Wabunge 15 wa kwanza viti maalum walivyopatikana 1985

Uchaguzi mkuu wa Oktoba 27, 1985 ulifanyika chini ya mfumo wa chama kimoja cha siasa, CCM.

Kwa mujibu wa Sheria ya Uchaguzi, mabadiliko kadhaa yalifanyika kama kuongeza idadi ya majimbo ya uchaguzi kutoka 106 hadi 119, kuondoa wabunge 20 wa mikoa waliokuwa wakichaguliwa na wabunge na kuweka nafasi 15 za viti maalumu vya wanawake.

Tangu mwaka 1980, Bunge lilipitisha uamuzi wa kutenga asilimia 10 ya viti kwa ajili ya wanawake.

Idadi hii imekuwa ikiongezwa mara kwa mara tangu wakati huo hadi kufikia asilimia 37 mwaka 2015.

Tangu uchaguzi wa Oktoba 27, 1985, idadi hiyo imekuwa ikiongezeka.

Kwa mfano, mwaka 1985 (idadi ilikuwa asilimia 10), mwaka 1995 (asilimia 15), mwaka 2000 (asilimia 20), mwaka 2005 (asilimia 30), 2010 (asilimia 35) na mwaka 2015 (asilimia 37).

Wabunge hao 15 wa viti maalumu na wengine 15 wa Taifa walianza kuchaguliwa Novemba 2, 1985 katika kikao cha kwanza cha Bunge jipya la Jamhuri ya Muungano kilichofanyika ukumbi wa Karimjee mjini Dar es Salaam.

Kazi nyingine ya kikao hicho, ilikuwa kumchagua Spika wa Bunge na kuwaapisha wabunge.

Adam Sapi Mkwawa alichaguliwa kuwa Spika wa bunge hilo.

Wagombea 60 wa viti maalumu walijitokeza na 30 walihojiwa na wabunge wakiwa kama kamati ya chama saa 4:00 asubuhi kwenye ukumbi wa Bunge.

Kila Jumuiya ya Wananchi kati ya tano zilizokuwapo, Washirika, Wazazi, Vijana, Jumuiya ya Wafanyakazi Tanzania (Juwata) na ya Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT), ilitoa majina sita ya wagombea kwa ajili ya viti 15 vya ubunge wa Taifa wakati kulikuwa na orodha nyingine ya wanawake 30 waliokuwa wanagombea viti maalumu.

Miongoni mwa wanawake 30 waliogombea viti hivyo ni Zaitun Fadhili, Thereza Olban Ali, Ashura Abeid Faraji, Lucy Lameck, Getrude Mongella, Dora Bantu, Mwanamkuu Makame Kombo na Fatma Said Ali.

Wengine ni Mosi Tambwe, Elizabeth Mwakatobe, Zaina Rashid, Mpaji Juma, Asha Chiliko, Edith Kapinga na Hulda Kibacha.

Pia walikuwamo; Zainabu Matovolwa, Fatma Said Jadi, Corona Busongo, Elizabeth Minde, Monica Kuga na Amina Salum Ali ambaye sasa ni waziri wa biashara, viwanda na masoko, wa Zanzibar.

Pia alikuwamo Zainabu Kawawa, Joyce Benjamin Hamisi, Zakia Meghji, Amina Feruzi, Venus Kimei, Jito Ram, Tatu Ali Abdallah, Mary Luwilo na Luteni Minael Mdundo.

Walioshinda ni Fatma Saidi Ally, aliyepata kura 143, Tatu Abdallah (122), Amina Salum Ali (114), Thereza Olban Ali (110) na Ashura Abeid Faraji (105).

Tanzania Bara ni Getrude Mongella (98), Mosi Tambwe (87), Zaituni Nyapili (71), Zakia Meghji (68) na Dk Zainab Gama (66).

Wabunge walioshinda kwa kura za kapu zilizowajumuisha wote ambao hawakupita kwa upande wa Tanzania Bara na visiwani, ni Amina Saad Ferizo (kura 71), Jito Ram (70), Mwanamkuu Makame Kombo (67), Corona Busongo (66) na Lucy Lameck (60).

Eda Sanga, mkurugenzi wa zamani wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (Tamwa) aliiambia Mwananchi kuwa kuanzishwa kwa viti hivyo kulianza kutoa fursa kwa wanawake kupaza sauti zao na kuonyesha kuwa wanaweza.

“Kuanzishwa kwa viti hivi maalumu tuliona ni jambo zuri, kihistoria, wanawake walikuwa wametengwa na kimtazamo wa jamii wanawake hawana hadhi, lakini tulipata mwanya kwa wanawake kupaza sauti zao na wao kuonekana wanaweza kuwa viongozi,” alisema Sanga.

Anasema walipoingia bungeni licha ya kuwa wachache, walipaza sauti kwa masuala ya wanawake lakini pia kuonyesha kuwa wakipatiwa fursa ya uongozi wanaweza na wana umuhimu katika kuchangia maendeleo.

Anasema Mwalimu Julius Nyerere alisema Taifa lisilotambua wanawake ni sawa na taifa linalotembea mguu mmoja.

Sanga ambaye pia aliwahi kuwa mkurugenzi wa RTD, anasema jitihada zilizofanywa na baadhi ya wanawake kama Anna Abdallah, Anne Makinda, Mongella na Kate Kamba ambaye ni mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam, ziliwafanya waaminike na kushika nyadhifa ndani na nje ya Serikali.

Ubunge wa Taifa

Kuchaguliwa kwa wabunge hao wa Taifa ilikuwa ni hatua ya kukamilisha idadi ya wabunge 244 wa Bunge la Muungano, ikilinganishwa na wabunge 239 wa mwaka 1980/1985.

Pamoja na wabunge 169 wa kuchaguliwa na wananchi kutoka majimbo 15, wa Jumuiya za Wananchi na wengine 15 wa viti maalumu vya wanawake, kulikuwa na wabunge wengine 15 wa kuteuliwa na Rais, na wengine 25 ambao walikuwa wakuu wa mikoa yote ya Tanzania na watano waliotoka visiwani.

Majina yaliyopitishwa na Halmashauri Kuu ya CCM kugombea ubunge wa Taifa kupitia Jumuiya za Wananchi yalitajwa pia.

Waliopitishwa kupitia Jumuiya ya Washirika ni Phillip Mtaki Ndaki, Leonard Kaboboye, Mambo Musa, Catherine Mbiki, Shehe Hamad Hamisi na Elia Nyambo.

Kupitia Jumuiya ya Wazazi walikuwa Gibbons Mwaikambo, Meshack Maganga, Thabita Siwale, Ally Haji Ally, Ali Ameir Mohammed na Salome Nyiti.

Kutoka Jumuiya ya Vijana, walioteuliwa walikuwa Anne Makinda, Pascal Mabiti, Sukwa Said Sukwa, Khatib Hassan Khatib, Edward Lowassa na Venannce Ngulla.

Waliopitishwa kutoka Juwata ni Joseph Rwegasira, Daudi Mwakawago, Ismail Saleh Ismail, Zahran Mohammed Nassor, Mboni Cheka na Peter Nyamuhokya.

Kutoka UWT waliopitishwa ni Salama Khamis Islam, Yasmin Esmail, Hasham Aloo, Margareth Jia, Judith Jumaa, Lea Seme na Mwanamkhasi Soud.

Miongoni mwa hao 60 waliokuwa wakigombea ubunge wa Taifa, 30 walichaguliwa usiku wa Novemba 2, 1985 na kuapishwa siku iliyofuata.

Kati ya walioapishwa, 15 ni wa viti maalumu. Wabunge 15 wengine waliwakilisha jumuiya zao, lakini kwa mujibu wa Katiba, walikuwa wabunge wa Taifa na si wa jumuiya zilizopendekeza majina yao.

Matokeo yatangazwa

Katika matokeo yaliyotangazwa usiku wa manane wa kuamkia Jumapili ya Novemba 3, 1985, walioshinda ni pamoja na mawaziri watatu wa zamani ambao ni Mongella, Makinda na Daudi Mwakawago.

Mbunge wa zamani aliyeshindwa katika viti vya jumuiya alikuwa Kaboboye.

Katika viti hivyo vya Jumuiya za Wananchi, UWT haikupata kiti hata kimoja. Umoja wa Vijana ulipata viti vyote sita, Jumuiya ya Wazazi ilipata viti vitano, Jumuiya ya Washirika ilipata kiti kimoja na Juwata ilipata viti vitatu.

Walioshinda usiku huo kwa upande wa Jumuiya za Wananchi ni Makinda (Vijana) kura 170, Mwaikambo (Wazazi) kura 162, Sukwa Said Sukwa (Vijana) kura 159, Meshack Maganga (Wazazi) kura 139 na Siwale (Wazazi) kura 127.

Wengine ni Rwegasira (Juwata) kura 121, Mboni Cheka (Juwata) kura 119 na Lowassa (Vijana) kura 117, Venannce Ngula (Vijana) kura 114, Philip Ndaki (Washirika) kura 101 na Mabiti (Vijana) kura 96.

Pia walikuwamo, Khatib Hassan Khatib (Vijana) kura 90, Ali Ameir Mohamed (Wazazi) kura 89, Mwakawago (Juwata) kura 87 na Ally Haji Ally (Wazazi) kura 84.

Mwananchi limezungumza na Makinda ambaye anasema kazi ya kwanza ya wabunge baada ya kuchaguliwa ilikuwa wakifika bungeni wanafanya kazi ya kuwachagua wabunge wa Taifa na wale wa viti maalumu.

Makinda, ambaye ni mwanamke wa kwanza kuwa Spika wa Bunge la 10 kati ya 2010-2015, anasema kila jumuiya ilikuwa inapeleka majina ya wagombea ambao walipaswa kujieleza mbele ya wabunge ili wawapigie kura.

“Lakini uchaguzi ukifanyika, walikuwa hawachagui kwa kuangalia jumuiya unayotoka bali wanaangalia uwezo na kwa maana hiyo, UWT kila mwaka ilikuwa inakosa wawakilishi kutokana na aina ya wagombea iliyokuwa inawapeleka,” anasema Makinda.

Wabunge walioshinda viti maalumu pamoja na kura walizopata baada ya nafasi tano kupigiwa kura kwa upande wa Tanzania Bara na nafasi nyingine tano kupigiwa kura kwa upande wa visiwani pamoja na watano waliopitia kapu moja, kwa upande wa Tanzania Visiwani, Fatma Saidi Ally (alipata kura 143), Tatu Ali Abdallah (kura 122), Amina Salum Ali (kura 114), Thereza Olban Ali (kura 110) na Ashura Abeid Faraji (kura 105).

Tanzania Bara alikuwa Mongella (kura 98), Mosi Tambwe (kura 87), Zaituni Nyapili (kura 71), Meghji (kura 68), Dk Zainab Gama (kura 66).

Wabunge walioshinda kwa kura za kapu zilizowajumuisha wote ambao hawakupita kwa upande wa Tanzania Bara wala visiwani ni Amina Saad Ferizo (kura 71), Jito Ram (kura 70), Mwanamkuu Makame Kombo (kura 67), Corona Busongo (kura 66) na Lucy Lameck (kura 60).