Siri za kimkakati Chadema shakani

Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole (kulia) akipena mkono na aliyekuwa Katibu Mkuu Chadema, Dk Vicent Mashinji ambaye ameomba kujiunga CCM katika mkutano uliofanyika katika ofisi ndogo za chama hicho zilizopo Lumumba Jijini Dar es salaam. Picha na CCM

Dar es Salaam. Chadema inaendelea kuandika historia ambayo kimsingi inaacha maswali mengi kwa wafuatiliaji wa masuala ya kisiasa.

Miongoni mwa maswali hayo ni usalama wa mikakati ya chama hicho kuelekea Uchauzi Mkuu wa mwaka huu, hasa baada ya baadhi ya viongozi wake na makada wake maarufu kutimkia CCM.

Jana chama hicho kilipata pigo baada ya aliyekuwa katibu mkuu wake, Dk Vincent Mashinji kujiunga na CCM, akiwa ni kiongozi wa nne kutoka ndani ya Kamati Kuu kufanya hivyo.

Hata hivyo, uongozi wa Chadema ulisema kuondoka kwa Dk Mashinji hakutakiathiri kwa namna yoyote chama hicho kwa kuwa kilifahamu atafanya hivyo na kuwa kina orodha ya makada wake wengine wenye mpango wa kutimka.

Msimamo huo unashabihiana na ule wa mchambuzi wa masuala ya kisiasa kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Muhidin Shangwe aliyelieleza Mwananchi kuwa haoni kama kuhama kwa Dk Mashinji kutailetea madhara Chadema.

“Dk Mashinji na wenzake sidhani kama wana madhara sana. Hamahama ikitokea kwa nadra inakuwa na tatizo, lakini kila ukiamka unakuta (mtu) kahama, inageuka na kuwa ya kawaida na haileti shida labda anayehama awe ni mkubwa sana.

“Wamehama wangapi? Mpaka mimi nimezoea. Sumaye alivyohama hata alivyokwenda upinzani sijaona zaidi ya kusema upinzani una mawaziri wakuu wawili lakini hakukuwa na tija na tunapoelekea watahama wengi,” alisema Dk Shangwe.

Uamuzi wa Dk Mashinji umekuja miezi michache tangu alipong’olewa katika nafasi ya katibu mkuu wa Chadema Desemba mwaka jana wakati wa uchaguzi mkuu wa ndani ya chama hicho.

Akizungumza jana kwenye ofisi ndogo za CCM zilizoko mtaa wa Lumumba jijini Dar es Salaam, Dk Mashinji alisema ameamua kujivua uanachama wa Chadema kutokana na kuona kuna haja ya kuchochea maendeleo ya watu na vitu.

Dk Mashinji anakuwa kigogo wa nne aliyefikia nafasi ya juu ya mjumbe wa kamati kuu ya Chadema kuhama chama hicho ndani ya takriban miezi 12.

Vigogo wengine ambao walikuwa wajumbe wa kamati kuu waliohama ni pamoja na mawaziri wakuu wa zamani Edward Lowassa na Frederick Sumaye pamoja na aliyekuwa mbunge wa Ndanda, Cecil Mwambe.

Mbali na Lowassa aliyeondoka Chadema Machi 1, 2019, wenzake watatu wameondoka mwezi huu, wakitanguliwa na Sumaye aliyeondoka Februari 10 na Mwambe Februari 15.

Kitendo hicho cha vigogo kuondoka kinatia wasiwasi kuhusu usalama wa taarifa na siri za kimkakati kuelekea uchaguzi mkuu baadaye mwaka huu, kutokana na ukweli kwamba viongozi hao waliwahi kushika nafasi zilizokuwa zikiwapa fursa ya kuingia katika vikao nyeti vya uamuzi.

Wakati Lowassa, Sumaye na Mwambe walikuwa wanaingia katika vikao vya kamati kuu, Mashinji akiwa katibu mkuu wa chama ndiye alikuwa anaongoza sekretarieti ambao hupanga mikakati na ajenda za vikao vya chama.

Wachambuzi wa mambo wanasema kitendo cha wanasiasa hao kuhamia CCM, wanaweza kuvujisha mipango na mikakati na mbinu za uendeshaji wa Chadema kwa mshindani walikohamia.

Hata hivyo, John Mrema, mkurugenzi wa Itikadi, Uenezi, Mawasiliano na Mambo ya Nje wa Chadema, alisema kuondoka kwa Mashinji na wengine wanaotarajia kuondoka hakutakuwa na athari zozote kwa chama hicho.

“Mashinji baada ya mtu aliyetaka kuwa mgombea wake wa urais kupitia Chadema, Sumaye kuondoka na mwenyekiti wake mtarajiwa wa chama ambaye ni Mwambe kuondoka, tulitegemea na yeye angeondoka na imekuwa hivyo.

“Bado tunategemea chaguo lake lingine, ambaye ni mtu ambaye aligombea nafasi ya makamu mwenyekiti naye atakwenda CCM na wajumbe wengine watatu ambao waliahidiwa kuwa wajumbe wa sekretarieti nao watakwenda,” alisema Mrema.

Pamoja na kwamba Mrema hakutaka kumtaja mgombea huyo wa nafasi ya makamu mwenyekiti, lakini waliojitokeza kuchukua fomu walikuwa sita ambao ni; Ahobokile Mwaikenda, Tundu Lissu, Saed Kubenea, Tiba Richard na Sophia Mwakagenda. Lissu aliibuka mshindi huku wengine wakijitoa.

Mwambe alishindwa kwenye nafasi ya mwenyekiti wakati Sumaye alidondoka kama mgombea pekee wa nafasi ya Mwenyekiti Kanda ya Pwani.

“Tulishachukua hatua tangu uchaguzi mkuu wa chama Desemba mwaka jana na wale waliokuwa wamejipanga hawakuweza kupenya. Kama aliondoka Dk Slaa aliyekuwa katibu mkuu kwa miaka kumi na hakuwa na athari, basi hata huyu hawezi kuwa na athari,” alisema Mrema.

Mrema alipoulizwa Chadema watamkumbuka Dk Mashinji kwa jambo gani, alisema:

“Kuna mambo yake mazuri alifanya kwa kushirikiana na sekretarieti, alikuta tunaanza maandalizi ya kuandika sera ya chama ya 2018, akaliendeleza na kuikamilisha, hilo tutamkumbuka.”