanduku mojawapo.

Watu walio karibu naye, wanasema aliwahi kujihusisha na matukio ya wizi mwaka 2018, kabla ya kuhamishia mchezo wake kanisani hivi karibuni.

Muiya anatarajiwa kufikishwa kizimbani Ijumaa katika Mahakama ya Muranga kwa kosa la kuvunja na kuiba.