Kesi ya kupinga ukomo wa urais yatinga kortini

Tuesday September 3 2019

 

By James Magai, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Wakati Rais aliyeko madarakani, Dk John Magufuli akiwa ameshaweka wazi msimamo wake kwamba hana mpango wa kuendelea baada ya kumaliza muda wa uongozi katika nafasi hiyo kikatiba, mwananchi mmoja amefungua kesi akihoji ukomo huo wa uongozi katika nafasi hiyo.

Patrick Dezydelius Mgoya, mkazi wa Mbezi Beach jijini Dar es Salaam amefungua kesi hiyo dhidi ya mwanasheria mkuu wa Serikali na ilisajiliwa Ijumaa iliyopita na kupewa namba 19 ya mwaka 2019 katika Mahakama Kuu, Masjala Kuu.

Mgoya amefungua kesi hiyo chini ya kifungu cha 4 cha Sheria ya Utekelezaji Haki na Wajibu, Sura ya 3 ya mwaka 1994 na chini ya Ibara ya 30 (3) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977.

Kwa mujibu wa hati ya madai ya kesi hiyo, Mgoya anahoji Ibara ya 40 (2) ya Katiba ambayo inaweka ukomo wa mihula miwili tu ya miaka mitano mitano (10) ya uongozi katika nafasi hiyo ya urais.

Hivyo anaiomba mahakama hiyo itoe tamko na tafsiri ya maana sahihi na athari za masharti ya ibara hiyo.

Pia anaiomba mahakama itoe tafsiri ya maana dhahiri ya masharti ya Ibara ya 42 (2) ya Katiba kwa kuhusianisha na masharti ya Ibara za 13, 21 na 22 za Katiba hiyo. Vilevile anaiomba mahakama itoe tafsiri ya maana ya Ibara hiyo ya 40(2) kwa kuhusianisha na Ibara ya 39 ya Katiba.

Advertisement

Katika hati yake ya kiapo kinachounga mkono kesi hiyo, Mgoya anadai kuwa shauri hilo linatokana na kukinzana kwa ibara mbalimbali katika Katiba ya nchi, ambazo anazitaja kuwa ni Ibara ya 13, 21, 22(2), 39 na 40(2).

Anafafanua kuwa Ibara ya 13 inatoa usawa mbele ya sheria na kwamba hakuna sheria ambayo itatungwa na mamlaka yoyote nchini, kuweka sharti ambalo ni la ubaguzi ama wa dhahiri au kwa tahathira yake.

Kuhusu Ibara ya 21 anaeleza kuwa inaweka haki na uhuru wa kushiriki kikamilifu katika kufikia uamuzi juu ya mambo yanayomhusu yeye, maisha yake na au yanayolihusu Taifa.

Kwa Ibara ya 22 (2) anasema kuwa inaeleza kwamba kila raia anastahili fursa na haki sawa kwa masharti ya usawa, ya kushika nafasi yoyote ya kazi na shughuli yoyote iliyo chini ya mamlaka ya nchi.

Mgoyo anabainisha kuwa ibara hizo zote 13, 21 na 22 (2) zinapatikana katika sehemu ya Tatu ya Sura ya Kwanza ya Katiba, ambazo mtu yeyote anaweza kutafuta nafuu katika mahakama hiyo kuhusu ukiukwaji wake.

Anadai kuwa Ibara ya 40(2) ya Katiba inaweka ukomo wa muda wa mtu kuchaguliwa kuwa rais, kwamba mtu hawezi kuchaguliwa zaidi ya mara mbili kushikilia wadhifa wa urais.

Hivyo anadai kuwa masharti ya ibara hiyo ya 40(2) yanakiuka haki za kikatiba za Ibara za 13, 21 na 22(2) za Katiba hiyohiyo kwa kutoa mihula miwili tu ya raia kuchaguliwa kuwa rais kwa ukomo wa miaka 10 tu.

Mgoya anadai kuwa ukomo uliowekwa chini ya Ibara ya 40 (2) ya Katiba yanakinzana na haki ya kikatiba ya uhuru wa kushiriki katika shughuli za umma kwa kuchagua au kuchaguliwa kuwa rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na usawa mbele ya sheria chini ya Ibara ya 21 na 13. “Kwa msingi huo ninaomba amri ninazoziomba zikubaliwe na mahakama hii.”

Hatua hii ya kisheria iliyochukuliwa na mwananchi huyo imekuja wakati Rais Magufuli amesikika mara kadhaa katika nyakati na maeneo tofauti kuwa hataongeza muda wa kuongoza hata kidogo baada ya kumaliza muda wake.

Rais Magufuli amekuwa akibainisha msimamo wake huo baada ya baadhi ya watu kujitokeza hadharani na kutaka aendelee kuongoza hata baada ya kumaliza muda wake wa miaka 10 (kama atagombea tena na kushinda).

Kesi nyingine za Kikatiba kuhusu masuala ya uchaguzi zilizowahi kufunguliwa mahakamani ni ya kutaka mgombea binafsi aruhusiwe na nyingine ni kupinga wakurugenzi wa halmashauri kuwa wasimamizi wa uchaguzi.

Advertisement