Zimbabwe yakabiliwa na baa la njaa la kutengeneza

Muktasari:

Uendeshaji mbovu wa uchumi, rushwa na upandaji bei wa asailimia 490 umechangia kuzorotesha uchumi.

Zimbabwe inakabiliwa na njaa ambayo imetengenezwa na binadamu, huku asilimia 60 ya wananchi wake wakishindwa kupata mahitaji muhimu ya chakula, mwakilishi maalum wa Umoja wa Mataifa alisema jana baada ya kulitembelea taifa hilo la kusini mwa Afrika.
Hilal Elver, ripota maalum katika masuala ya haki ya chakula, imeiweka Zimbabwe katika orodha ya nchi nne zinazokabiliwa na upungufu mkubwa wa chakula.
"Taratibu watu wa Zimbabwe wanaingia katika kiwango cha kutaabika na njaa iliyotengenezwa na watu," mwakilishi huyo alisema katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika Harare, akiongeza kuwa watu milioni nane wataathirika ifikapo mwishoni mwa mwaka.
"Leo, Zimbabwe ni moja ya nchi nne ambazo hazina uhakika wa chakula," alisema baada ya ziara ya siku kumi na moja, akiongeza kuwa mavuno madogo yamechangiwa na upandaji bei usio wa kawaida wa asilimia 490.
"Kwa sasa watu milioni 5.5 wanakabiliwa na hali ya kutokjuwa na uhakika wa chakula" katika maeneo ya vijijini ambako mavuno yaliathiriwa na ukame, alisema.
Watu wengine milioni 2.2 walio maeneo ya mijini pia wanakabiliwa na uhaba wa chakula na hawawezi kupata huduma za jamii, kama maji safi na huduma za afya.
"Ifikapo mwisho wa mwaka... hali ya usalama wa chakula itakuwa mbaya zaidi hukiu watu wanaokisiwa kuwa milioni nane wakihitaji hatua za haraka kupunguza tofauti ya matumizi ya chakula na kuokoa maisha," alisema, akielezea takwimu hizo kuwa zinatisha.
Zimbabwe inakaribia kuingia katika hali mbaya ya kiuchumi, rushwa, umaskini na mfumo mbovu wa afya.
Uchumi, uliovurugwa na uendeshaji mbaya chini ya rais wa zamani, Robert Mugabe, haujaweza kuamka chini ya utawala wa Emmerson Mnangagwa, ambaye alichukua uongozi baada ya majeshi kumlazimisha Mugabe aachie ngazi.