Mbunge agoma kutoka studio, polisi wakimsubiri nje

Muktasari:

Mbunge huyo amedai hawezi kutoka ndani ya studio za Royal Media Service kwenda nje kwasababu kwanza hana uhakika kama waliopo nje wakimsubiri kumkamata ni polisi ama laa.

Dar es Salaam. Mbunge wa Kiharu nchini Kenya, Ndindi Nyoro amegoma kutoka ndani ya studio za Royal Media Services usiku Jumapili Septemba 8,  2019 wakati polisi wakidaiwa kumsubiri nje ya studio hizo ili wamkamate.

Mbunge huyo alidai hawezi kutoka ndani ya studio hizo kwenda nje kwasababu kwanza hana uhakika kama waliopo nje wakimsubiri kumkamata ni polisi ama laa.

“Siwezi kujipeleka nje ya kampuni ya Royal Media Services kwa sababu sijui kama wanaoningojea ni polisi. Mimi nalala hapa kwa kiti kwenye Royal Media Services”, amesema Ndindi Nyoro

Kuhusu kufuatwa na polisi katika studio hizo, mbunge huyo amesema, "Matukio ya leo yamenishangaza. Iwapo nina makossa, ningependa kujua ili nijisalimishe kwa polisi mimi mwenyewe."

Licha ya sababu za watu wanaodaiwa kuwa polisi kumsubiri nje ya studio hizo kwa lengo la kumkamata, Mbunge huyo amesema yeye kama mbunge wa Kiharu nchini humo ana haki ya kuzuru eneo lolote na watu wasifikirie watamtisha kwa sababu wazazi wake hawajulikani.

Mwanasheria wa mbunge huyo, Alice Wahome alikuwepo ndani ya studio hizo pamoja na mbunge huyo amehoji kwanini mbunge huyo amefuatwa kukamatwa usiku, wakati sio mhalifu.

Mwanasheria huyo ameongeza Ndindi Nyoro atalala katika studio hizo za Royal Media Services na kama polisi wanamuhitaji mbunge huyo basi yeye pamoja na wenzake watampeleka wenyewe katika kituo cha polisi kesho Jumatatu Septemba 9, 2019 mchana kweupe, kwasababu hawawezi kumkabidhi kwa watu wasiojulikana hususani kwa usiku huu.

Polisi nchini Kenya bado hawajaptikana kuzungumzia chochote kuhusu mbunge huyo.

Endelea kufuatilia Mwananchi kwa habari zaidi