Virusi hatari vyazidi kusambaa, Serikali yasema imejipanga

Thursday January 23 2020

Abiria wa usafiri wa ndege wakiwa wamefunika

Abiria wa usafiri wa ndege wakiwa wamefunika pua na mdomo kwa ajili ya kujikinga na maambukizi ya virusi vya Corona, wakati wapo katika Uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Hong Kong. Ugonjwa huo umelipuka nchini China na kusababisha vifo vya watu tisa na wengine zaidi 200 wanaugua. Picha na AFP 

By Herieth Makwetta, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Wakati Shirika la Afya Duniani (WHO) likikutana leo jijini Geneva kuamua kama mlipuko wa virusi hatari nchini China unastahili kutangazwa kama “janga la dharura la afya kimataifa”, Tanzania imesema inafuatilia kwa karibu na imeweka tahadhari mipakani.

Virusi hivyo vya corona vinavyofanana na ugonjwa wa SARS (ugonjwa unaoathiri mfumo wa hewa), hadi jana ulikuwa umeua watu tisa nchini China na ulikuwa ukienea sehemu kadhaa, huku mgonjwa mmoja akibainika Marekani na Uingereza ikichukua hatua kudhiti wasafiri katika ndege zinazotoka moja kwa moja China.

Tayari virusi hivyo vimeshaathiri watu 440 nchini China na wengi wao wakitoka Wuhan, AFP imeripoti. Li Bin wa Kamisheni ya Afya ya Taifa ya China alikaririwa na AFP akisema watu 1,394 walikuwa wakiendelea kuangaliwa na wauguzi.

Lakini Naibu Waziri wa Afya, Dk Faustine Ndugulile amesema tayari mifumo ya udhibiti ipo katika maeneo yote wanayopita wageni kuingia nchini.

“Kwa kuwa dunia ni kama kijiji, Serikali ya Tanzania inafuatilia kwa karibu mlipuko wa ugonjwa huu huko China,” alisema Dk Ndungulile.

“Hawa ni wenzetu na tuna ukaribu nao. Wataalamu wa afya hapa nchini tayari wanafanya ufuatiliaji kupitia mifumo yetu ambayo ipo tayari kugundua wagonjwa.

Advertisement

“Utaona hata huko China wenzetu pia wana vifaa kama vya kwetu vya thermo scanner. Sisi tumeifunga katika maeneo yote ambayo wageni wanaingia.”

Dk Ndugulile alisema wamefunga vifaa hivyo katika viwanja vya ndege ili kubaini mwenye homa, baada ya hapo tutamchukua na kumhoji ametoka wapi, historia yake ya safari. Yeyote anayehisiwa tunamuweka pembeni kwa uchunguzi zaidi.”

Naibu waziri huyo alisema mashine hizo zina uwezo wa kuwatambua watu wengi.

“Hata wawe 100 au ndege nzima vifaa vyetu ni vya kisasa sana. Si lazima kukagua mtu mmoja mmoja, hivyo vina uwezo wa kumbaini mgonjwa na tukamchukulia hatua za kumwangalia zaidi,” alisema.

Sampuli ya virusi vilivyochukuliwa kutoka kwa mgonjwa na kuchunguzwa katika maabara na maafisa wa serikali ya China pamoja na wale wa Shirika la Afya Duniani (WHO) zinaonyesha ugonjwa huo unafanana na SARS kwa asilimia 80.

Korea Kusini pia iliripoti mtu aliyebainika kuwa na virusi hivyo Jumatatu baada ya Thaialnd na Japan.

Jijini Geneva, WHO inatarajiwa kutoa tamko la hali ya dharura iwapo itabaini virusi hivyo ni “hatari, vya dharura, si vya kawaida au havikutegemewa”.

Tamko hilo litamaanisha virusi hivyo vina hatari ya kusambaa zaidi duniani na kunahitajika kuchukuliwa hatua na jumuiya ya kimataifa.

Na tamko hilo likitolewa litakuwa likipitiwa kila baada ya miezi mitatu na kamati ya dharura ya WHO.

Kuhusu Coronavirus

Virusi hivyo ni familia kubwa ya virusi sita na kirusi hicho kipya kitaongeza idadi hiyo kufikia saba na ni maarufu kwa kusababisha ya maambukizi miongoni mwa binadamu.

Akiongea na AFP, Dk Nathalie MacDermott wa Chuo cha King jijini London alisema inaonekana kuna uwezekano mkubwa virusi hivyo vinasambazwa na kwa matone yanayoingiwa hewani baada ya mtu kukohoa au kupumua.

Jumanne, madaktari katika Chuo Kikuu cha Hong Kong walichapisha andiko la awali likionyesha kusambaa kwa virusi hivyo, likisema kuwa kuna watu 1,343 wanaohisiwa kuwa na virusi hivyo jijini Wuhan -- sawa na makisio ya wiki iliyopita ya watu 1,700 yaliyofanywa na wataalamu wa Chuo cha Imperial cha London.

Taarifa hizo mbili ni kubwa kuliko taarifa rasmi.

Mlipuko huo umekuja wakati China ikijiandaa kwa sherehe za mwaka mpya maarufu kama Lunar New Year Holiday, ambazo huhudhuriwa na mamilioni ya watu wanaosafiri sehemu mbalimbali kuona familia.

Profesa Antoine Flahault, mkurugenzi wa Taasisi ya Afya ya Dunia katika Chuo Kikuu cha Geneva aliiambia AFP kwamba kutokana na ukweli kwamba virusi havionekani kuwa hatari kwa watu wengi, kimsingi hilo linatakiwa litie hofu zaidi kwa kuwa hali hiyo huwezesha watu kusafiri umbali mrefu kabla ya kubainika kuwa na virusi.

“Wuhan ni sehemu kubwa ya makutano na kwa kuwa usafiri ndio kitu kikubwa kinachofanyika wakati wa kuelekea mwaka mpya wa China, wasiwasi unatakiwa kuendelea kuwa mkubwa,” alisema Dr Jeremy Farrar, mkurugenzi wa taasisi ya Wellcome.

Advertisement