CAG wataja sababu za umaskini nchini Tanzania

Dar es Salaam. Askofu wa Kanisa la Calvary Assemblies of God (CAG) Dk Danstan Maboya ametaja sababu za watu wengi kukabiliwa na wimbi la umaskini kuwa ni uvivu wa kufanya kazi na uwezo mdogo wa kufikiri.

Dk Maboya alisema hayo alipozungumza kwenye mkutano ulioandaliwa na Taasisi ya Christian Leaders Fellowship (CLF) katika ukumbi wa Mlimani City Jijini Dar es Salaam ukiwa lengo la kutoa mafunzo ya namna ya kufikiri vizuri ili kupambana na umaskini.

Alisema si mpango wa Mungu watu wake waishi kwenye wimbi la umaskini lakini wengi wamejikuta kwenye hali hiyo kwa sababu ya kusukumwa kufanya kazi huku wakishindwa kufikiri sawasawa ili wapate njia za kufikia kwenye ndoto zao za mafanikio.

“Biblia yenyewe inasema asiye fanya kazi na asile, kwa hiyo usipo fanya kazi huwezi kufikia ndoto za mafanikio yako na kushindwa kufanya kazi maana yake huwezi kufikiri sawasawa, lazima akili ifunguke ndipo utapiga hatua,” alisema Maboya

“Huu ni mkutano wa kukomboa fikra za watu, tunataka watu wafikiri sawasawa na kupiga hatua kwenye maisha yao.”

Awali, aliyekuwa Waziri wa Habari, Fenella Mukangara alisema Tanzania ni kati ya nchi zilizobarikiwa kuwa na rasilimali nyingi .

Pia, alisema mafundisho ya ukombozi wa fikra na umuhimu wa kufanya kazi kwa bidii yanakwenda sambamba na mtazamo wa Serikali ya awamu ya tano wa namna ya kuondokana na umaskini na kufikia uchumi wa kati na viwanda.