Kampuni ya Kenya yashindwa kununua korosho nchini

Thursday May 09 2019
KOROSHO PC

Dar es Salaam. Serikali imesema kwamba makubaliano yake na kampuni ya Kenya ya kuuza tani 100,000 za korosho hayajafanikiwa baada ya kampuni hiyo kushindwa kutekeleza matakwa ya mkataba kwa wakati.

Januari 30 mwaka huu, serikali, kupitia kwa Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko (CPB), iliingia katika makubaliano na kampuni ya Indo Power kwa ajili ya ununuzi wa tani 100,000 za korosho, makubaliano ambayo yangeipatia Serikali Dola za Marekani 180.2milioni, sawa na Sh418 bilioni.

Mkurugenzi Mkuu wa Indo Power, Brian Mutembei alisema wakati wa kutiliana saini kwa ajili ya makubaliano hayo kwamba kampuni yake ingelipa moja kwa moja kwa serikali ya Tanzania kwa ajili ya korosho ambazo hazijabangulia na kwamba usafirishaji wake kwenda Kenya ungeanza ndani ya wiki ya kwanza ya mwezi Februari baada ya malipo kufanyika.

Lakini kwa mujibu wa waziri wa viwanda na biashara Joseph Kakunda amelieleza gezeti dada la Mwananchi, The Citizen, Jumatatu wiki hii kwamba kampuni hiyo imeshindwa kumalizia baadhi ya taratibu muhimu za kisheria kabla ya kufanya malipo na kuanza kwa mchakato wa usafirishaji. Waziri Kakunda alisema kwamba kufuatia hatua hiyo, serikali tayari imeingilia makubaliano na kampuni nyengine sita kwa ajili ya ununuzi wa korosho.

“Achana na ile kampuni ambayo tuliingia nayo makubaliano kule Arusha (Indo Power) kwa sababu imeshindwa kuyaheshimu makubaliano yenyewe,” alisema. “Hizi kampuni sita kwa sasa ziko mbioni kukamilisha matakwa ya mikataba. Zile ambazo zitawahi kufanya malipo ndizo zitakazoweza kuchukua mzigo uliopo kwa sasa.”

Waziri Kakunda alishindwa kuzitaja kampuni zenyewe ingawaje ametanabahisha kwamba mbili kati ya hizo ni za Kitanzania na zilizobaki ni za kigeni. Amesema kwamba endapo kama kampuni hizo sita zitatimiza matakwa ya mikataba, tani zote 222,000 za korosho zitanunuliwa.

Advertisement

Kwa mujibu wa Kakunda, kuchelewa kwa wanunuzi kutimiza matakwa yao ya kimkataba kunatokana na masharti yanayowataka kujipanga na kuhakikisha kwamba punde tu baada ya malipo kufanyika basi wakusanye mzigo wao ili kutoa nafasi kwenye maghala yanayopaswa kuhifadhi mazo mengine.

“Wiki iliyopita, wawakilishi wa kampuni mbili za kigeni waliwasili nchini kwa ajili ya kukagua miundo mbinu ikiwemo barabara na bandari kabla ya kutoa mrejesho kwa nchi zao husika. Kwa ujumla, walionesha kuridhishwa,” alidokeza Kakunda.

Alipoulizwa kuhusu hali ya ubora wa korosho zenyewe, Kakunda alisema kwamba zipo katika hali nzuri hata kama zitaendelea kubaki mpaka Juali au Agosti mwaka huu.

Hatua hii mpya ya serikali imethibitisha wasiwasi na mashaka waliokuwa nayo baadhi ya wadau kuhusu uwezo wa Indo Power katika ununuzi wa korosho hizo, wakisema ni ndogo sana, huku baadhi yao wakisema kwamba inaweza kuwa inafanya kazi ya udalali ya kuiwakilisha kampuni nyengine (third party).

Advertisement