Magufuli atoa maagizo kuwaokoa viboko Hifadhi ya Taifa Katavi

Thursday October 10 2019

 

By Peter Elias, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Rais John Magufuli ameiagiza Mamlaka ya Hifadhi za Wanyamapori nchini (Tawa) kuchimba bwawa na kujaza maji kwa ajili ya viboko wanaoishi katika Hifadhi ya Taifa ya Katavi.

Rais Magufuli ametoa agizo hilo leo Alhamisi Oktoba 10, 2019 wakati akizungumza na wananchi wa Mpanda Mjini ikiwa ni mwendelezo wa ziara yake mkoani Katavi.

Amesema alipita kwenye hifadhi ya Katavi na kuona maji yakiwa yamekauka kwenye mto wenye viboko na baadhi wameanza kupasuka kutokana na kupigwa jua.

“Ninawaagiza Tawa kuanzia kesho wapeleke maji  wachimbe bwawa wajaze maji. Wanyama hao wanatuingizia fedha nyingi, kwa nini tushindwe kuwatunza,” amesema Rais Magufuli.

Wakati huo huo, Rais Magufuli ameiagiza Wizara ya Maliasili na Utalii kufungua mabucha ya nyamapori kwa ajili ya watu wa Mpanda. Amesema maisha bora kwa Watanzania ni pamoja na kunufaika na rasilimali zao.

“Watu wa maliasili leteni hapa bucha ya nyamapori hata mara moja kwa wiki. Haya ndiyo maisha bora kwa kila Mtanzania. Haiwezekani umezaliwa karibu na hifadhi lakini hujawahi kula nyama ya porini,” amesema Rais Magufuli.

Advertisement

Kuhusu suala la wakimbizi, amesema baadhi  wamekuwa wakijihusisha na ujambazi na kuibua hofu kwa wakazi wa Mpanda. Amesema Serikali itaendelea kuchukua hatua za kisheria kwa wote watakaobainika.

 

 

Advertisement