Tasaf waja na mpango mwingine kusaidia kaya masikini

Muktasari:

Baada ya utafiti wa mapato na matumizi ya kaya kwa mwaka 2017/2018 kuonyesha  asilimia 9.7 ya Watanzania wanaishi kwenye umaskini uliokithiri,  Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (Tasaf) umekuja na kipindi cha pili cha awamu ya tatu ya mpango wa kunusuru kaya maskini ili kuzifikia kaya zilizoachwa  kipindi cha kwanza.

Dar es a Salaam. Baada ya utafiti wa mapato na matumizi ya kaya kwa mwaka 2017/2018 kuonyesha  asilimia 9.7 ya Watanzania wanaishi kwenye umaskini uliokithiri,  Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (Tasaf) umekuja na kipindi cha pili cha awamu ya tatu ya mpango wa kunusuru kaya maskini ili kuzifikia kaya zilizoachwa  kipindi cha kwanza.

Hayo yameelezwa leo Alhamisi Februari 13, 2020 na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Utumishi na Utawala Bora), George Mkuchika.

Mkuchika amesema mpango huo unatekelezwa ili kupunguza umaskini na athari zake kwa wananchi na kuwezesha nchi kufikia uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025.

Waziri Mkuchika  amesema kipindi  cha pili cha mpango huo kimekuja kufuatia awamu ya kwanza iliyohitimishwa Desemba 2019 kushindwa kuwafikia walengwa wote, umasikini kuendelea kuwatafuna.

Amesema ni asilimia 70 pekee ya wananchi wanaoishi katika hali duni ndio walifikiwa na mpango huo, kwamba  asilimia 30 iliyosalia inaenda kufikiwa katika kipindi cha pili.

Amesema kipindi hicho cha pili kitakachozinduliwa Februari 17 na Rais John Magufuli kitahusisha halmashauri 185 na kaya 300,000 zitanufaika.

“Katika kipindi cha kwanza tulifikia kaya 1.1 milioni lakini lengo letu awamu ya tatu ifikie kaya 1.4 milioni hivyo tutaongeza hizo kaya 300,000,”

“Mkazo mkubwa katika kipindi cha pili utawekwa katika kuwezesha kaya zitakazoandikishwa kwenye mpango ni kufanya kazi ili kuongeza kipato,” amesema Mkuchika

Mkurugenzi Mtendaji wa Tasaf,  Ladslaus Mwamanga amesema Sh2 trilioni zimetengwa kwa ajili ya utekelezaji wa kipindi hicho cha pili cha awamu ya tatu ya mpango wa kupunguza umaskini.

Amesema ili kuepuka malalamiko wameboresha namna ya kuwapata walengwa kwa kufanya zoezi hilo kwa kutumia teknolojia.

“Tumeshafanya majaribio katika halmashauri tatu kwa hiyo teknolojia mpya na tumeona imekuwa na matokeo chanya na tumejiridhisha walengwa ndiyo watakaowafikiwa,” amesema Mwamanga.