Mnyika ataja mambo matano, Mashinji atamani

Katibu Mkuu pya wa Chadema, John Mnyika akizungumza wakati wa mkutano na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana. Picha na Ericky Boniphace

Dar es Salaam. John Mnyika amebainisha vipaumbele vitano atakavyoanza kuvifanyia kazi baada ya kupewa jukumu la kuwa Katibu Mkuu wa Chadema.

Amevitaja vipaumbele hivyo ni pamoja na kudai tume huru ya uchaguzi, maandalizi ya wagombea wa uchaguzi mkuu 2020, kuandaa ilani ya uchaguzi, kuendeleza sera ya Chadema ni msingi na Chadema Digital ili kuimarisha chama hicho.

Mnyika ametaja vipaumbele hivyo jana katika mkutano wake na waandishi wa habari makao makuu ya Chadema, Kinondoni jijini Dar es Salaam ikiwa mara ya kwanza tangu ateuliwe kumrithi Dk Vincent Mashinji, wiki iliyopita.

Wakati Mnyika akitaja vipaumbele vyake hivyo, Dk Mashinji aliyehudumu nafasi hiyo kwa miaka mitatu tangu 2016, alielezea alitamani kuendelea na ukatibu mkuu huku akibainisha mambo kadhaa aliyopanga kuyafanya iwapo angeendelea na wadhifa huo.

Dk Mashinji aliyechukua nafasi ya Dk Wilbrod Slaa aliyejiuzulu mwaka 2015, alisema miongoni mwa mipango yake inaweza kutumiwa na Mnyika kama ataona inafaa ili kukiimarisha chama hicho.

Katika maelezo yake, Mnyika alisema kwa kipindi kirefu wamekuwa wakidai tume huru ya uchaguzi bila mafanikio lakini safari hii watatilia mkazo suala hilo, akisema ni haki kuwa na tume huru ili uchaguzi uwe huru na wa haki.

“Kutokana na mazingira yaliyojitokeza katika chaguzi za marudio na ule wa serikali za mitaa tumeona ipo haja kuliwekea nguvu sana suala hilo. Kazi ya kwanza itakuwa kudai tume huru ya uchaguzi kwa njia mbalimbali,” alisema Mnyika ambaye pia ni mbunge wa Kibamba.

Alisema tofauti na miaka iliyopita hivi sasa Chadema itakuja na mfumo mpya utakaohakikisha wagombea wa nafasi mbalimbali wanaandaliwa mapema kabla ya uchaguzi mkuu.

“Tumeshazindua sera mbadala, kinachofuata ni maandalizi ya ilani ya uchaguzi mkuu 2020. Tutafanya kazi ya kuzipitia sera na kuangalia hali halisi ya nchi kwa sasa na kupata vipaumbele vya wananchi ili kuandaa ilani ya uchaguzi itakayoifanya Chadema izidi kukubalika” alisema Mnyika.

Pia alisema wataendeleza kazi ya Chadema ni msingi ili kuwa na mtandao thabiti wa kuingia kwenye uchaguzi mkuu kukiwa na nguvu ya umma (peoples power) kauli mbiu ya chama hicho.

“Chadema digital, hii tekinolojia ya habari na mawasiliano itatumika kufanikisha mabadiliko nchini. Haya ni mambo matano yatakayofanyika ikiwa ni sehemu ya lengo kuu la kuchukua dola mwakani,” alisema Mnyika.

Naye Dk Mashinji alizungumza na Mwananchi jana lililomuuliza kama angetamani kuendelea na ukatibu mkuu, alijibu; “`Yeah of course’ (ndio kwa kweli)”.

Hata hivyo, Dk Mashinji hakutaka kuingia kwa undani kuzungumzia kuhusu suala la kutoteuliwa kuendelea na wadhifa huo licha ya kutaka kubakia.

Mwananchi lilipotaka kujua ni jambo gani kubwa angelifanya kama angeendelea na ukatibu.

Dk Mashinji alieleza alipania kuandaa mikakati ya chama hicho kushinda uchaguzi wa mwaka 2020.

“Ili kuhakikisha tunapata wagombea wanaotokana na wananchi, hivyo tungekwenda kutekeleza agizo la kamati kuu la kuwaomba wanachama wanaotaka kugombea urais, ubunge na udiwani wajitokeze.

“Ningelipenda watu hao watangazwe mapema ili wananchi waanze kuwatafiti na hatimaye kuwa na kiongozi anayetokana na wao na hili lingefanyika Januari mwakani.

“Inasaidia kukijenga chama kwani tungewapa nafasi ya kujitambulisha kwa wananchi nao wangekishauri chama hivyo kuwa na wagombea wanaokubalika kwa wananchi,” alieleza Dk. Mashinji, ambaye wazo kama hilo liligusiwa na Mnyika jana.

Dk Mashinji alishauri, hata hivyo, nguvu kubwa inapaswa kuelekezwa kwenye nafasi ya urais kwani ni muhimu wagombea wakajulikana mapema kwa wananchi ili waweze kuwatafiti ili kupata kiongozi atakayeleta mabadiliko.

“Nchi nyingine wagombea urais wanajulikana hadi miaka miwili au mmoja kabla na hili linawafanya watu kuchambua makandokando yake, ili aweze kujulikana na kukijenga chama na kujitambulisha pia na hata tukija kufanya kura ya maoni tunafanya kwa mtu anayejulikana,” alisema daktari huyo wa magonjwa ya binadamu.

Alipoulizwa kuhusu kauli tata ambazo amekuwa akitoa tangu atolewe ukatibu mkuu wa chama hicho, Dk Mashinji alijibu, “Kazi ya siasa ni kuwafikirisha watu, kuna wengine watasema hiki, mwingine atasema vile.”

Baadhi ya kauli zake ni kama ile aliyokaririwa na gazeti hili wiki iliyopita akimtaka Mnyika afanye kazi kwa ufanisi ili chama kisihodhiwe na watu wachache.

Pia aliandika kwenye mtandao wa kijamii wa twitter, “Haikuwa rahisi lakini tumetoka wote salama na tukiwa wamoja. Kichwani mwa kila kiongozi kumejaa siri nyingi sana... Eeh, Mungu mwenye enzi, nakushukuru sana kwa kutulinda mpaka tukatoka salama. Asanteni wana Chadema wote, na Watanzania kwa ushirikiano mwema!”