Chadema pekee kutoa wabunge viti maalum

Katibu wa Bunge la Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Stephen Kagaigai akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma jana. Picha na Jonathan Musa

Muktasari:

Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imesema vyama viwili kati ya 20 vilivyoshiriki katika uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba 28 mwaka huu ambavyo ni CCM na Chadema, ndio vyenye sifa ya kupata wabunge wa viti maalum kwenye Bunge la 12.

Dodoma. Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imesema vyama viwili kati ya 20 vilivyoshiriki katika uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba 28 mwaka huu ambavyo ni CCM na Chadema, ndio vyenye sifa ya kupata wabunge wa viti maalum kwenye Bunge la 12.

Wakati NEC ikieleza hayo, jana Katibu wa Bunge, Stephen Kagaigai alieleza kuwa mkutano wa kwanza wa Bunge la 12 utaanza jijini Dodoma Jumanne ijayo, huku mambo matatu yakitawala katika vikao hivyo ikiwamo uchaguzi wa Spika wa naibu wake.

Idadi ya wabunge wa viti maalum hutokana na idadi ya kura za wabunge wote wa chama husika, ambapo chama kinatakiwa kupata asilimia tano ya kura zote halali za ubunge.

Katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015, CCM ilipata kura za ubunge milioni 8.3m Chadema milioni 4.6 na CUF milioni 1.2. kutokana na kura hizo CCM ilipata viti 64, Chadema 36 na CUF 10.

Akizungumza na Mwananchi jana, Mkurugenzi wa uchaguzi wa NEC, Wilson Mahera hakuweza kutaja idadi ya wabunge hao na kutaka kiulizwe chama husika.

Viongozi wa Chadema walitafutwa jana na gazeti hili, lakini simu zao za mkononi zilikuwa zikiita bila majibu.

Katika ufafanuzi wake, Mahera alisema vyama hivyo ndivyo vilivyofikisha asilimia tano ya jumla ya kura halali zilizopigwa kwa wagombea ubunge kwenye uchaguzi huo.

Hata hivyo, alisema ni CCM tu waliopeleka majina ya wanachama wao katika tume hiyo na tayari yamefanyiwa kazi na kurejeshwa kwao.

“Tumepata majina kutoka chama cha CCM pekee na tayari tumeshayafanyia kazi na kuwarejeshea tangu wiki iliyopita,” alisema.

Alisema taarifa zaidi ya idadi ya wabunge wa viti maalum ilivyopata chama hicho itafahamika wiki ijayo.

Kuhusu viti vya ubunge walivyopata vyama vya upinzani, Dk Mahera alisema vyama vya upinzani vilipata viti nane kati ya 264 vilivyopo nchini, viwili Tanzania Bara na sita Zanzibar.

Alisema kwa upande wa Tanzania Bara, chama cha CUF kilipata kiti kimoja (Mtwara Vijijini) na Chadema kiti kimoja Nkasi Kaskazini.

Alisema Zanzibar chama cha ACT- Wazalendo kilipata viti vinne na CUF kilipata viti viwili.

Yatakayojiri bungeni

Mbali na uchaguzi wa Spika, mambo mengine yatakayojiri bungeni ni wabunge kuthibitisha jina la Waziri Mkuu na Rais John Magufuli kulizindua Bunge hilo.

CCM wamempendekeza aliyekuwa Spika wa Bunge la 11, Job Ndugai kutetea kiti hicho huku nafasi ya unaibu spika akipendekezwa Naibu Spika wa Bunge lililopita Dk Tulia Ackson.

Akizungumza jana Kagaigai aliwataka wabunge wateule wote kufika jijini Dodoma kwa ajili ya usajili na taratibu nyingine za kiutawala.

Alisema kuwa shughuli za usajili na taratibu nyingine za kiutawala zitafanyika hadi Ijumaa Novemba 13 2020.

“Naomba muwafahamishe wabunge wote shughuli za usajili na taratibu nyingine za kiutawala zitafanyika bungeni Dodoma kuanzia Novemba 7 hadi Novemba 9 mwaka huu,”alisema.

Alisema kikao cha kwanza cha Bunge la 12 kitafanyika Novemba 10 mwaka huu kama ilivyotamkwa katika tangazo la Rais.

Alisema shughuli ambazo zinatakiwa kufanyika katika mkutano huo ni kusoma tangazo la Rais la kuitisha Bunge na kwamba shughuli kubwa itakayofanyika ni kumchagua spika.

Alisema baada ya spika kuchaguliwa na kuapa kitakachofuatia ni kiapo cha wabunge wote wateule.

Kagaigai alisema baada ya hapo Bunge litafanya shughuli kubwa nyingine ya kuthibitisha jina la waziri mkuu litakalokuwa limewasilishwa bungeni na Rais John Magufuli.

Alibainisha kuwa baada ya kuthibitisha jina hilo, shughuli nyingine itakuwa ni kumchagua naibu spika wa Bunge na kisha ufunguzi rasmi wa Bunge utakaofanywa na Rais John Magufuli.

Kagaigai aliwaomba wabunge watakapofika jijini Dodoma kuwa na nyaraka za hati za kuchaguliwa au kuteuliwa kuwa mbunge, nakala ya kitambulisho cha taifa na kadi ya benki.

Nyaraka nyingine wanazotakiwa kufika nazo ni cheti cha ndoa kinachotambuliwa na Serikali (kwa wale wenye ndoa), vyeti vya taaluma, vyeti vya kuzaliwa vya watoto wenye umri wa chini ya miaka 18 (kwa walionao), picha ndogo nane.

Pia aliwataka kuja na nakala ya wasifu (CV) ambazo zitalisaidia Bunge wakati wa uundaji wa kamati za Bunge.

Aidha, jana Mwananchi ilishuhudia mafundi wakimalizia shughuli za ukarabati wa majengo ya Bunge kwa kupaka rangi.

Viti maalum baraza la wawakilishi

Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC ) imewatangaza wajumbe 18 kutoka CCM kwa nafasi ya viti maalum vya wanawake vya ujumbe wa Baraza la Wawakilishi.

Tume imetangaza majina ya wajumbe hao katika mkutano uliofanyika jana katika ukumbi wa mikutano wa tume hiyo Maisara Mjini Zanzibar.

Kwa mujibu wa Ofisa habari wa tume hiyo, Jaala Makame Haji tume imewatangaza wajumbe hao kwa mujibu wa masharti na maelekezo ya ibara ya 67 ya Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984.

Alisema tume imewatangaza wajumbe hao baada ya kuridhika kuwa wote wana sifa ya kuwa wajumbe wa Baraza la Wawakilishi kama zilivyoainishwa katika Katiba ya Zanzibar ibara ya 68.

Aliwataja waliotangazwa kuwa ni pamoja na Panya Ali Abdallah, Bihindi Hamad Hassan, Salma Mussa Bilali, Shadya Moh’d Suleiman, Fatma Ramadhan Mohamed (Mandoba), Sada Ramadhan Mwenda na Mwantatu Mbaraka Khamis

Aliwataja wengine ni Zainab Abdalla Salum, Riziki Pemba Juma, Leila Muhamed Mussa, Salha Mwinyi Juma, Hudhaima Mbarak Tahir, Sabiha Fil fil Thani, Aza Januar Joseph, Mwanaid Kassim Mussa, Mgeni Hassan Juma, Mwanajuma Kassim Makame na Rahma Kassim Ali.

“Tume tayari imeshawasilisha majina ya wajumbe hao kwa Katibu wa Baraza la Wawakilishi, kwa ajili ya hatua nyingine za kisheria”alisema Makame Haji.