Nzige watua DRC

Thursday February 27 2020
nzige pic

DRC. Kundi la nzige wa jangwani limeingia katika nchi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) ikiwa ni mara ya kwanza kwa wadudu hao kuonekana katika Taifa la Afrika ya Kati tangu mwaka 1944.

Shirika la Chakula Duniani (Fao) jana lilionya juu ya tishio la njaa katika mataifa ya Afrika Mashariki baada ya kuvamiwa na nzige hao.

Kenya, Somalia na Uganda zimekuwa zikipambana na wadudu hao waharibifu ambao katika baadhi ya maeneo, historia inaonyesha kwamba walishuhudiwa miaka 70 iliyopita.

Umoja wa Mataifa umesema nzige hao pia wameonekana Djibout na Eritrea na katika siku za karibuni wamefika Sudan Kusini, Taifa ambalo takribani nusu ya idadi ya watu wake wanakabiliwa na njaa baada ya miaka kadhaa ya vita vya wenyewe kwa wenyewe.

Kwa mujibu wa shirika la habari la DW likinukuu taarifa ya pamoja ya viongozi wa mashirika ya kimataifa iliyotolewa jana jioni, imefananisha kundi hilo la nzige kama janga lililozungumziwa kwenye bibilia na linalokumbushia hatari inayoukabili ukanda huo. 

Msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Stephane Dujarric, akiwa mjini New York, jana alitoa wito wa kasi ya utekelezaji kupitia ufadhili uliotolewa na Fao wa Dola za Marekani 76 milioni wa kupambana na wadudu hao.

Advertisement

“Maofisa wameomba msaada huo wakati nzige walipoendelea kuvamia kote Mashariki mwa Afrika. Gharama za kukabiliana nao zimeongezeka mara mbili hadi Dola 138 milioni.

“Mpango wa chakula umeonya gharama za kupambana na athari za nzige kwa usalama wa chakula tu, zinaweza kuwa mara 15 zaidi ya gharama ya kuwazuia kusambaa. Hadi sasa ni Dola 33 milioni tu zimetolewa au kuahidiwa,” amesema Dujarric.

Shirika hilo limebainisha kuwa nzige waliozeeka, wanaoletwa kwa sehemu na upepo, waliwasili katika pwani Magharibi mwa Ziwa Albert, karibu na mji wa Bunia, Mashariki mwa DRC siku ya Ijumaa. Taifa hilo halijawahi kushuhudia nzige kwa miaka 75.

 

Advertisement