Amchinja mkewe mjamzito wa miezi nane, ajisalimisha

Rombo. Anthony Asenga (33), mkazi wa Kijiji cha Mrere wilayani Rombo anashikiliwa na polisi kwa tuhuma za mauaji ya mkewe, Happiness Sianga aliyekuwa na ujauzito unaokadiriwa kuwa wa miezi minane.

Asenga anatuhumiwa kumuua mwanamke huyo kwa kutenganisha kiwiliwili na kichwa chake usiku wa kuamkia jana na kisha akajisalimisha katika Kituo cha Polisi cha Mashati.

Tukio hilo limeacha simanzi katika kijiji hicho na Kamanda wa polisi mkoani hapa, Salum Hamduni amesema wanamshikilia mtu huyo wakimuhusisha na mauaji hayo.

“Ni kweli kuna tukio la mume kumuua mke wake huko Rombo. Tunamshikilia mtuhumiwa,” alisema Kamanda Hamduni.

“Uchunguzi unaendelea na utakapokamilika hatua nyingine za kisheria zitafuata.”

Akisimulia ilivyokuwa, mwenyekiti wa Kitongoji cha Sembalo, Kijiji cha Mrere, Faustina Urassa alisema walikuta mwili wa marehemu ukiwa umefunikwa kitandani mithili ya mtu aliyelala.

Mwenyekiti huyo alisema wanandoa hao waliwahi kugombana na kutengana kwa muda mrefu, na kwamba siku ambayo tukio limetokea ndiyo waliyopatana na kuanza kuishi tena pamoja.

Alisema kifo hicho kimeacha maswali kwa jamii kwa kuwa walitarajia kupata mtoto baada ya kurudiana na hivyo amani ingerejea katika familia yao.

“Tunashangaa tukio hili la kikatili kutokea siku ambayo wawili hawa walipatana na kuamua kurudiana,” alisema mwenyekiti huyo.

“Baada ya kutengana, mume alifanya kila jitihada ili warudiane. Sasa hatujui ni nini kilichotokea hadi kufikia hatua ya kumchinja shingo kama kuku na kumuua.

“Baada ya kuachana na mumewe, mwanamke huyo aliondoka na mtoto wake wa miaka miwili na kwenda kuishi kwa wazazi wake, na hatukuwahi kujua ni nini kiliwasibu hadi kugombana. Waliporudiana hatukuwa tumejua ni nini pia kilitokea hadi kufikia hatua hiyo.”

Diwani wa kata ya Mrau Keryo, Athuman Kimario alisema kwamba matukio ya mauaji ya kikatili wilayani humo yanaonekana kujirudia.

“Tukio hili ni la kusikitisha sana. Hivi kwa nini binadamu tumekuwa wakatili kwa kiasi hiki hadi kufikia kuuana? Imefika wakati tunaogopana zaidi ya wanyama. Sasa jamii inapaswa kupaza sauti ili watu wa namna hii wachukuliwe hatua za kisheria ambazo zitatoa fundisho katika jamii,” alisema diwani huyo.

Imeandikwa na Janeth Joseph, Florah Temba (Moshi) na Emmanuel Mtengwa