Moto wawaka maaskofu KKKT

Askofu Fredrick Shoo

Moshi. Moshi unafuka ndani ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) kutokana na taarifa zinazodai kuwa kuna mpango wa kumshinikiza mkuu wa kanisa hilo, Askofu Fredrick Shoo ajiuzulu.

Askofu Shoo alifanikiwa kurejea kwenye nafasi hiyo katika uchaguzi uliofanyika Agosti mwaka jana mkoani Arusha, lakini baada ya mpinzani wake, Abednego Keshamshahara kujitoa katika raundi ya pili.

KKKT ni umoja wa dayosisi za kanisa hilo ambazo zinajitegemea na zina mamlaka kamili yanayoelezwa katika katiba zao.

Tayari hofu imetanda makao makuu ya KKKT baada ya kuenea kwa uvumi kuwa shinikizo la kutaka kumuengua mkuu huyo wa kanisa linatoka kwa maaskofu wenzake.

Wakati hali ikiwa hivyo, inadaiwa maaskofu kutoka dayosisi 21 kati ya 26 waliitana jijini Dodoma kati ya Februari 4-6 kufanya kikao cha kutafuta njia ya kuliepusha kanisa na mgogoro huo.

Hata hivyo, chanzo kingine ndani ya kanisa hilo kimelieleza gazeti hili kuwa maaskofu waliohudhuria kikao hicho ni 10 tu kati 21 waliokuwa wamethibitisha awali kuwa wangehudhuria.

Baadhi ya wachungaji, wanaona mgogoro huo ni wa kutengenezwa, ikiwa ni mwendelezo wa nguvu kubwa inayotumika kutaka kumng’oa, baada ya njama hizo kugonga mwamba Agosti 25, 2019.

‘Binafsi ukiniuliza kama mchungaji ninayelifahamu kanisa nitakujibu kuwa hiki kinachoendelea ni mwendelezo wa kundi lililokuwa limejipanga kumuangusha mwaka jana,” alidai mchungaji mmoja ambaye hakutaka jina lake litajwe.

Chanzo kingine kinadai kiini ni hatua ya baadhi ya maaskofu kutaka kuanzisha chombo kipya kitakachoitwa Baraza la Maaskofu ambacho kitakuwa na rais wake tofauti na mkuu wa kanisa kama ilivyo sasa.

Lakini chanzo kingine kinadai kuwa masuala ya kifedha hayajakaa sawa ndio maana Halmashauri Kuu ya KKKT ikaagiza manaibu katibu wakuu watatu, waondolewe.

Mbali na hilo, taarifa za uhakika ambazo tunazo, Askofu wa Dayosisi ya Kaskazini Mashariki, Dk Stephen Munga amemuandikia Askofu Shoo kuhusu mgogoro huo.

Habari hizo zinadai ujumbe huo wa Askofu Munga unatokana na barua ya mkuu wa kanisa ya Januari 31, 2020 kwenda kwa wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Kanisa hilo.

Katika barua hiyo, yenye kurasa 4, Askofu Shoo anaanza kwa kunukuu kanuni XII (A) ya katiba ya kanisa hilo toleo la 2015, akielezea nafasi ya mkuu wa kanisa katika kuongoza.

“Atakuwa kiongozi mkuu wa mambo ya kiroho na mambo ya kazi katika kanisa hili. Atachunga, atashauri na ataonya kanisa kuwa na uaminifu kwa imani ya kweli,” inasema barua hiyo.

Ni kutokana na kipengele hicho, Askofu Shoo anadaiwa kukitumia kubatilisha maagizo ya Halmashauri Kuu ya kuwaondoa kazini watendaji wanaotakiwa waondolewe kutokana na matatizo katika masuala ya kifedha.

Askofu Shoo aliandika katika barua hiyo kuwa baada ya kufuatilia, kuchunguza, kutafakari na kuomba sana kuhusu maamuzi hayo ya Halmashauri Kuu, ameona ashauri utekelezaji usitishwe.

“Ikumbukwe kuwa chanzo cha haya yote ni mkopo uliochukuliwa benki kinyemela na watu waliojifanya wadhamini wa kanisa. Manaibu tunaotaka kuwaondoa hawajatuhumiwa popote,” alisema.

“Watumishi walengwa wameonyesha kuumia na kuona kuwa hawatendewi haki. Baadhi yao wamedai kuwa wanaandamwa kwa sababu ya visasi kwa kutekeleza wajibu wao kwa uadilifu.”

Mkuu huyo amesema baada ya kufuatilia ameona ashauri uamuzi wa kuwafuta kazi usitishwe.

“Ni hekima na afya kwa kanisa letu kusitisha utekelezaji wa mapendekezo ya kamati maalum na maamuzi ya kuwaondoa manaibu wakuu wote kazini kwa sasa,” ameandika.

“Ninafanya hivi kwa dhamira safi ili mtazamo wangu uwe bayana wala silazimishi Halmashauri Kuu kukubaliana na mtazamo huu. Kimsingi nimetahadharisha zipo athari kubwa kisheria na kifedha.

“Endapo kutakuwapo haja ya maelezo ya kina kuhusu haya niliyoyaandika hapa nitakuwa tayari kuyatolea ufafanuzi na kuwajibika kwayo mbele ya kikao cha kawaida cha Halmashauri Kuu”

Kikao cha kawaida cha Halmashauri kuu ya KKKT kimepangwa kufanyika Aprili 2020 na baadaye mkutano mkuu.

Ujumbe wa Askofu Munga

Hata hivyo, barua hiyo ya mkuu wa Kanisa inaonekana kuibua mgawanyiko na Askofu Munga amemueleza waziwazi kuwa ameligawa kanisa.

“Inasikitsha kuwa umelimega kanisa bila sababu zozote za msingi na hii inasikitisha. Inaelekea huelewi kuwa umoja wa KKKT ni wa maridhiano na kamwe si wa kimamlaka ya utawala,” ameandika Munga.

“Kulingana na maridhiano ya kuundwa kwa KKKT, wewe si archbishop bali ni askofu mmoja anayewatangulia wengi katika mambo ya kazi za umoja na si zaidi ya hapo.

“Hii ndio sababu nilikuandikia email nikikuambia nenda na maaskofu. Ujue maaskofu ni wakuu wenzako ambao huna mamlaka ya kuingilia mambo ya dayosisi zao.

“Unakiri wazi kwenye waraka wako kwamba unaweza kubadilisha na kuvunja maagizo ya Halmashauri Kuu kwa utashi wako na bila shaka kwa ushauri wa pembeni.

“Hili ni kosa kubwa sana na uvunjifu wa katiba ya KKKT. Tena unasambaza haya kwa njia ya mitandao kama kwamba hujui maana ya confidentiality (usiri).

“Kwa nini unafanya makosa haya ya wazi?! Inaelekea unafukuzana na kivuli chako mwenyewe unapodhani kuwa kuna maaskofu wanaokuhujumu.”

Askofu Munga alipotafutwa jana ili kuzungumzia ujumbe huo ambao aliutuma kwa email kwa maaskofu wote juzi Januari 7,2020 saa 4:18 asubuhi, hakupatikana kwani simu iliita bila majibu.