Vyama vyaihoji NEC uchaguzi huru, vyashauri vita vya corona

Tuesday March 24 2020

Mkurugenzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC),

Mkurugenzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Dk Wilson Mahera (kulia) akimkabidhi naibu katibu mkuu Chadema (Bara), Benson Kigaila orodha ya majina ya vituo vya uchaguzi, wakati wa mkutano wa wadau wa vyama vya siasa uliofanyika jijini Dar es Salaam jana. Pichana Said Khamis 

By Elias Msuya, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Watendaji na viongozi wa vyama vya siasa wamehoji uhuru wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), wakiitaka ithibitishe kwa vitendo ahadi ya Rais John Magufuli ya kuwa na uchaguzi huru na wa haki.

Wanasiasa hao pia wameishauri NEC isitishe shughuli za uboreshaji wa Daftari la Wapigakura wakati huu wa vita dhidi ya maambukizi ya ugonjwa wa virusi vya corona.

Walisema hayo katika mkutano wa pamoja na viongozi wa NEC uliofanyika jana jijini Dar es Salaam.

Ahadi ya uchaguzi huru na wa haki ilitolewa na Rais mapema mwaka huu wakati akizungumza na mabalozi na wawakilishi wa taasisi za kimataifa katika hafla ya kuukaribisha mwaka jijini Dar es Salaam.

Ahadi hiyo pia ilirudiwa na Waziri wa Mambo ya Nje, Profesa Palamagamba Kabudi wakati alipohutubia mkutano wa Umoja wa Mataifa jijini Geneva, Uswisi.

Katika mkutano huo, mwenyekiti wa Baraza la Vyama vya Siasa, John Shibuda alisema NEC ina jukumu la kuthibitisha kauli ya Rais John Magufuli kuwa uchaguzi wa mwaka huu utakuwa huru na wa haki.

Advertisement

Alisema licha ya Rais kutoa ahadi hiyo, kuna utata katika maandalizi yanayofanywa na tume hiyo, ikiwa ni pamoja na matumizi ya wakurugenzi wa halmashauri kuendelea kuwa wasimaizi wa uchaguzi.

“Ma-DED hawa watatangaza matokeo ya kukipendelea chama tawala kwa sababu wanalinda ajira zao,” alisema Shibuda.

Vyama vya upinzani vilifanikiwa kuwaondoa wakurugenzi hao kwa hukumu ya kesi ya Mahakama Kuu baada ya kujenga hoja kuwa ni wateule wa Rais, ambaye ni mwenyekiti wa CCM na kuwasilisha orodha ya wakurugenzi ambao ni wakereketwa wa chama hicho tawala.

Hata hivyo, Serikali ilikata rufaa na baadaye Mahakama ya Rufani ikawarejesha.

Jana, Shibuda, ambaye aliiomba Ofisi ya Waziri Mkuu inayosimamia mambo ya siasa kuliwezesha baraza analoliongoza, pia alishauri NEC ivikutanishe vyama vya siasa, Takukuru, Tamisemi na wakuu wa wilaya ili kuruhusu shughuli za kisiasa zifanyike bila upendeleo.

“Viongozi wa vyama vya siasa wanaokwenda mikoani wanakamatwa hata wanapofanya mikutano ya ndani,” alisema.

“Wakifanya vikao vya ndani Dar es Salaam hawakamatwi, wakienda mikoani wanakamatwa. Hii inatengeneza dosari kwamba uchaguzi unaosimamiwa na tume ya uchaguzi hautakuwa uwazi na ukweli,” alisema Shibuda.

Kauli hiyo ya Shibuda iliungwa mkono na mkurugenzi wa kampeni na uchaguzi wa NCCR -Mageuzi, Martin Mng’ong’o ambaye alitoa mfano wa uchaguzi wa Serikali za Mitaa uliofanyika Novemba 24, 2019 ambao baadhi ya vyama vya siasa viliususia.

“Hata wakati wa uchaguzi wa Serikali za Mitaa tulikaa na Tamisemi vizuri tukajadili kanuni, lakini katika utekelezaji ikawa ni ajali ya kisiasa. Mtu anaenguliwa eti hajui kusoma na kuandika wakati ni mwalimu mstaafu,” alisema Mung’ong’o.

Mung’ongo pia aliitaka tume hiyo kukutana na wadau wengine wasio wanachama wa vyama vya siasa lakini ni wapigakura.

Akijibu hoja hizo, Mwenyekiti wa Nec, Jaji Semistocles Kaijage alisema ameyapokea, huku pia akieleza kuwa wamekuwa wakikutana na makundi tofauti ya wananchi na kuyashirikisha hatua zote za maandalizi ya uchaguzi.

Uboreshaji wa daftari

Kuhusu uboreshaji wa Daftari la Wapigakura ulioanzia Julai 28, 2019 na kuisha Februari 23, baadhi ya viongozi wa vyama hivyo waliitaka NEC kusitisha kazi hizo kupisha mapambano ya maambukizi ya ugonjwa wa virusi vya corona unaotikisa dunia kwa sasa.

“Sasa hivi ni Machi na tumebaki na miezi michache kufikia uchaguzi mkuu. Kuna hatari ya ugonjwa wa corona, mtafanyaje uboreshaji wa awamu ya pili na hali hii?” alihoji Rashid Rai wa Chama cha AFP.

“Kwa nini hizo fedha za uboreshaji msizipeleke katika mapambano ya ugonjwa huo?”

Kauli kama hiyo ilitolewa na Costa Kibonde wa Demokrasia Makini. “Mimi ni miongoni mwa wagombea urais mwaka huu. Nataka wapigakura wangu wawe na afya njema. Tunataka uboreshaji wa daftari la wapigakura usitishwe,” alisema.

Licha ya kukiri kuwa ugonjwa huo umeathiri ratiba za NEC, Jaji Kaijage alisema hawawezi kusimamisha kazi hiyo bila kuwasikiliza wadau wake, ambao ni pamoja na Serikali.

Ugonjwa huo ambao ulianzia jiji la Wuhan nchini China umeshaua zaidi ya watu 14,000 kote duniani na wengine zaidi ya 300,000 wameambukizwa.

Hadi sasa Tanzania imegundua watu 12 walioambukizwa virusi hivyo na wote waligundulika baada ya kuingia wakitoka nje ya nchi.

Naye naibu katibu mkuu wa Chadema, Benson Kigaila alisema kuna hatari ya wananchi wengi kutopiga kura.

“Mwaka 2015 baadhi ya wanafunzi waliandikishwa shuleni, wakati wa uchaguzi wakawa wamefunga shule, wengi hawakupiga kura,” alisema Kigaila.

Hoja hiyo iliungwa mkono na Idd Mkanza, ofisa mipango wa CUF, aliyesema tume inatumia fedha nyingi, lakini wananchi wengi hawapigi kura.

Advertisement